Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_301026_111126

Stanbic Bank Banner_201026

Tuesday, 17 November 2026

SAVANNA TELECOM YAFIKISHA WATEJA 250,000 WA INTANETI YA FAIBA MAJUMBANI AFRIKA MASHARIKI

  • Kampuni imewekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 108 hadi sasa na kuchangia kutengeneza ajira zaidi ya 2,100, huku ikiongoza kwa sehemu ya soko la intaneti ya faiba majumbani nchini Uganda na Tanzania.
  • Savanna Telecom (Africa) Limited na mshirika wake FiberHome wanaendeleza dhamira ya pamoja ya kufanya huduma za intaneti ya kasi majumbani zipatikane kwa gharama nafuu barani Afrika.

CAPE TOWN, Afrika Kusini, Novemba 16, 2026: Wakati maandalizi yakiendelea kuelekea ufunguzi wa Maonesho ya Teknolojia ya Afrika (Africa Tech Festival – ATF), mkutano mkubwa zaidi wa sekta ya mawasiliano ya simu barani Afrika, utakaofanyika kuanzia Novemba 17 hadi 19 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Cape Town (Cape Town International Convention Centre), Savanna Telecom (Africa) Limited, kampuni mama yenye makao yake nchini Mauritius inayomiliki Savanna Fibre nchini Uganda, Tanzania na Kenya, imetangaza mafanikio makubwa katika shughuli zake pamoja na mpango kabambe wa kupanua miundombinu ya mawasiliano mwaka 2027.

Katika kipindi kifupi cha shughuli zake, Savanna imevuka idadi ya wateja 250,000 wanaotumia huduma ya intaneti ya kasi kupitia nyaya za nyuzinyuzi (fibre optic) majumbani nchini Uganda, Tanzania na Kenya. Mafanikio haya yamefikiwa kupitia miundombinu inayofikia zaidi ya makazi milioni moja katika maeneo ambayo huduma hiyo imefikishwa.

Ikiendeleza kasi hiyo ya ukuaji, kampuni imekamilisha usanifu wa kihandisi kwa ajili ya upanuzi zaidi wa miundombinu utakaowezesha huduma kufikia makazi mengine milioni moja ndani ya kipindi cha miezi 12 ya mwaka 2027. Mpango huo unawakilisha upanuzi mkubwa wa miundombinu ya mawasiliano katika Afrika Mashariki, huku sehemu kubwa ya uwekezaji huo ikielekezwa katika miji midogo na vitongoji ambavyo havijawahi kufikiwa na huduma za intaneti ya faiba kutoka kwa kampuni nyingine.

Kuweka Huduma za Intaneti Nafuu na Kupatikana kwa Wote Barani Afrika

Savanna ilianzishwa kwa imani moja kuu: upatikanaji wa intaneti unapaswa kuwa jambo la kawaida na la gharama nafuu kama kuwasha taa. Kwa muda mrefu, huduma za intaneti ya kasi barani Afrika zimejikita zaidi katika maeneo ya biashara mijini na vitongoji vinavyoishi watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha.

Savanna inalenga kuwafikia wananchi wengine ambao hawajafikiwa vya kutosha, wakiwemo wanafunzi wanaojisomea nyakati za usiku, wafanyabiashara wanaopokea malipo kupitia simu za mkononi, vituo vya afya vya vijijini vinavyopata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu walioko mijini, pamoja na kaya ambazo hazijawahi kuwa na huduma ya intaneti ya uhakika.

Upatikanaji wa huduma za intaneti ya kasi kwa gharama nafuu ni kichocheo cha moja kwa moja cha ukuaji wa uchumi. Huduma hizi huchochea ajira, kusaidia ukuaji wa biashara ndogo ndogo na kupanua fursa za upatikanaji wa huduma za kifedha za kidijitali, elimu na afya. Kwa kufanya hivyo, intaneti inachangia kuleta mabadiliko chanya katika jamii, kaya moja baada ya nyingine.

Ukuaji wa Haraka na Uongozi wa Soko

Ukuaji wa shughuli za Savanna unaonesha wazi ongezeko la mahitaji ya huduma za intaneti ya kasi kwa gharama nafuu.

  • Uwekezaji na Uzalishaji wa Ajira: Savanna imewekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 108 katika biashara yake hadi sasa. Baada ya kuanza shughuli zake nchini Uganda mwezi Februari 2024 ikiwa na wafanyakazi watatu pekee, kampuni hiyo sasa ina jumla ya wafanyakazi zaidi ya 2,100, wakiwemo walioajiriwa moja kwa moja na wale wanaotoa huduma kwa mikataba katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.
  • Miundombinu ya Mawasiliano: Kampuni tayari imejenga zaidi ya kilomita 16,000 za miundombinu ya nyaya za nyuzinyuzi za mawasiliano nchini Uganda, Tanzania na Kenya, huku ujenzi wa kilomita nyingine 8,000 ukiendelea.
  • Sehemu ya Soko: Kwa mujibu wa takwimu za ndani za kampuni, Savanna ndiyo kampuni inayokua kwa kasi zaidi katika sekta ya intaneti nchini Uganda, ikiwa na asilimia 56 ya soko la huduma ya intaneti ya faiba majumbani. Nchini Tanzania, kampuni inaongoza kwa asilimia 41 ya soko hilo. Savanna Fibre Kenya nayo inaendeleza mfumo huo wa upanuzi wa haraka wa intaneti kwa kupeleka huduma hatua kwa hatua katika kaunti mbalimbali.

Mpango wa kufikisha huduma za intaneti katika makazi mengine milioni moja mwaka 2027 unatarajiwa kuongeza zaidi ya mara mbili wigo wa huduma za Savanna. Hatua hiyo itaifanya kampuni kufikisha miundombinu yake katika jumla ya makazi zaidi ya milioni mbili, na hivyo kuimarisha msingi wa utekelezaji wa dira yake ya muda mrefu ya kujenga miundombinu ya intaneti itakayohudumia nchi mbalimbali barani Afrika.

Ufadhili Wapatikana kwa Ajili ya Upanuzi wa Intaneti Barani Afrika

Waanzilishi na wawekezaji wa Savanna wameahidi kuongeza mtaji kupitia uwekezaji wa hisa ili kugharamia mpango wa kuharakisha upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano ya intaneti ya faiba. Kampuni pia imefanikiwa kupata mikopo inayohitajika kuziba pengo la kifedha katika kugharamia upanuzi huo mkubwa wa mtandao.

Aidha, kampuni ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha zoezi lake la kwanza la kutafuta mtaji kupitia uuzaji wa hisa. Fedha zitakazopatikana zinatarajiwa kuharakisha utekelezaji wa mpango wa upanuzi wa intaneti kwa mwaka 2027 na kugharamia kuingia katika masoko mapya nje ya Afrika Mashariki.

Maelezo ya Uongozi wa Kampuni

Bw. Rashmi Shah, Mwenyekiti wa Savanna Telecom (Africa) Limited, alisema:

“Wakati tunaanzisha Savanna, tulijiuliza swali rahisi: Kwa nini familia inayoishi Gulu au Mwanza ilipe gharama kubwa zaidi na kusubiri muda mrefu kupata huduma ya intaneti ya uhakika ikilinganishwa na familia inayoishi Johannesburg au London?

“Huduma za mawasiliano si anasa tena; ni nyenzo inayomwezesha mtoto kujifunza, mfanyabiashara kupokea malipo na kituo cha afya kupata ushauri kutoka kwa mtaalamu. Dhamira yetu ni kufanya huduma za intaneti ya kasi zipatikane kwa urahisi na gharama nafuu, kwa kupeleka miundombinu ya nyaya za nyuzinyuzi katika jamii ambazo kwa muda mrefu zimekuwa hazipewi kipaumbele.

“Mafanikio ambayo timu zetu zimeyapata nchini Uganda na Tanzania ndani ya kipindi kifupi yanaonesha kile kinachowezekana. Mwaka 2027, tutapanua mfumo huu kwa kiwango kikubwa zaidi, na huu ni mwanzo tu wa safari yetu ya kuunganisha Afrika.”

Ushirikiano wa Kimkakati Tangu Kuanzishwa kwa Kampuni

Ukuaji wa haraka wa Savanna umechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano wake wa kimkakati na Wuhan FiberHome International Technologies Co., Ltd. (FiberHome), ambayo imekuwa mshirika wa kampuni tangu ilipoanzishwa.

FiberHome imekuwa ikiisaidia Savanna kupitia upatikanaji wa vifaa na teknolojia za kisasa za mawasiliano ya nyuzinyuzi (optical network), nyaya za nyuzinyuzi (fibre optic cables), pamoja na timu za wataalamu wa kiufundi na uhandisi wanaotoa usaidizi wa moja kwa moja katika maeneo ya utekelezaji wa miradi. Ushirikiano huu umeiwezesha Savanna kudumisha kasi ya juu ya ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano, kuanzia kwenye mtandao mkuu hadi kufikisha huduma moja kwa moja katika makazi ya wateja.

Bw. Naky Pei, Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Afrika wa Wuhan FiberHome International Technologies Co., Ltd., alisema:

“Afrika Mashariki ina fursa kubwa ya kupanua upatikanaji wa huduma za intaneti ya kasi na kukuza uchumi wa kidijitali. Kama mdau muhimu katika kuimarisha mawasiliano ya kidijitali kati ya China na Afrika, FiberHome inaendeleza kwa vitendo usambazaji wa miundombinu mipya ya kidijitali katika nchi mbalimbali za Afrika.

“Tunaamini kuwa ujenzi wa kisasa wa miundombinu ya mawasiliano ya nyuzinyuzi yenye ubora na inayohudumia watu wengi utaweka msingi imara wa mageuzi ya kidijitali na maendeleo jumuishi katika Afrika Mashariki.

“FiberHome inathamini ushirikiano wake wa muda mrefu wa kimkakati na Savanna na itaendelea kuunga mkono upanuzi wa mtandao wa Savanna kwa kuzingatia masharti ya kibiashara yaliyokubaliwa na mikataba ya kila mradi husika.”

Kutana na Savanna katika Maonesho ya Teknolojia ya Afrika

Timu ya uongozi wa Savanna itakuwepo katika Maonesho ya Teknolojia ya Afrika (Africa Tech Festival) kwa muda wote wa maonesho hayo, yatakayofanyika kuanzia Novemba 17 hadi 19, 2026, katika vyumba vya mikutano namba 1.71 na 1.72 (Meeting Suites 1.71 & 1.72).

Washirika wa sekta, kampuni nyingine za mawasiliano, wawekezaji na wadau wa ufadhili, pamoja na wanahabari, wanaalikwa kutembelea banda la kampuni ili kujadili mpango wa upanuzi wa intaneti kwa mwaka 2027 na fursa za ushirikiano wa baadaye.

Kuhusu Savanna Telecom (Africa) Limited

Savanna Telecom (Africa) Limited ni kampuni mama ya kundi la kampuni za mawasiliano lenye makao yake nchini Mauritius, linalomiliki Savanna Fibre nchini Uganda, Tanzania na Kenya. Savanna inajenga na kuendesha mitandao ya intaneti ya kasi kupitia nyaya za nyuzinyuzi, ikitoa huduma za intaneti kwa makazi, huduma za mawasiliano kwa biashara na huduma za simu za mkononi kupitia chapa zake za kibiashara, zikiwemo SavWiFi na SavGo.

Dhamira ya kampuni ni kufanya huduma za mawasiliano zipatikane kwa urahisi na gharama nafuu barani Afrika, ili kila mwananchi aweze kushiriki katika uchumi wa kidijitali.

Tovuti: savannafibre.com (Uganda) | savannafibre.co.ke (Kenya) | savannafibre.co.tz (Tanzania)

Kuhusu FiberHome

Wuhan FiberHome International Technologies Co., Ltd. (FiberHome) ni kampuni inayoongoza duniani katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Huduma na bidhaa zake zinajumuisha mitandao ya mawasiliano ya waya na isiyotumia waya, nyaya za nyuzinyuzi za mawasiliano, mitandao ya mawasiliano ya chini ya bahari, pamoja na mifumo ya nishati ya kidijitali.

Kupitia teknolojia na suluhisho zake, FiberHome inaziwezesha kampuni za mawasiliano duniani kujenga mitandao imara na ya kuaminika inayowaunganisha watu na biashara.

Tovuti: en.fiberhome.com

No comments:

Post a Comment