Kampuni ya huduma za malipo ya Pesapal imeanzisha huduma mpya ya kusaidia kusimamia uendeshaji wa vituo vya mafuta na mauzo ya nishati nyingine unaotumia teknolojia za kisasa na kufanya kazi kiotomatiki.
Viongozi wa kampuni hiyo wamebainisha kuwa lengo kuu la suluhisho hilo ni hasa kuwasaidia wamiliki wa vituo hivyo kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi katika biashara ya reja reja ya mafuta.
Kupitia teknolojia hii, Pesapal imejipanga kuhakikisha hadi mwisho wa mwaka huu vituo 100 vya mafuta kwenye masoko ya Tanzania, Kenya na Uganda vitakuwa vinatumia mfumo huu mpya.
Kitaalamu na kibiashara suluhisho hili linajulikana kama 'Pesapal Forecourt Management Solution (PFMS)'.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam, kampuni hiyo imesema PFMS ndilo jibu la takwa la wenye vituo vya mafuta la kuwa na muunganiko wa vifaa vya mauzo usiokuwa na hitilafu yoyote.
Pia PFMS ina uwezo mkubwa wa kusimamia na kufuatilia kwa karibu sana jinsi uuzaji mafuta unavyofanyika. Uwezo huu ndio unaipa suluhisho hii sifa ya kupunguza gharama za uendeshaji lakini pia kusaidia kuondokana na ulaghai huku ikiboresha namna wateja wanavyohudumiwa kwa mawanda mapana ya koungeza mauzo.
“Suluhisho ya PFMS inawezesha wamiliki wa vituo vya mafuta kuweza kufuatilia na kusimamia bila kuwepo vituoni mauzo ya gesi na mashine za kujazia mafuta, mfumo wa vipimo vya matenki, bodi za bei na jinsi malipo yanavyofanyika,” Pesapal ilibainisha katika taarifa yake.
Mwezi Februari mwaka jana Pesapal ilipata kibali cha kutoa suluhisho jumuishi za malipo kwa vituo vya mafuta kutoka kwa jukwaa la kimataifa la viwango la IFSF. Taasisi hii ni jumuiya ambayo imejikita zaidi kufanikisha kuwepo teknolojia za viwango vya kimataifa kwa ajili ya kusaidia kuboresha uendeshaji wa vituo vya mafuta ya magari na nishati nyingine.
Akizungumza hivi karibuni kwenye utambulisho wa PFMS katika masoko ya ukanda huu, Afisa Mtendaji Mkuu wa Pesapal Limited, Bw Agosta Liko, alibainisha umuhimu wa kuufanya mchakato mzima wa usimamizi wa mafuta kuwa wa kiotomatiki.
Uwekezaji huu, kiongozi huyo alifafanua, hutengeneza mazingira mathubuti katika sekta ya reja reja ya mafuta na kuimarisha eneo mtambuka la biashara hiyo kwa hasa kupunguza gharama za uendeshaji na kuimarisha huduma kwa wateja.
Bw Liko alisema matumizi ya suluhisho ya PFMS ili kusaidia zaidi kurahisisha malipo kwenye vituo vya kuuzia mafuta yatafanyika kwa ushirikiano wa kimkakati kati ya Pesapal na wamiliki wa vituo husika.
“Katika nyanja inayobadilika kwa kasi kama hii ya usimamizi wa kuuza mafuta reja reja, zinahitajika suluhisho ambazo ni za kisasa na zinazoanzisha mienendo mipya ya kufanya mambo,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Meneja wa Pesapal Tanzania, Bi Bupe Mwakalundwa, pamoja na suluhisho yao kuwa bunifu zaidi pia inazingatia sana kuwapa wenye biashara ya vituo vya mafuta uwezo wa kuboresha huduma kwa wateja na kuwahudumia watu wengi kwa ufanisi mkubwa.
“Hii suluhisho uwapa wateja fursa ya kufanya manunuzi yao kwa mkupuo wa muamala mmoja, huku wasimamiaji wa vituo vya mafuta wakiwezeshwa kuidhinisha miamala haraka na kwa usalama,” Bi Mwakalundwa alinukuliwa katika taarifa ya Pesapal kwa vyombo vya habari.
Pesapal Limited ni kampuni kinara wa huduma za malipo inayohusika na zana za kuchakata malipo zikiwemo zile za kidijitali na kimtandao hususani kwa ajili ya mashirika ya kibiashara na taasisi nyingine zenye mwelekeo huo.
Pesapal ilianzishwa mwaka 2009 na kwa sasa hivi inafanya biashara katika nchini sita za Kiafrika ambazo ni pamoja na Zambia, Zimbabwe and Malawi.
Kwa hapa nchini, imekuwepo tangu Julai mwaka jana baada ya kupata idhini ya Benki Kuu kutoa huduma za malipo yasiyohusisha pesa taslimu chini ya Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya Mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment