Watoa Huduma Migodini Kupata Msukumo wa Mtaji Kupitia NMB, TAMISA
Dar es Salaam - Oktoba 7, 2026: Benki ya NMB na Tanzania Mining Industry Suppliers Association (TAMISA) zimesaini Makubaliano ya Ushirikiano ya miaka mitano yenye lengo la kuwawezesha wanachama wa TAMISA kupata huduma za kifedha, elimu ya fedha, ushauri wa biashara na mafunzo.
Kupitia makubaliano hayo, NMB itapokea na kutathmini miradi ya wanachama wa TAMISA na kutoa ufadhili kwa miradi itakayokidhi vigezo vya mikopo vya benki hiyo.
Ushirikiano huo pia unalenga kuwajengea uwezo wanachama wa TAMISA katika usimamizi wa fedha na utekelezaji wa kandarasi, hatua inayotarajiwa kuwawezesha kushiriki kwa ufanisi zaidi katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.
Akizungumza kuhusu ushirikiano huo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema changamoto kubwa inayowakabili watoa huduma wengi katika sekta ya madini ni upatikanaji wa mtaji.
Alisema NMB imeendelea kuimarisha huduma zake kwa sekta ya madini, ikiwemo kuanzisha dawati maalum kwa ajili ya kuwahudumia wasambazaji na watoa huduma katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Masoko na Uwekezaji ya TAMISA, Dk. Sebastian Ndege, alisema makubaliano hayo yatawasaidia wanachama wa chama hicho kuongeza uwezo wa kushindania zabuni, kupata mitaji na kushiriki kwa tija katika fursa zinazotokana na sekta ya madini.
Ushirikiano kati ya NMB na TAMISA unatarajiwa kuongeza fursa za upatikanaji wa fedha na huduma za kitaalamu kwa watoa huduma katika sekta ya madini, huku ukiimarisha ushiriki wa wafanyabiashara wa ndani katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Kuhusu Kitomari Banking & Finance Blog
Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari na uchambuzi kuhusu biashara, benki, fedha, uwekezaji na maendeleo ya sekta mbalimbali nchini Tanzania.
Tufuate:
LinkedIn | Facebook | Instagram | X (Twitter)



No comments:
Post a Comment