Foreign Exchange Rates

Equity Bank Advert_12 February 2026

CRDB Bank Advert_070325

Global Sanctions Compliance Masterclass

Friday, 13 February 2026

CRDB BANK FOUNDATION YAZINDUA "GO GREEN NA IMBEJU", VIJANA KUPATA MITAJI HADI SH. MIL. 500

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (katikati), akiwa na viongozi wengine wa Serikali, Bunge na Benki ya CRDB, wakipata maelezo kutoka kwa mwanzilishi wa kampuni ya Aquafresh iliyoshiriki katika maonesho ya biashara changa bunifu za vijana, wakati wa hafla ya uzinduzi wa programu ya Go Green na IMBEJU inayolenga kuwezesha biashara na bunifu za kijani za vijana kama sehemu ya kuchochea uchumi wa kijani kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (katikati), akipokelewa na kikundi cha ngoma za asili wakati alipowasili katika uzinduzi wa programu ya Go Green na IMBEJU inayolenga kuwezesha biashara na bunifu za kijani za vijana kama sehemu ya kuchochea uchumi wa kijani kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Wengine pichani ni, kushoto kwake, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Daniel Sillo; Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori; na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.

Dodoma, 12 Februari 2026 – Waziri wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo, ameipongeza CRDB Bank Foundation na Benki ya CRDB kwa kuanzisha programu ya Go Green na IMBEJU, akisema ni hatua ya kimkakati inayounganisha ajenda ya Serikali ya uchumi wa kijani na uwezeshaji wa vijana.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma, Prof. Mkumbo alisema mpango huo unaendana kikamilifu na Dira ya Taifa 2050, ambayo imeweka mkazo katika uchumi jumuishi, shindani na himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi huku ikitambua vijana kama msingi wa mafanikio ya Taifa.

Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuwawezesha vijana kiuchumi, kukuza uchumi wa kijani na kujenga mifumo imara ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Miradi ya vijana inayolinda mazingira kama tunavyoiona leo ni utekelezaji wa moja kwa moja wa Dira ya Taifa 2050 kwa vitendo,” alisema Prof. Mkumbo.

Alisisitiza kuwa ushiriki wa sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha mawazo bunifu ya vijana yanageuzwa kuwa biashara endelevu zenye ajira na tija kwa Taifa.


Mitaji Nafuu Kuanzia Shilingi 500,000 hadi Milioni 500

Programu ya Go Green na IMBEJU inalenga kuwawezesha vijana wenye miradi bunifu inayohusiana na:

  • Kilimo himilivu
  • Nishati safi na jadidifu
  • Teknolojia za maji
  • Usimamizi wa taka
  • Uhifadhi wa mazingira
  • Ubunifu wa kidijitali

Kupitia dirisha hili, vijana wanaweza kupata mitaji nafuu kuanzia Shilingi 500,000 hadi Shilingi milioni 500, kulingana na ukubwa na mahitaji ya mradi.


Daraja Kati ya Fedha za Tabianchi na Ubunifu wa Vijana

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema mpango huo ni daraja kati ya fedha za kimataifa za tabianchi na vijana wabunifu ambao mara nyingi hukosa dhamana au historia ya mikopo inayohitajika katika mifumo ya kawaida ya kifedha.

Kupitia Go Green na IMBEJU tunaamini vijana wengi zaidi watafikiwa, kuandaliwa na kuwezeshwa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kijani. Huu ni muunganiko wa kimkakati kati ya ufadhili wa kimataifa wa tabianchi na ubunifu wa vijana wa Tanzania,” alisema Nsekela.

Alibainisha kuwa kupitia programu ya TACATDP yenye thamani ya Dola milioni 200 kwa ushirikiano na Green Climate Fund (UN GCF), tayari zaidi ya Shilingi bilioni 100 zimetolewa kuwafikia takribani wanufaika 600,000 kote nchini.


