Benki ya KCB Tanzania imezindua huduma inayowawezesha Watanzania kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti zao za PayPal kwenda moja kwa moja kwenye akaunti za benki kupitia programu ya KCB Mobile App, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa mapato yanayotokana na kazi na biashara za kimataifa.
Huduma hiyo iliyozinduliwa Oktoba 9, 2026, inawawezesha wateja kuunganisha akaunti zao za PayPal na akaunti za KCB, kupokea malipo kutoka kwa wateja walioko nje ya nchi na kuhamisha fedha hizo kwenda kwenye akaunti zao za benki kwa kutumia simu za mkononi.
Ujumuishaji huo unalenga kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza katika upatikanaji wa mapato ya kimataifa, huku ukiwawezesha wateja kusimamia fedha zao kwa urahisi zaidi kupitia huduma za kidijitali.
KUFUNGUA FURSA KWA WAFANYAKAZI NA WAFANYABIASHARA WA MTANDAONI
Huduma hiyo inatarajiwa kuwa na manufaa kwa makundi mbalimbali yanayopata kipato kupitia shughuli za kimataifa, yakiwemo wafanyakazi wa kujitegemea (freelancers), wabunifu wa maudhui (content creators), waandishi, wataalamu wa teknolojia, wafanyabiashara wa mtandaoni pamoja na kampuni za utalii zinazopokea malipo kutoka kwa wateja wa nje ya nchi.
Kupitia huduma hiyo, makundi hayo yanaweza kutumia mfumo wa PayPal kupokea malipo ya huduma na bidhaa wanazotoa katika masoko ya kimataifa, kisha kuhamisha fedha hizo kwenda kwenye akaunti zao za KCB.
Akizungumzia uzinduzi wa huduma hiyo, Mkuu wa Huduma za Kifedha za Kidijitali wa KCB, Josina Njambi, amesema ushirikiano huo unalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha za kidijitali kwa wateja wanaofanya kazi na wateja kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Ameeleza kuwa huduma hiyo pia ni sehemu ya kampeni ya benki hiyo ya Ina-Make Cents, inayolenga kuongeza matumizi ya huduma za kibenki kupitia simu za mkononi.
USHINDANI KATIKA HUDUMA ZA MALIPO YA KIMATAIFA
Kuunganishwa kwa PayPal na KCB Tanzania kunaongeza chaguo kwa Watanzania wanaotafuta njia rahisi za kupokea mapato kutoka masoko ya kimataifa kupitia mifumo ya kidijitali.
Hatua hiyo inafuatia pia ushirikiano kati ya Vodacom Tanzania na PayPal uliotangazwa Mei 2026, unaolenga kupanua upatikanaji wa huduma za malipo ya kimataifa kupitia mfumo wa M-Pesa.
Kuongezeka kwa huduma hizo kunaashiria nafasi inayozidi kupanuka ya mifumo ya malipo ya kidijitali katika kuwaunganisha Watanzania na fursa za kiuchumi nje ya mipaka ya nchi.
Hata hivyo, wateja wanaotaka kutumia huduma hiyo wanashauriwa kufahamu gharama za miamala, viwango vya kubadilisha fedha za kigeni na masharti ya uhamishaji wa fedha kabla ya kufanya miamala.
Kwa ujumla, hatua ya KCB Tanzania kuunganisha PayPal na huduma zake za benki inaongeza njia za upatikanaji wa mapato ya kimataifa na kuunga mkono ukuaji wa biashara za kidijitali, uchumi wa kujitegemea na ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa dunia.
Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari, uchambuzi na taarifa mbalimbali kuhusu sekta ya benki, fedha, biashara na uchumi.
Tufuate kwenye mitandao ya kijamii:
LinkedIn | Facebook | Instagram | X (Twitter)

No comments:
Post a Comment