Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Stanbic Bank Banner_070826

Stanbic Bank Banner_070826

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

Thursday, 6 August 2026

TWENDE BUTIAMA YABADILISHWA JINA KUWA "NYERERE CYCLING TOUR", VODACOM YAZINDUA VODACOM COASTAL CLASSIC

Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando (katikati), akizungumza na waandishi wa habari kuhusu msimu mpya wa msafara wa Nyerere Cycling Tour (zamani Twende Butiama), utakaozinduliwa mwezi Oktoba sambamba na mashindano ya mbio za Vodacom Coastal Classic.
Wadau na washiriki wa Nyerere Cycling Tour (zamani Twende Butiama) wakipiga makofi kuashiria kufurahia uzinduzi wa mashindano ya mbio za Vodacom Coastal Classic.

DAR ES SALAAM - Agosti 6, 2026: Vodacom Tanzania Plc kwa kushirikiana na Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA) wametangaza rasmi kubadilishwa kwa jina la msafara wa baiskeli wa Twende Butiama na kuwa Nyerere Cycling Tour, hatua inayolenga kuenzi urithi wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere huku ikiupa mchezo wa baiskeli nchini mwelekeo mpya wa kimataifa.

Sambamba na mabadiliko hayo, Vodacom pia imezindua mashindano mapya ya Vodacom Coastal Classic, mbio za kilomita 109 zinazotarajiwa kuwa moja ya mashindano makubwa ya baiskeli nchini na kuvutia washiriki kutoka Tanzania, Afrika Mashariki na mataifa mbalimbali duniani.

Tangazo hilo limetolewa leo, Agosti 6, 2026, jijini Dar es Salaam.

Miaka 10 ya Kuendeleza Elimu Kupitia Baiskeli

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016, msafara huo umekuwa ukitumia mchezo wa baiskeli kama chombo cha kuhamasisha maendeleo ya elimu kwa kuenzi maono ya Mwalimu Nyerere ya kutoa fursa sawa kwa kila mtoto.

Kupitia kampeni hiyo, zaidi ya shule 107 zimefikiwa huku zaidi ya wanafunzi 75,000 wakinufaika na ujenzi wa madarasa jumuishi, miundombinu ya vyoo pamoja na upatikanaji wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Vodacom Tanzania Foundation ilianza kushirikiana na CHABATA kufadhili msafara huo miaka minne iliyopita, ambapo katika kipindi hicho ushiriki umeongezeka mara nne na kuvutia waendesha baiskeli kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Nyerere Cycling Tour Kuanza Oktoba

Msafara wa mwaka huu utafanyika kuanzia Oktoba 5 hadi 14, 2026, ukianzia Bagamoyo kuelekea Butiama.

Kwa mujibu wa waandaaji, kubadilishwa kwa jina kuwa Nyerere Cycling Tour kunaakisi dhamira ya kuendelea kuhifadhi urithi wa Mwalimu Nyerere huku wakijenga mashindano yatakayokua na kutambulika kimataifa.

Vodacom Coastal Classic Kuleta Ushindani wa Kimataifa

Mbio mpya za Vodacom Coastal Classic zitafanyika kwa mara ya kwanza Jumapili, Oktoba 4, 2026, siku moja kabla ya kuanza kwa Nyerere Cycling Tour.

Mashindano hayo yataanzia Dar es Salaam, kuelekea Makurunge mkoani Pwani na kuhitimishwa katika eneo la kihistoria la Old Boma, Bagamoyo, yakikamilisha safari ya kilomita 109.

Kuanzia mwaka huu, mashindano hayo yatafanyika kila mwaka katika Jumapili ya kwanza ya mwezi Oktoba.

Zaidi ya washiriki 400 kutoka Tanzania na nchi mbalimbali duniani wanatarajiwa kushiriki katika toleo la kwanza.

Vodacom: Tunataka Kuibua Vipaji vya Watanzania

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, alisema lengo kuu ni kukuza mchezo wa baiskeli na kuwapa Watanzania fursa ya kushindana katika viwango vya kimataifa.

"Tunataka kukuza mchezo huu. Kila siku tunaona waendesha baiskeli kwenye barabara zetu, aidha wakiwa wataalamu au washiriki wa kawaida. Hakuna sababu kwa nini Abella kutoka Mwanza au Saidi kutoka Shinyanga wasiweze kushindana hapa Tanzania na kwenye majukwaa ya kimataifa. Wanachohitaji ni vifaa sahihi na mafunzo sahihi. Vodacom Coastal Classic inalenga kuhamasisha na kuwapa motisha Watanzania wengi zaidi kuingia katika mchezo huu," alisema Kamando.

CHABATA: Mwanzo wa Safari Mpya

Kwa upande wake, Mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour, Gabriel Landa, alisema mashindano hayo sasa yamevuka kuwa msafara wa baiskeli pekee na kuwa jukwaa la kuendeleza maono ya Mwalimu Nyerere.

"Nyerere Cycling Tour imekuwa zaidi ya msafara wa baiskeli. Ni kuhusu kuendeleza maono ya Mwalimu Nyerere ya heshima na fursa sawa kwa kila Mtanzania. Kubadilisha jina la mashindano haya kwa heshima yake, sambamba na kuanzisha mbio za kiwango cha kimataifa za Vodacom Coastal Classic, ni mwanzo wa safari mpya. Tunajenga jukwaa ambalo vipaji vya Watanzania vinaweza kuibuka na kuvutia waendesha baiskeli kutoka kote duniani kushiriki," alisema Landa.

Tarehe Muhimu

  • Vodacom Coastal Classic (Kilomita 109): Jumapili, 4 Oktoba 2026 – Dar es Salaam, Makurunge hadi Old Boma, Bagamoyo.
  • Nyerere Cycling Tour: 5–14 Oktoba 2026 – Bagamoyo hadi Butiama.

Kuhusu Nyerere Cycling Tour

Awali ikijulikana kama Twende Butiama, Nyerere Cycling Tour inalenga kuenzi urithi wa Mwalimu Julius K. Nyerere kwa kuhamasisha upatikanaji wa elimu bora na jumuishi nchini. Kupitia kampeni hiyo, zaidi ya shule 107 zimewezeshwa huku wanafunzi zaidi ya 75,000 wakinufaika na mazingira bora ya kujifunzia.

Kuhusu Vodacom Tanzania Foundation

Vodacom Tanzania Foundation ni taasisi ya kijamii ya Vodacom Tanzania Plc inayotumia teknolojia na ushirikiano na wadau mbalimbali kuboresha maisha ya Watanzania, ikijikita katika sekta za elimu, afya na ujumuishaji wa kijamii. Foundation imekuwa mshirika mkuu wa Nyerere Cycling Tour kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.

Mwanzilishi wa Twende Butiama, Gabriel Landa, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu msimu mpya wa Nyerere Cycling Tour (zamani Twende Butiama), utakaozinduliwa mwezi Oktoba.
Wadau wa Nyerere Cycling Tour (zamani Twende Butiama) wakisikiliza kwa makini maelezo kuhusu msimu mpya wa msafara huo na uzinduzi wa mashindano ya Vodacom Coastal Classic, yatakayofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Chanzo: Vodacom Tanzania Plc.

Kwa mawasiliano zaidi;

Deborah Kaluzi
Barua pepe: deborah.kaluzi@vodacom.co.tz
Simu: +255 754 710 200


Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari za uhakika kuhusu biashara, benki, uwekezaji, uchumi na maendeleo ya sekta mbalimbali nchini Tanzania.

No comments:

Post a Comment