Foreign Exchange Rates

Equity Bank Advert_12 February 2026

CRDB Bank Advert_070325

Wednesday, 1 April 2026

BENKI YA KCB YASHIRIKIANA NA MIXX BY YAS KUTOA MIKOPO YA KIDIGITALI KWA MAWAKALA

Mkurugenzi Mtendaji wa KCB Bank Tanzania (kushoto), Cosmas Kimario, na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas, Angelica Pesha (kulia), wakiwa kwenye uzinduzi huo.

Dar es Salaam, 31 Machi 2026 – Benki ya KCB Tanzania imezindua rasmi ushirikiano wa kimkakati na Mixx by Yas unaolenga kutoa mikopo ya kidigitali kwa mawakala, hatua inayotarajiwa kubadilisha tasnia ya huduma za kifedha na kupanua upatikanaji wake nchini kote. Uzinduzi huo umefanyika katika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam.

Ushirikiano huu unaunganisha nguvu ya kifedha ya KCB pamoja na mtandao mpana wa mawakala wa Mixx by Yas wenye zaidi ya wanachama 200,000. Kupitia muunganiko huu, taasisi hizi mbili zinajenga mfumo thabiti unaolenga kuwafikia Watanzania wengi zaidi, hasa katika maeneo ambayo huduma za kifedha bado hazijafika kwa kiwango kinachohitajika.

Kiini cha ushirikiano huu ni uzinduzi wa huduma ya Bustisha Wakala, suluhisho la mkopo wa muda mfupi (overdraft) lililobuniwa kuwapatia mawakala ukwasi wa haraka na wa uhakika. Hatua hii inalenga kuondoa changamoto za upungufu wa fedha taslimu ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikikwamisha utoaji wa huduma kwa wateja.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa KCB Bank Tanzania, Cosmas Kimario, alisema:

Mawakala ni zaidi ya watoa huduma—wao ni daraja muhimu linalounganisha mamilioni ya Watanzania na huduma za kifedha. Kupitia Bustisha Wakala, tunawapa uwezo wa kupata fedha pindi wanapozihitaji, tukihakikisha huduma zisizokatika na fursa endelevu za kiuchumi.”

 

Tangu kuanza kwa majaribio ya huduma hii tarehe 27 Februari 2026, zaidi ya mawakala 7,000 tayari wamefaidika na mpango huo. KCB ina matarajio ya kuona huduma hii ikikua kwa kasi kupitia mtandao wa Mixx by Yas, hatua itakayochochea zaidi ushirikishwaji wa kifedha na kukuza biashara ndogo ndogo nchini.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas, Angelica Pesha, alieleza kuwa uwezeshaji wa mawakala ni msingi wa mafanikio ya mfumo wa kifedha wa kidigitali:

Tunapowawezesha mawakala wetu kupata mikopo ya papo hapo, tunaimarisha uwezo wao wa kuhudumia wateja, kuongeza uaminifu, na kukuza biashara zao. Bustisha Wakala si bidhaa tu bali ni kichocheo cha ustahimilivu wa kiuchumi na fursa katika ngazi ya chini.”

Mbali na hilo, KCB Bank Tanzania inaendelea kuhimiza matumizi ya huduma zake za kidigitali kupitia programu ya KCB Mobile TZ App, inayopatikana kwenye App Store na Play Store, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuimarisha huduma za kifedha kwa njia ya teknolojia.

Ushirikiano huu unaashiria hatua muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi jumuishi wa kidigitali, ambapo mawakala wanawezeshwa si tu kutoa huduma, bali pia kukua kama nguzo muhimu ya maendeleo ya kifedha na kijamii.

No comments:

Post a Comment