Dar es Salaam: Benki ya Equity Tanzania imeungana na dunia kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani 2026 kwa kusherehekea na kutambua mchango mkubwa wa wanawake ambao ni wateja na pia wafanyakazi wa benki hiyo.
Maadhimisho hayo yalileta pamoja wanawake kutoka makundi mbalimbali, yakitoa fursa ya kutambua na kusherehekea mchango wao muhimu katika maendeleo ya biashara, jamii na uchumi kwa ujumla. Tukio hilo pia lilikuwa jukwaa la kukutana, kubadilishana mawazo na kusherehekea nguvu, uthabiti na ubunifu wa wanawake wanaoendelea kufanya mambo yawezekane kila siku.
Kupitia kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Wanawake Duniani, “Give to Gain,” Equity Bank Tanzania imewahimiza wanawake kutambua kuwa maendeleo ya kweli hupatikana pale wanapowekeza kwa wengine, wanapofungua milango ya fursa na kujenga mazingira ya ujumuishi kwa wote.
Benki hiyo pia imeeleza kujivunia mchango mkubwa wa wanawake katika safari yake ya mafanikio, kuanzia katika utoaji wa huduma kwa wateja, uendeshaji wa biashara hadi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya taasisi hiyo.
Katika mwezi huu wa kuadhimisha wanawake, Equity Bank Tanzania inaendelea kuwawezesha wanawake kifedha kupitia dirisha lake maalum la Mwanamke Plus, ambalo limebuniwa kusaidia kukuza uwezo wa kiuchumi wa wanawake.
Kupitia huduma hiyo, wanawake wanaweza kupata ufadhili wa mikopo kwa asilimia 100 kwa ajili ya biashara na makazi, pamoja na mafunzo na elimu ya kifedha bila malipo ili kuwajengea uwezo wa kusimamia vyema fedha na biashara zao.
Aidha, mpango huo unatoa mikopo ya ushonaji kwa masharti nafuu, inayolenga kusaidia wanawake wanaojihusisha na shughuli za ushonaji na ubunifu wa mavazi kukuza biashara zao.
Vilevile, huduma ya Mwanamke Bima inawawezesha wanawake kupata huduma muhimu za afya, ikiwemo vipimo vya afya ya uzazi, huduma baada ya kujifungua na vipimo vya homoni. Bima hii pia inatoa nafasi kwa wanawake kuwakatia bima watu wengine hata kama si ndugu wa damu, hivyo kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za afya.
Kupitia mipango hii, Equity Bank Tanzania inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuwawezesha wanawake na kutambua nafasi yao muhimu katika kuchochea maendeleo endelevu ya uchumi na jamii.










No comments:
Post a Comment