Dar es Salaam, Oktoba 29, 2026 – Airtel Tanzania imezindua mnara mpya wa mawasiliano katika eneo la Gongo la Mboto Markaz, jijini Dar es Salaam, unaotarajiwa kunufaisha zaidi ya wakazi 10,460 kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kidijitali.
Sambamba na uzinduzi huo, kampuni hiyo iliendesha zoezi la usafi wa mazingira lililowakutanisha wafanyakazi wake, viongozi wa serikali za mitaa na wanajamii, kwa lengo la kuhamasisha uwajibikaji wa pamoja katika kutunza mazingira.
Washiriki walishirikiana kukusanya taka na kusafisha maeneo yanayozunguka mnara huo, hatua iliyoonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na jamii katika kuboresha mazingira ya makazi.
Mnara huo ni sehemu ya uwekezaji unaofanywa na Airtel Tanzania katika kupanua na kuimarisha miundombinu ya mawasiliano ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya huduma za simu na teknolojia za kidijitali.
Uwekezaji huo unalenga kuwawezesha wakazi, vijana na wafanyabiashara kupata huduma bora za mawasiliano zinazoweza kurahisisha shughuli zao za kila siku na kuwafungulia fursa zaidi katika uchumi wa kidijitali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Bernard John, mkazi wa eneo hilo na mwakilishi wa Serikali ya Mtaa wa Markaz, aliipongeza Airtel Tanzania kwa uwekezaji huo, akieleza kuwa upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano utasaidia kufungua fursa zaidi kwa vijana na wajasiriamali.
Alisema mtandao wenye uhakika utarahisisha upatikanaji wa taarifa, kusaidia shughuli za biashara na kuwawezesha wananchi kutumia majukwaa ya kidijitali kutafuta fursa za ajira na kujiajiri.
Kwa wafanyabiashara wadogo, huduma imara za mawasiliano ni nyenzo muhimu katika kuwafikia wateja, kutangaza bidhaa na huduma, kuwasiliana na wasambazaji pamoja na kuratibu shughuli zao za kila siku.
Aidha, zoezi la usafi lililoambatana na uzinduzi huo limeonesha dhamira ya kampuni hiyo ya kuendelea kushirikiana na jamii katika masuala ya kijamii na kimazingira. Ushirikiano wa aina hiyo ni sehemu muhimu ya juhudi za kujenga jamii inayojali mazingira na kuhimiza maendeleo endelevu.
Kadiri jiji la Dar es Salaam linavyoendelea kukua, mahitaji ya huduma za mawasiliano yanaongezeka sambamba na upanuzi wa shughuli za kijamii na kiuchumi. Uzinduzi wa mnara huo wa Gongo la Mboto Markaz unaongeza juhudi za Airtel Tanzania za kusogeza huduma za mawasiliano karibu zaidi na wananchi na wafanyabiashara.
Kupitia uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano na ushirikiano na jamii, Airtel Tanzania inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kusogeza mawasiliano Kila Kona, huku ikiendeleza juhudi za kuhamasisha utunzaji wa mazingira na matumizi ya teknolojia katika kukuza fursa za kijamii na kiuchumi.
Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari, taarifa na uchambuzi kuhusu biashara, benki, fedha na maendeleo ya sekta mbalimbali.
Tufuatilie katika mitandao ya kijamii:
LinkedIn | Facebook | Instagram | X (Twitter)

No comments:
Post a Comment