Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Monday, 2 February 2026

BENKI YA I&M YAPANDA MIKOKO 20,000 KIGAMBONI: UENDELEVU NA UWEZESHAJI WA WANAWAKE

Dar es Salaam, Tanzania – Benki ya I&M Tanzania imepandikiza miche 20,000 ya mikoko katika eneo la Tundwi Songani, Kigamboni, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi mazingira.

Mradi huu umehusisha wafanyakazi wa benki, wateja, na wadau mbalimbali, kwa kushirikiana na shirika la Africa Transformational Initiative (ATI), na kuonyesha jinsi ushirikiano unaoweza kufanikisha ajenda za maendeleo endelevu.

Akizungumza kuhusu mpango huu, Maria Gonsalves, Mkuu wa Idara ya Sheria na Kiongozi wa Masuala ya Uendelevu wa I&M Bank Tanzania, alisema mradi huu ni sehemu ya Mpango wa Urejeshaji wa Mikoko wa Tundwi Songani na Uwezeshaji Wanawake, unaounganisha ujumuishaji wa kifedha kwa wanawake na uhifadhi wa mazingira.

Benki inapanda mti mmoja kwa kila wanawake 100 wanaofadhiliwa kupitia jukwaa la kidijitali la Kamilisha, sambamba na lengo la SDG 13 la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Gonsalves.

Kwa upande wake, Bwana Zahid Mustafa, Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa I&M Bank Tanzania, alisema kuwa uendelevu ni msingi wa biashara yao na wajibu wao kwa jamii. Alisisitiza kwamba kuunganisha uwezeshaji wa wanawake na urejeshaji wa mazingira ni ushuhuda kwamba maendeleo ya kiuchumi yanaweza kwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa jamii.

Mwakilishi wa ATI, Wisdom Rober Mande, aliongeza kuwa ushirikiano huu unaonesha jinsi urejeshaji wa mazingira unavyoweza kuambatana na uwezeshaji wa jamii. Alibainisha kuwa mikoko ina mchango mkubwa katika kulinda ukanda wa pwani, kuhifadhi bioanuwai, na kuboresha maisha ya jamii zinazotegemea rasilimali za bahari.

Kwa hatua hii, I&M Bank Tanzania inathibitisha kuwa uwekezaji katika uendelevu na jamii unaweza kuleta faida za muda mrefu, si tu kwa benki, bali pia kwa mazingira na jamii zinazozunguka.








No comments:

Post a Comment