Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_301026

Stanbic Bank Banner_201026

Monday, 9 November 2026

TIRA NA ARiS WAPANDA MLIMA KILIMANJARO KUADHIMISHA MIAKA 30 YA SEKTA YA BIMA TANZANIA

KILIMANJARO, Novemba 6, 2026 – Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na kampuni ya ARiS Risk & Insurance Solutions wameanza safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 tangu sekta ya bima ilipofunguliwa kwa ushindani nchini Tanzania.

Safari hiyo pia inalenga kuadhimisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya bima, kutambua mchango wake katika ukuaji wa uchumi na kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa bima katika kulinda maisha, mali na shughuli za kiuchumi.

Wapandaji 22 Waanza Safari ya Kilimanjaro

Safari hiyo ilianza Novemba 6, 2026, kupitia Lango la Machame katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, ikiwa na washiriki 22 kutoka taasisi hizo mbili wanaolenga kufika kileleni mwa mlima huo wenye urefu wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari.

Kwa mujibu wa ratiba, safari ya kupanda mlima itafanyika kuanzia Novemba 6 hadi 11, huku washiriki wakitarajiwa kushuka kupitia Lango la Mweka Novemba 12, 2026.

Katika hafla ya kuwaaga washiriki iliyofanyika katika Lango la Machame, Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, aliwakabidhi bendera za taasisi hizo kabla ya kuanza safari.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi na wafanyakazi wa ARiS Insurance Brokers, menejimenti na wafanyakazi wa TIRA pamoja na wadau wengine wa sekta ya bima.

Ushirikiano na Ustahimilivu Katika Kukuza Sekta ya Bima

Safari hiyo imeandaliwa chini ya Kili Insurance Summit 2026 yenye kaulimbiu isemayo, “Miaka 30 ya Ubora katika Sekta ya Bima, Tukifikia Viwango Vipya kwa Pamoja – Kilele Kimoja cha Kipekee.”

Kupitia safari hiyo, waandaaji wanalenga kuonesha umuhimu wa maandalizi, ushirikiano, nidhamu na ustahimilivu katika kukabiliana na changamoto na kufikia malengo makubwa.

Maadili hayo yanaendana pia na misingi ya usimamizi wa vihatarishi na huduma za bima, ambazo husaidia watu binafsi na taasisi kujiandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababisha athari za kifedha.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Saqware alisema safari hiyo ni kielelezo cha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) kupitia TIRA na ARiS, huku ikitoa fursa ya kuelimisha umma kuhusu mafanikio ya sekta ya bima na malengo yake ya baadaye.

Alisema juhudi hizo pia zinaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, iliyozinduliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini.

“Kupanda Mlima Kilimanjaro kunatukumbusha kuwa kufikia malengo makubwa kunahitaji maandalizi ya kina, nidhamu na uwezo wa kushinda changamoto zinazojitokeza njiani. Hii pia ni misingi muhimu ya bima: kutambua vihatarishi mapema na kuchukua hatua za kujilinda dhidi ya athari zake za kifedha.

“Tunaipongeza ARiS Insurance Brokers kwa kuanzisha wazo hili la kampeni ya uhamasishaji kupitia utangazaji wa utalii wa ndani na safari ya kupanda mlima,” alisema Dkt. Saqware.

Aidha, aliwataka Watanzania kutumia huduma za wataalamu na washauri wa bima wanaponunua bidhaa mbalimbali za bima ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kuwasilisha madai.

Alisisitiza kuwa bima ni mkataba unaohitaji uelewa wa kutosha, hivyo ni muhimu kutumia huduma za madalali wa bima (Insurance Brokers) wenye ujuzi, sifa stahiki na usajili unaotambuliwa na TIRA.

Alisema matumizi ya wataalamu hao yanaweza kusaidia kupunguza migogoro na malalamiko yanayoweza kujitokeza wakati wa mchakato wa madai ya bima.

Pia alihimiza watu binafsi, wafanyabiashara na taasisi kutambua bima kama nyenzo muhimu ya kulinda maisha, mali na shughuli zao za kiuchumi.

ARiS Yasisitiza Umuhimu wa Uelewa wa Usimamizi wa Vihatarishi

Meneja Mkuu na Afisa Mkuu wa Bima wa ARiS Insurance, Bw. Christopher Siara, alisema Kili Insurance Summit 2026 inaakisi hatua na mabadiliko yaliyofikiwa na sekta ya bima nchini Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya kampuni hiyo, alisema ARiS inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa maandalizi na usimamizi wa vihatarishi katika maisha ya kila siku na shughuli za biashara.

Alieleza kuwa ARiS, ambayo ndiyo mwanzilishi wa Kili Insurance Summit, nayo inaadhimisha miaka 28 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa na uzoefu wa zaidi ya miongo miwili katika kutoa huduma za udalali wa bima na kuwa miongoni mwa kampuni zinazoongoza kwa sehemu ya soko nchini.

“Tumechagua kuadhimisha hatua hii muhimu kupitia safari inayoakisi aina ya huduma tunazotoa. Kama ambavyo kupanda mlima kunahitaji maandalizi, watu binafsi na biashara wanahitaji kupanga, kutambua vihatarishi vinavyoweza kujitokeza na kuchukua hatua za kujilinda dhidi ya athari zake.

“Kupitia safari hii, tunalenga kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa bima na kuonesha dhamira yetu endelevu ya kusaidia watu binafsi na biashara kusimamia vihatarishi na kujiandaa kwa siku zijazo,” alisema Bw. Siara.

Washiriki Wajiandaa kwa Safari ya Kilimanjaro

Timu ya wapandaji inajumuisha viongozi waandamizi na wafanyakazi kutoka TIRA na ARiS, huku asilimia 95 ya washiriki wakitarajiwa kupanda Mlima Kilimanjaro kwa mara ya kwanza.

Ushiriki wao unaonesha umuhimu wa maandalizi, nidhamu na ushirikiano katika kukabiliana na changamoto na kufikia malengo ya pamoja.

Kabla ya kuanza safari hiyo, washiriki walipitia ratiba maalumu ya mazoezi chini ya uongozi wa wataalamu, iliyojumuisha mazoezi ya kujenga utimamu wa mwili pamoja na matembezi ya milimani.

Maandalizi hayo yalihusisha mazoezi katika eneo la Pugu jijini Dar es Salaam na safari ya siku mbili katika Milima ya Uluguru, mkoani Morogoro, iliyofanyika Oktoba 24 na 25, 2026.

Katika safari hiyo ya Uluguru, washiriki walipanda hadi Kilele cha Bondwa chenye urefu wa mita 2,170 kutoka usawa wa bahari, kabla ya kushuka na kurejea Morogoro siku iliyofuata.

Zoezi hilo lililenga kuwajengea washiriki uzoefu na ustahimilivu unaohitajika katika safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro.

Ahsante Tours Washiriki Kuratibu Safari ya Kilimanjaro

Ahsante Tours, kampuni inayojihusisha na huduma za utalii na usimamizi wa safari, ndiyo waandaaji wa safari hiyo ya kupanda Mlima Kilimanjaro.

Kampuni hiyo inaratibu safari na kuhakikisha washiriki wanapata usimamizi na maandalizi yanayohitajika katika kipindi chote cha zoezi hilo, kuanzia maandalizi ya awali hadi kukamilika kwa safari.

Ushirikiano huo unaonesha umuhimu wa wadau wa sekta ya utalii katika kukuza na kuendeleza utalii wa ndani nchini Tanzania.

Aidha, safari hiyo inaweka mfano wa ushirikiano kati ya sekta ya bima na utalii katika kuadhimisha miaka 30 ya mafanikio ya sekta ya bima nchini, huku ikiitumia fursa hiyo kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, hususan Mlima Kilimanjaro.

Kuhusu TIRA

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha Sheria ya Bima, Sura ya 394, kwa lengo la kusimamia na kuendeleza sekta ya bima nchini.

Miongoni mwa majukumu yake ni kuhakikisha sekta ya bima inatoa huduma bora na zinazoaminika, pamoja na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kuhusu ARiS Group

ARiS Risk & Insurance Solutions Limited ni kampuni yenye makao yake nchini Tanzania inayotoa huduma za ushauri wa kitaalamu kuhusu bima na usimamizi wa vihatarishi kwa watu binafsi na taasisi.

Kampuni hiyo ilianza shughuli zake mwaka 1998 kama wakala mdogo wa mtu binafsi na baadaye kukua na kuwa miongoni mwa watoa huduma wakubwa wa udalali wa bima nchini Tanzania.

Kupitia ukuaji wake, ARiS imepanua shughuli zake nje ya Tanzania na kuanzisha kampuni tanzu katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, zikiwemo Kenya na Uganda.

Huduma zake kuu ni pamoja na ushauri na uandaaji wa programu za bima, bima ya afya na huduma za ustawi wa afya, mipango ya ufadhili wa malipo ya bima, usimamizi wa madai ya bima pamoja na mafunzo kuhusu sekta ya bima.


Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari, uchambuzi na taarifa mbalimbali kuhusu sekta ya benki, fedha, biashara na uchumi.

Tufuatilie katika mitandao ya kijamii:

LinkedIn | Facebook | Instagram | X (Twitter)


No comments:

Post a Comment