Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_301026

Stanbic Bank Banner_201026

Tuesday, 3 November 2026

NMB YATENGA ZAWADI ZA SH. MILIONI 600 KWA WATEJA, MAGARI MATATU KUONGOZA KAMPENI YA ‘WEKA NA USHINDE’

Dar es Salaam; November 3, 2026 - Benki ya NMB imezindua kampeni ya Bonge la Mpango ‘Weka na Ushinde’, inayolenga kuhamasisha utamaduni wa kuweka akiba kwa kuwazawadia wateja wake zawadi zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 600.

Kampeni hiyo iliyoanza Novemba 1, 2026 na itakayodumu hadi Januari 31, 2027, inatoa fursa kwa wateja kushinda zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu, pikipiki na magari matatu, ikiwemo Toyota Land Cruiser la utalii na magari mawili aina ya Ford Ranger.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Novemba 3, 2026, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema kampeni hiyo imeandaliwa kama sehemu ya juhudi za benki hiyo kuwahamasisha Watanzania kujiwekea akiba huku wakipata nafasi ya kunufaika na zawadi mbalimbali.

Alisema kupitia droo 13 za kila wiki, jumla ya wateja 130 watajishindia Shilingi 100,000 kila mmoja, huku wateja wengine 30 wakipata Shilingi 500,000 kila mmoja kupitia droo za kila mwezi.

Mbali na zawadi hizo za fedha, zawadi kuu zitakuwa magari matatu, ambayo ni Toyota Land Cruiser moja lililokusudiwa kwa shughuli za utalii na Ford Ranger mbili.

AMCOS KUNUFAIKA NA KAMPENI

Katika kuunga mkono sekta ya kilimo na kuimarisha ushirikiano na vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS), Mponzi alisema kampeni hiyo pia imejumuisha vyama vya ushirika katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

Alieleza kuwa NMB imetenga zaidi ya pikipiki 20 kwa ajili ya kuvizawadia vyama vitakavyopitisha malipo ya zao la korosho kupitia benki hiyo katika msimu wa 2026/2027.

Hatua hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya mifumo rasmi ya kifedha katika malipo ya mazao na kuongeza fursa za ushirikiano kati ya benki na wadau wa sekta ya kilimo.

NMB YAHAMASISHA UTAMADUNI WA KUWEKA AKIBA

Kwa upande wake, Mkuu wa Matawi na Mauzo wa NMB, Donatus Richard, aliwahimiza Watanzania kutumia fursa ya kampeni hiyo kufungua akaunti na kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya malengo yao ya kifedha.

Alisema NMB inaendelea kuboresha huduma zake za kidijitali kupitia NMB Mkononi, inayowawezesha wateja kufanya miamala na kupata huduma mbalimbali za kibenki kwa urahisi kupitia simu zao za mkononi.

Aliongeza kuwa huduma hiyo inawawezesha pia wateja kupata mikopo ya hadi Shilingi milioni tano bila dhamana, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha.

Kupitia kampeni ya Bonge la Mpango ‘Weka na Ushinde’, NMB inaendelea kuhamasisha Watanzania kujenga nidhamu ya kuweka akiba huku ikiwapatia wateja wake fursa ya kunufaika na zawadi mbalimbali katika kipindi cha miezi mitatu ya kampeni hiyo.


Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari, uchambuzi na taarifa mbalimbali kuhusu sekta ya benki, biashara na fedha.

Tufuatilie katika mitandao ya kijamii:

LinkedIn | Facebook | Instagram | X (Twitter)








No comments:

Post a Comment