Dar es Salaam, Januari 30, 2026 – Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) nchini Tanzania limewapatia wanafunzi wajasiriamali 20 kutoka vyuo vikuu mbalimbali zawadi za fedha taslimu zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 70, kufuatia shindano la uwasilishaji wa mawazo bunifu ya biashara lililoandaliwa chini ya Awamu ya Pili ya programu ya Youth Ignite Student Founders Fellowship.
Programu hiyo inatekelezwa kupitia Programu ya FUNGUO ya UNDP Tanzania, kwa ufadhili wa pamoja wa Serikali ya Uingereza kupitia Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO), Umoja wa Ulaya (EU), pamoja na Serikali ya Finland.
Kukuza Ubunifu na Ujasiriamali wa Vijana
Hafla hiyo iliwakutanisha wanafunzi 30 kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini, waliowasilisha mawazo yao ya biashara mbele ya jopo la majaji. Mawazo hayo yalilenga kutoa suluhisho bunifu kwa changamoto za kijamii na kiuchumi, hatua inayoonesha ukuaji wa ubunifu na ujasiriamali miongoni mwa vijana wa Kitanzania.
Mbali na tuzo za fedha, washiriki wa programu walipatiwa msaada wa kitaalamu ikiwemo mafunzo ya maendeleo ya biashara, ushauri elekezi (mentorship), pamoja na maandalizi ya kuwafanya wawe tayari kuvutia wawekezaji.
Serikali Yapongeza Ushirikiano
Mgeni rasmi wa hafla hiyo, Dkt. Harun Makandi, Mkurugenzi Msaidizi wa Sayansi na Teknolojia kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, alisema programu hiyo inaendana kikamilifu na ajenda ya Serikali ya kukuza utafiti wenye tija kibiashara, ubunifu na ujasiriamali miongoni mwa vijana.
“Mpango huu unaunga mkono jitihada za serikali za kulea kizazi kipya cha wabunifu na wazalishaji wa ajira kutoka taasisi zetu za elimu ya juu. Unaakisi mwelekeo wa Tanzania wa kuunganisha sayansi, teknolojia na ujasiriamali katika maendeleo ya taifa,” alisema Dkt. Makandi.





