Mfumo Mpya Waunganisha Mikopo, Bima, Uwekezaji na Huduma za Vikundi
Dar es Salaam, Tanzania; Juni 16, 2026 – Benki ya NMB imezindua rasmi NMB Mkononi Super App, jukwaa jipya la kidijitali linalounganisha huduma mbalimbali za kifedha katika mfumo mmoja, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za benki na kuimarisha ujumuishaji wa kifedha nchini.
Kupitia jukwaa hilo, wateja wataweza kupata huduma za mikopo, bima, uwekezaji, malipo, huduma za vikundi pamoja na ununuzi wa bando la mawasiliano bila ulazima wa kutembelea matawi ya benki kwa huduma za kawaida.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bank Plc, Ruth Zaipuna, alisema kuwa NMB Mkononi Super App ni zaidi ya programu ya kibenki, bali ni jukwaa la fursa na uwezeshaji linalolenga kuwahudumia makundi mbalimbali ya Watanzania.
“Jukwaa hili limeundwa kuwawezesha wanafunzi, wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara, wajasiriamali na wawekezaji kusimamia mahitaji yao ya kifedha kwa urahisi kupitia simu zao za mkononi,” alisema Zaipuna.
Katika hatua ya kuongeza upatikanaji wa mitaji, NMB imesema wateja binafsi wanaokidhi vigezo wataweza kuomba mikopo ya hadi Shilingi milioni mbili kupitia programu hiyo, huku wafanyabiashara wadogo wanaostahili wakipata mikopo ya hadi Shilingi milioni tano.
Hata hivyo, wataalamu wa sekta ya fedha wanaona kuwa ongezeko la upatikanaji wa mikopo kidijitali linaifanya elimu ya fedha kuwa muhimu zaidi, hasa katika kuwawezesha wananchi kuelewa gharama za mikopo, masharti ya mikataba, muda wa marejesho na uwezo wao wa kulipa kabla ya kukopa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Ubunifu wa NMB, Josina Njambi, alisema ufunguaji wa akaunti kupitia NMB Mkononi Super App umeboreshwa kwa kiwango kikubwa, ambapo mteja anaweza kufungua akaunti kwa kutumia namba ya simu na namba ya NIDA ndani ya dakika tano pekee.
Alibainisha kuwa mafanikio ya jukwaa hilo hayatategemea tu upana wa huduma zake, bali pia uwezo wake wa kuwasaidia wateja kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, kuongeza utamaduni wa kuweka akiba na kutumia huduma za kifedha kwa uwajibikaji.
Uzinduzi wa NMB Mkononi Super App unaashiria hatua nyingine muhimu katika safari ya mageuzi ya kidijitali ya sekta ya benki nchini Tanzania, huku ukionyesha namna teknolojia inavyoendelea kubadilisha upatikanaji na matumizi ya huduma za kifedha kwa wananchi wa kada mbalimbali.
Mkononi Patamu.
No comments:
Post a Comment