
Kama ilivyokuwa kwa misimu ya awali, mchakato wa Umebima wa mwaka huu ni wa kitaifa na lengo lake kuu ni kuunga mkono ajenda ya taifa ya bima kwa wote.

Wakizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika Mwanjelwa-Kabwe, maafisa wa NMBwalisema kampeni hiyo inashabiiana na malengo ya serikali ya kuongeza uelewa wa masuala ya bima na kuongeza matumizi ya huduma zake.

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Bw. Filbert Mponzi, alisema kwa sasa uelewa wa bima nchini ni mdogo sana na kusisitiza kuwa bado kuna kazi kubwa kuhakikisha watu wengi zaidi wanakata bima kujikinga na majanga ili kuboresha kiwango cha asilimia 1.6 cha kusambaa kwa huduma hizo.

Aidha, alibainisha kuwa kimsingi kampeni ya Umebima imejikita kuyakabili mapungufu hayo kwa kuuelimisha umma kuhusu umuhimu na faida za bima hasa kwa wale ambao hawajafikiwa na huduma hiyo au kufahamu uwepo wake.

Bw Mponzi alisema tangu NMB ipate leseni ya uwakala wa bima mwaka 2020 imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia kuongeza uelewa wa bima nchini na sasa hivi watu wengi wanazidi kukata bima na kuwa na kinga ya uhakika dhidi ya majanga.















