Maombi Kidijitali Kupitia FursaHub

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, alisema maombi ya Go Green na IMBEJU yatafanyika kidijitali kupitia jukwaa la FursaHub kwa kushirikiana na NEDC.

Maombi ya Go Green na IMBEJU yatafanyika kidijitali kupitia mfumo wa FursaHub kuanzia tarehe 12 Februari hadi 11 Machi 2026. Mfumo huo utachuja maombi kulingana na vigezo vilivyowekwa, na yale yatakayokidhi masharti yatawasilishwa kwenye kamati ya wataalamu kwa tathmini ya kina,” alisema Mwambapa.

Aliongeza kuwa waombaji watakaofaulu wataalikwa kushiriki mafunzo maalum ya biashara na ubunifu kupitia Kituo cha Ubunifu cha CRDB Bank Foundation kabla ya kupewa uwezeshaji wa kifedha.

Aidha, miradi itakayofanya vizuri zaidi itapata fursa ya ruzuku ya kati ya Shilingi 500,000 hadi Shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuongeza kasi ya ukuaji wa biashara.

Tangu kuanzishwa kwa CRDB Bank Foundation mwaka 2023, zaidi ya wajasiriamali 1,250,000 wamefikiwa kupitia elimu ya fedha, mafunzo na mitaji wezeshi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 21.


Msingi wa Kisheria na Ushirikiano wa Kitaifa

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daniel Sillo, alisema Bunge limeweka msingi imara wa kisheria unaowezesha ulinzi wa mazingira na kukuza uchumi wa kijani, huku akitaja programu hiyo kama mfano halisi wa kuunganisha sera, mitaji na ubunifu wa vijana.


Ushuhuda wa Mnufaika: “Inawezekana Kabisa

Akizungumza kwa niaba ya biashara changa bunifu za vijana, Irene Vambi, mwanzilishi wa Mrembo Naturals, alisema kupitia programu ya IMBEJU ameweza kupata mafunzo, ushauri wa kitaalamu na mitaji iliyomwezesha kupanua uzalishaji wa bidhaa zake za asili na kuongeza ajira kwa vijana wengine.

IMBEJU imenisaidia kubadilisha wazo langu kuwa biashara inayokua na kuajiri vijana wengine. Go Green na IMBEJU ni fursa ya kweli kwa vijana wenye ubunifu na ndoto. Nawasihi vijana wenzangu wachangamkie fursa hii, waombe na wajiamini. Inawezekana kabisa,” alisema Irene Vambi.


Jinsi ya Kutuma Maombi

Kwa taarifa zaidi kuhusu jinsi ya kushiriki katika programu ya Go Green na IMBEJU, tembelea:

Programu hii inaweka msingi mpya wa kuunganisha uchumi wa kijani, mitaji ya tabianchi na ubunifu wa vijana – hatua muhimu kuelekea Tanzania yenye uchumi himilivu na shindani.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (wa pili kushoto), akipata maelezo kutoka kwa wawakilishi wa kampuni ya Kana Wine iliyoshiriki katika maonesho ya biashara changa bunifu za vijana, wakati wa hafla ya uzinduzi wa programu ya Go Green na IMBEJU inayolenga kuwezesha biashara na bunifu za kijani za vijana kama sehemu ya kuchochea uchumi wa kijani kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Wengine pichani ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (wa tatu kulia); Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dkt. Donald Mmari (wa pili kulia); Mwenyekiti wa CRDB Bank Foundation, CPA Osward Urassa (wa kwanza kulia); na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (wa pili kushoto), akiwasili katika hafla ya uzinduzi wa programu ya Go Green na IMBEJU, inayolenga kuwezesha biashara na bunifu za kijani za vijana kama sehemu ya kuchochea uchumi wa kijani kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Alioongozana nao ni Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Daniel Sillo (katikati); Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (wa pili kulia); Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa kwanza kushoto); na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa.

No comments:

Post a Comment