 |
Mkuu wa Idara ya Sekta ya Umma Benki ya NBC, Bi Joyce Maruba (kulia) akizungumza na baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) waliotembelea banda la maonesho ya huduma za benki hiyo lililopo kwenye viunga vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma unaponyika mkutano huo. Benki ya NBC ni mmoja wa wadhamini muhimu wa mkutano huo. |
 |
Mkuu wa Idara ya Sekta ya Umma Benki ya NBC, Bi Joyce Maruba (kulia) akizungumza na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bi Zainab Katimba wakati wa Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) unaofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. |
 |
Meneja Mahusiano Wateja Binafsi, Benki ya NBC Bi Zawadi Kanyawana (kulia) akisalimiana na baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) waliotembelea banda la maonesho ya huduma za benki hiyo lililopo kwenye viunga vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma unaponyika mkutano huo. |
 |
Mkuu wa Idara ya Sekta ya Umma Benki ya NBC, Bi Joyce Maruba (katikati) sambamba na wafanyakazi wengine wa benki hiyo wakiwa tayari kuwahudumia washiriki wa Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) kwenye banda la maonesho ya huduma za benki hiyo lililopo kwenye viunga vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma unaponyika mkutano huo. |
 |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na taasisi wadhamini wa Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma jana. |
Dodoma, 12 Machi 2025: Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya kushirikiana na halmashauri pamoja na mamlaka zote za tawala za mikoa na serikali za mitaa katika kuboresha ukusanyaji wa mapato kwa njia za kidijitali na kuongeza uwazi katika mifumo ya fedha ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan linalozitaka mamlaka hizo kukabiliana na upotevu wa mapato ya serikali.

Akizungumza jana jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT), Rais Samia alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, pamoja na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanasimamia vyema ukusanyaji wa mapato ili kubaini wahusika na kuchukua hatua.
Kufuatia agizo hilo la Rais Samia, Benki ya NBC ambayo ni mmoja wa wadhamini muhimu wa Mkutano wa ALAT na mdau wa huduma za kifedha kwa halmashauri hizo, kupitia kwa Mkuu wa Idara yake ya Sekta ya, Umma Bi Joyce Maruba alielezea mkakati wa ushirikiano na halmashauri hizo kuhakikisha agizo hilo la Rais linatekelezwa kwa urahisi zaidi kupitia huduma zake kisasa kwa njia ya kidigitali hususani katika ukusanyaji wa mapato hayo ya serikali.
“Agizo hili la Rais limekuja wakati muafaka ambapo ni hivi karibuni tu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alituzindulia rasmi huduma yetu kidijitali ya ‘NBC Kiganjani’ ambayo imeboreshwa zaidi ikiwa inalenga kuwarahisishia watanzania upatikanaji wa huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo malipo mbalimbali ya serikali na hivyo kuihakikishia serikali uhakika wa kupokea makusanyo yake kwa urahisi, uwazi na bila upotevu wowote.’’ Alisema Bi Maruba wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano huo.