Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_301026_111126

Stanbic Bank Banner_201026

Thursday, 12 November 2026

TPA YAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA UWEKEZAJI WA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 60 KATIKA BANDARI ZA ZIWA VICTORIA


MWANZA - Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 60 katika kuboresha bandari za Mwanza Kaskazini, Bukoba na Kemondo, hatua inayolenga kuimarisha usafirishaji wa abiria na mizigo, kurahisisha biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi katika Ukanda wa Ziwa Victoria.

Shukrani hizo zimetolewa jijini Mwanza na Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Rosemary Ndesamburo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa. Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu ya usafiri wa majini na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Ndesamburo amesema maboresho ya Bandari ya Mwanza Kaskazini yalianza Mei 2023 kwa gharama ya Shilingi bilioni 18.6 na hadi sasa yamefikia asilimia 83 ya utekelezaji. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2026.

Ameeleza kuwa maboresho ya Bandari za Bukoba na Kemondo yamekamilika kwa asilimia 100, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri wa majini katika maeneo hayo.

Amesema uwekezaji huo una manufaa makubwa kwa wananchi na wafanyabiashara wa Ukanda wa Ziwa Victoria kwa kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, kuimarisha shughuli za biashara na kufungua fursa zaidi za kiuchumi.

Aidha, amesema TPA itaendelea kusimamia na kutunza miundombinu hiyo ili kuhakikisha inatumika kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa watumiaji wa bandari.

Kwa upande wao, baadhi ya abiria wanaotumia Bandari ya Mwanza Kaskazini wamesema maboresho yaliyofanyika yameongeza ubora wa huduma, hususan kwa kuboresha maeneo ya kupumzikia na kusubiri safari.

Wamesema mazingira mapya yamefanya kipindi cha kusubiri usafiri kuwa cha faraja zaidi, huku yakiboresha uzoefu wa abiria wanaotumia huduma za usafiri wa majini.

Uwekezaji huo unatarajiwa kuimarisha zaidi nafasi ya bandari za Ziwa Victoria katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kukuza biashara ndani na nje ya ukanda huo, hivyo kuongeza mchango wa sekta ya usafiri wa majini katika uchumi wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment