Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_170926_270926_101026

Absa Banner_170926_270926_101026

Stanbic Bank Banner_070826

Stanbic Bank Banner_070826

Monday, 12 October 2026

TANZANIA KUTUMIA FURSA ZA MIKUTANO YA IMF NA BENKI YA DUNIA, BANGKOK-THAILAND KIMKAKATI

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) akiongoza kikao cha ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika jijini Bangkok nchini Thailand, kuanzia tarehe 12 hadi 18 Oktoba 2026.

Bangkok, Thailand; Oktoba 11, 2026 - Tanzania imejipanga kutumia mikutano ya mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group) inayofanyika Bangkok, Thailand, kuanzia Oktoba 12 hadi 18, 2026, kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kuvutia rasilimali za maendeleo na kupanua fursa za uwekezaji nchini.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesisitiza kuwa ushiriki wa Tanzania katika mikutano hiyo ni wa kimkakati, ukilenga kuhakikisha nchi inanufaika na fursa za ufadhili, kuimarisha usimamizi wa fedha za nje na kuendeleza ajenda za maendeleo ya Taifa.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (katikati), akiongoza kikao cha ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika jijini Bangkok nchini Thailand, kuanzia tarehe 12 hadi 18 Oktoba 2026. Wengine katika picha ni Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil (Mb) (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (wa pili kulia), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida (kulia), Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba (kushoto).

Akizungumza katika kikao cha maandalizi ya ushiriki wa ujumbe wa Tanzania, Waziri Omar alisema mikutano hiyo itatoa fursa ya kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na viongozi wa taasisi hizo, wakiwemo makamu wa rais anayesimamia Kanda ya Kusini-Mashariki mwa Afrika pamoja na wakurugenzi watendaji, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa maendeleo.

Alieleza kuwa mojawapo ya maeneo muhimu yatakayopatiwa kipaumbele ni utekelezaji wa mzunguko wa 21 wa Mfuko wa Maendeleo wa Kimataifa (IDA 21), ambapo Serikali tayari imewasilisha orodha ya awali ya miradi inayotarajiwa kufadhiliwa na Benki ya Dunia.

“Moja ya maeneo muhimu yanayopewa kipaumbele ni utekelezaji wa mzunguko wa 21 wa IDA (IDA 21), ambayo Serikali imewasilisha orodha ya awali ya miradi inayotarajiwa kufadhiliwa na Benki ya Dunia na kuhakikisha kuwa miradi ya kipaumbele ya Taifa inapata ufadhili unaostahili,” alisema Waziri Omar.

Tanzania Kupanua Vyanzo vya Fedha za Maendeleo

Mbali na ushirikiano na Benki ya Dunia, Tanzania inaendelea kupanua wigo wa ushirikiano na wadau wengine wa maendeleo, huku ikiendeleza mazungumzo na mashirika ya ukadiriaji wa mikopo ya Moody’s na Fitch.

Jitihada hizo pia zinahusisha kuvutia wakopeshaji wapya ili kuongeza fursa za upatikanaji wa fedha na kuimarisha imani ya wawekezaji katika uchumi wa Tanzania.

Serikali imesisitiza kuwa ushiriki wake katika mikutano hiyo hauishii katika kuimarisha diplomasia ya kiuchumi, bali unalenga kupata matokeo ya moja kwa moja yatakayosaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Katika kufanikisha hilo, Serikali inalenga kuhakikisha fursa za ufadhili zinatumika ipasavyo na miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika. Aidha, pale itakapohitajika, Serikali itatafuta msaada wa kibajeti (General Budget Support – GBS) ili kukidhi mahitaji ya rasilimali kwa ajili ya programu mbalimbali za maendeleo.

Tanzania Kuimarisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Thailand

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ubalozi wa Heshima wa Tanzania nchini Thailand, Balozi wa Heshima, Mhe. Florean Rwehumbiza, alisema ofisi yake inaendelea kuimarisha diplomasia ya kiuchumi kupitia uhusiano wa kibiashara, utalii na huduma za afya kati ya nchi hizo mbili.

Alieleza kuwa ofisi hiyo imekuwa ikitangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia, zikiwemo Malaysia, Vietnam, Cambodia, Laos na Hong Kong.

Kwa mujibu wa Rwehumbiza, jitihada hizo zimechangia kushawishi mashirika ya ndege kuanzisha safari za moja kwa moja kuelekea Tanzania, hatua inayolenga kurahisisha usafiri kwa watalii na wafanyabiashara.

Watanzania Watumia Baht Milioni 150 kwa Matibabu Thailand

Katika sekta ya afya, Rwehumbiza alisema Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi za Afrika zinazotuma wagonjwa wengi nchini Thailand kwa ajili ya matibabu, akibainisha kuwa nchi hiyo imeshika nafasi ya pili barani Afrika kwa idadi ya wagonjwa wanaopelekwa huko.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa kuanzia Desemba 2025 hadi Juni 2026, Watanzania walitumia takribani baht milioni 150 za Thailand kwa huduma za matibabu nchini humo.

Jitihada za Kurahisisha Usafiri na Upatikanaji wa Visa

Katika upande wa usafiri, Rwehumbiza alisema Tanzania ina fursa maalumu kwa wasafiri wanaoelekea Thailand bila kuhitaji kadi ya chanjo ya homa ya manjano, mradi safari zao hazipiti Nairobi.

Aidha, alisema ofisi yake inaendelea kufuatilia uwezekano wa kuwezesha wasafiri kutoka Tanzania kupata visa wanapowasili Thailand (visa on arrival), hatua inayolenga kurahisisha zaidi safari na mwingiliano wa watu kati ya nchi hizo mbili.

Bunge Lapongeza Ushirikishwaji katika Mikutano

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Ali Hassan Omar (Mb), aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kulishirikisha Bunge katika mikutano hiyo ya mwaka ya IMF na Benki ya Dunia.

Alisema juhudi za Serikali za kuhakikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 unafanikiwa zinahitaji upatikanaji wa rasilimali fedha na mipango madhubuti ya kukuza uchumi.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil (Mb); Mjumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Mhe. Enock Zadock Koola (Mb); Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba; Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mipango, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida; Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba; pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na taasisi zake.

Mikutano hiyo inatoa fursa kwa Tanzania kuimarisha ushirikiano na taasisi za fedha za kimataifa, kutafuta rasilimali za kufadhili vipaumbele vya maendeleo na kujenga mazingira yanayovutia uwekezaji, sambamba na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.


Fuata Kitomari Banking & Finance Blog kupata habari na uchambuzi kuhusu sekta ya benki, fedha, biashara, uwekezaji na maendeleo ya uchumi.

Mitandao yetu ya kijamii:









No comments:

Post a Comment