Arusha, Oktoba 9, 2026 – Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE), kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation, imezindua Kituo cha Rasilimali za Walimu katika Shule ya Msingi Naurei, wilayani Arusha, ikiwa ni hatua ya kupanua upatikanaji wa mafunzo ya kidijitali kwa walimu nchini.
Kituo hicho ni cha kwanza kati ya vituo 50 vinavyotarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kuwawezesha walimu kupata mafunzo endelevu ya kitaaluma kupitia teknolojia, kuboresha mbinu za ufundishaji na kuongeza fursa za wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao.
Ushirikiano huo unatekelezwa kupitia Programu ya Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (TCPD/MEWAKA), inayolenga kuimarisha matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Kujifunza (LMS) pamoja na Vituo vya Rasilimali za Walimu (TRC).
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kituo hicho, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, alisema uwekezaji katika maendeleo ya walimu ni muhimu katika kuimarisha uwezo wao wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuboresha ubora wa elimu nchini.
Alisema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuboresha miundombinu, teknolojia na mifumo ya kujifunzia unawawezesha walimu kuendelea kujifunza na kuimarisha ujuzi wao katika kipindi chote cha utumishi wao.
“Mwalimu anayepata maarifa mapya, anayeongeza kiwango cha elimu alichonacho na kutumia teknolojia kwa ufanisi, huongeza nafasi ya wanafunzi kufaulu na kufikia ndoto zao,” alisema Lugangira.
Alieleza kuwa tathmini ya mahitaji ya programu ya TCPD/MEWAKA, iliyohusisha Vituo vya Rasilimali za Walimu 178, walimu 350 na wadau mbalimbali, imebaini kuwa walimu wengi wana hamasa ya kujifunza na kutumia teknolojia.
Kwa mujibu wa tathmini hiyo, asilimia 99 ya walimu waliohusishwa walikuwa wanafahamu mfumo wa LMS, huku asilimia 71 wakiwa na uelewa wa msingi wa TEHAMA.
Hata hivyo, tathmini hiyo ilibainisha kuwa upatikanaji mdogo wa vifaa vya TEHAMA, kompyuta, huduma za intaneti na usaidizi wa kiufundi bado ni miongoni mwa changamoto zinazozuia matumizi kamili ya mifumo ya kidijitali, hasa katika maeneo ya vijijini.
Lugangira alisema mafanikio ya programu hiyo yanahitaji uwekezaji unaoendelea katika vifaa, muunganisho wa intaneti, mafunzo ya vitendo na mifumo imara itakayowezesha walimu kunufaika kikamilifu na teknolojia.
Pia aliipongeza Vodacom Tanzania Foundation kwa mchango wake katika kuendeleza elimu na kuhamasisha taasisi nyingine za sekta binafsi kuunga mkono juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah, alisema uwekezaji katika maendeleo ya walimu ni mojawapo ya njia muhimu za kuboresha mfumo wa elimu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Alisema walimu wanapopata fursa za kujifunza na kutumia teknolojia kwa ufanisi, manufaa yake huonekana kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
“Hii ndiyo sababu Vodacom Tanzania Foundation imeamua kuwekeza katika mifumo na miundombinu inayowezesha maendeleo ya walimu kwa njia endelevu,” alisema Farah.
Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano na TIE, walimu wanaotumia mtandao wa Vodacom wanaweza kufikia mfumo wa LMS bila kutozwa gharama za data, hatua inayolenga kupunguza vikwazo vya upatikanaji wa maudhui ya mafunzo na maendeleo ya kitaaluma.
Farah alisema mpango huo unalenga kuhakikisha walimu wengi zaidi wanapata fursa ya kujiendeleza kitaaluma kupitia teknolojia, bila kujali maeneo wanayoishi au kufanyia kazi.
Alisisitiza kuwa sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kuharakisha utekelezaji wa mipango ya elimu kupitia uwekezaji katika teknolojia, muunganisho wa intaneti, vifaa vya TEHAMA, ubunifu na utaalamu wa kidijitali.
Kwa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, juhudi hizo zinalenga kujenga mfumo wa elimu unaokidhi mahitaji ya karne ya 21 na kuwawezesha walimu na wanafunzi kunufaika zaidi na fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia.
Kitomari Banking & Finance Blog – Kwa habari zaidi kuhusu biashara, benki, fedha, teknolojia na maendeleo ya sekta mbalimbali, endelea kutufuatilia kupitia blogu yetu.
Tufuatilie kwenye mitandao ya kijamii:
LinkedIn | Facebook | Instagram | X (Twitter)






No comments:
Post a Comment