Foreign Exchange Rates

Equity Bank Advert_12 February 2026

CRDB Bank Advert_070325

Global Sanctions Compliance Masterclass

Friday, 27 February 2026

NMB YATOA SH12.4 BILIONI KWA WAFANYABIASHARA 6,011 KUPITIA MPANGO WA MIKOPO YA ASILIMIA 10

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Reuben Kwagilwa (kushoto), akisalimiana na Meneja Mwandamizi wa Biashara za Serikali wa NMB Bank Plc, Amanda Feruzi, alipowasili kufungua Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa Viongozi wa Jumuiya ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Ukanda wa Ziwa Victoria, uliofanyika jijini Dodoma. NMB ni mdhamini mkuu wa mkutano huo.

Dodoma – Jumla ya Sh12.4 bilioni zimetolewa kwa zaidi ya wafanyabiashara 6,011 kupitia mpango wa mikopo ya asilimia 10, huku wanufaika wakipatiwa pia elimu ya fedha na uongozi ili kuimarisha usimamizi na uendelevu wa biashara zao.

Takwimu hizo zimetolewa na Meneja Mwandamizi wa Idara ya Biashara za Serikali wa NMB, Amanda Feruzi, wakati wa mkutano wa Jumuiya ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa Ukanda wa Ziwa Victoria (LVRLAC) unaoendelea katika Ukumbi wa Jiji la Dodoma.


Fedha za Serikali Zilizotengwa kwa Makundi Maalum

Kwa mujibu wa Feruzi, fedha hizo ni sehemu ya Sh13 bilioni zilizotolewa na Serikali kwa NMB kwa ajili ya utekelezaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotengwa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Mpango huo unatekelezwa kwa mfumo wa majaribio katika Halmashauri sita ambazo ni:

  • Jiji la Dar es Salaam
  • Jiji la Dodoma
  • Manispaa ya Songea
  • Halmashauri ya Newala
  • Halmashauri ya Bumbuli
  • Halmashauri ya Itilima

Lengo la mfumo huo wa majaribio ni kupima ufanisi wa usimamizi wa mikopo hiyo kwa kushirikiana na taasisi ya kifedha, huku ukilenga kuongeza uwazi, nidhamu ya matumizi na marejesho.


NMB Yajivunia Uzoefu wa Ufadhili wa Miradi

Feruzi amesema NMB ipo tayari kuendelea kushirikiana na Jumuiya hiyo kama ambavyo imekuwa ikifanya kwa kufadhili mikutano yao kila mwaka na kushirikiana na Serikali katika miradi mbalimbali ya uwezeshaji wananchi.

Alieleza kuwa benki hiyo ina uzoefu katika mfumo wa Alternative Project Financing (APF), akibainisha kuwa imefanikiwa kutoa hati fungani, pamoja na taasisi nyingine, zenye thamani ya takribani trilioni moja.

NMB ilitajwa kuwa benki ya kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kutoa hati fungani ya jinsia (Jasiri Bond) pamoja na hati fungani ya uendelevu (Jamii Bond), hatua iliyovutia wawekezaji wa ndani na nje katika masoko ya mitaji ya kimataifa.

Aidha, alikumbusha kuwa NMB ilikuwa benki ya kwanza kuunganishwa katika mfumo wa malipo wa Serikali (GePG), jambo lililowezekana kutokana na uwekezaji mkubwa katika teknolojia, bidhaa na huduma za kifedha, na kusaidia kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.


Wito wa Kupanua Vyanzo vya Mapato

Akizungumza mbele ya wajumbe 42 kutoka mikoa ya Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Kagera, Feruzi aliwataka viongozi wa Serikali za Mitaa kutumia fursa ya kutafuta mitaji kutoka kwa wawekezaji ili kuzalisha vyanzo vipya vya mapato.

Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) pamoja na mifumo ya APF katika kutekeleza miradi ya kimkakati.

Miongoni mwa manufaa ya mbinu hizo ni:

  • Kuharakisha maboresho ya miundombinu
  • Kupunguza utegemezi wa bajeti kuu ya Serikali
  • Kuruhusu utekelezaji wa miradi kuanza mara moja
  • Kutumia uzoefu na mitaji ya sekta binafsi


Serikali Yasisitiza Uwajibikaji

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Reuben Kwagilwa, aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kote nchini kufanya kazi kwa ushirikiano na sekta binafsi huku akisisitiza kuitumia NMB katika kupata masuluhisho ya kifedha.

Alisema katika baadhi ya maeneo kumekuwepo na kulegalega katika matumizi ya fedha na kuonya kuwa Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayebainika kukiuka taratibu.

Ninyi Wakurugenzi hakikisheni mnalipa madeni ya Jumuiya kwa wakati ili muweze kujiendesha, na mnaweza kufanikiwa zaidi mkishirikiana na NMB katika mipango yenu,” amesema Kwagilwa.

Katika hatua nyingine, aliwataka Wakurugenzi kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati badala ya kusubiri viongozi wa juu kuja kuwasikiliza wananchi.


Mtazamo wa Kitomari Banking & Finance Blog

Hatua ya kusimamia mikopo ya asilimia 10 kupitia taasisi ya kifedha inaashiria mabadiliko muhimu katika namna programu za uwezeshaji zinavyotekelezwa nchini. Kuunganisha mitaji na elimu ya fedha kunaongeza uwezekano wa mikopo hiyo kuwa endelevu na yenye matokeo chanya kwa walengwa.

Iwapo usimamizi utaendelea kuwa wa kitaalamu, wenye uwazi na nidhamu ya marejesho, mfumo huu unaweza kuwa mfano wa kitaifa wa namna ushirikiano kati ya Serikali na sekta ya fedha unavyoweza kugeuza mikopo ya kijamii kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa ndani.



No comments:

Post a Comment