Benki ya NMB imeendeleza jitihada zake za kujenga nguvu kazi yenye ujuzi na maarifa ya kisasa katika sekta ya fedha nchini kwa kusaidia mafunzo ya kitaaluma na utalaamu kwa vijana 100 kupitia mpango maalumu wa Graduate Banker Readiness Programme (GBRP) unaotekelezwa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Kupitia mpango huo, NMB kwa kushirikiana na UDSM, inatoa mafunzo ya kitaaluma yanayochanganya nadharia na vitendo, yakilenga kuwajengea washiriki uelewa mpana na wa kina wa sekta ya fedha. Kundi la nne la washiriki, kama ilivyokuwa kwa makundi yaliyotangulia, limehitimu Ijumaa iliyopita baada ya kukamilisha mafunzo hayo.
Akizungumza kabla ya kuwakabidhi wahitimu vyeti, Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa NMB, Erica Hanson, alisema mpango huo ni matokeo ya ushirikiano wa kimkakati kati ya benki hiyo na UDSM kupitia Shule ya Biashara ya chuo hicho, ukiwa na lengo la kuunganisha elimu ya darasani na uhalisia wa kazi za benki.
Bi. Hanson alibainisha kuwa washiriki wamepata mafunzo katika maeneo muhimu ikiwemo uchambuzi wa kifedha, uendeshaji wa benki, usimamizi na udhibiti wa vihatarishi, uzingatiaji wa kanuni, utoaji bora wa huduma kwa wateja pamoja na mifumo ya benki ya kidijitali.
“Kuhitimu kwa vijana hawa leo kunaongeza nguvu katika dhamira ya NMB ya kuendelea kujijenga kama mwajiri pendwa nchini, jambo ambalo limethibitishwa kwa kutunukiwa Tuzo ya Mwajiri Bora kwa miaka mitatu mfululizo. Haya yote ni matokeo ya uwekezaji wa makusudi katika watu, vipaji na maendeleo endelevu ya rasilimali watu,” alisema Bi. Hanson.
Kwa upande wa wanataaluma kutoka UDSM, wakiongozwa na Mkuu wa Kitivo cha Biashara, Omari Mbura, walisema mpango huo unachangia kupunguza pengo la ujuzi sokoni kwa kuhakikisha wahitimu wanakidhi mahitaji halisi ya tasnia ya fedha.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Kituo cha Utafiti wa Benki na Huduma za Kifedha (CBFSR), Esther Ishengoma, pamoja na Mkuu wa Idara ya Fedha, Thobias Swai, ambao walisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano kati ya vyuo vikuu na sekta binafsi ili kukuza wahitimu wenye ushindani.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Marcelina Evarist aliishukuru NMB kwa kufadhili na kuwezesha mpango huo kabambe uliowajengea uwezo na kuongeza uelewa wao wa kina kuhusu sekta ya fedha.
Kupitia GBRP, NMB inaendelea kuthibitisha nafasi yake kama mdau muhimu katika maendeleo ya rasilimali watu nchini, huku ikiwekeza katika kizazi kipya cha wataalamu wa sekta ya benki na huduma za kifedha.
No comments:
Post a Comment