Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_170926_270926_101026

Absa Banner_170926_270926_101026

Stanbic Bank Banner_070826

Stanbic Bank Banner_070826

Sunday, 11 October 2026

NBC YAIPAMBA DABI YA KARIAKOO, YAMKABIDHI ELIE MPANZU TUZO YA MCHEZAJI BORA

Mkurugenzi wa Wateja Wadogo wa NBC, Elibariki Masuke (kulia), akimkabidhi tuzo mshambuliaji wa Simba SC, Elie Mpanzu (kushoto), aliyeibuka Mchezaji Bora wa mechi ya Ligi Kuu ya NBC iliyozikutanisha Simba SC na Yanga SC, maarufu kama Dabi ya Kariakoo, iliyochezwa jana katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Mchezo huo ulimalizika kwa Simba SC kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga SC.

Dar es Salaam, Oktoba 11, 2026 – Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya NBC, imeongeza msisimko katika Dabi ya Kariakoo kati ya Simba SC na Yanga SC kwa kuandaa shughuli mbalimbali zilizowakutanisha mashabiki wa soka na wateja wake, huku ikimkabidhi mshambuliaji wa Simba SC, Elie Mpanzu, tuzo ya mchezaji bora wa mechi hiyo.

Simba SC iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, katika mchezo uliovuta hisia za mashabiki na kuendeleza ushindani mkali kati ya miamba hiyo ya soka nchini.

Mkurugenzi wa Wateja Wadogo wa NBC, Elibariki Masuke (kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki NBC, Msafiri Shayo (kushoto) wakifuatilia mchezo huo.

Kupitia shughuli hizo, NBC ilitumia fursa ya dabi hiyo kubwa kuimarisha uhusiano na wateja wake, huku ikiendeleza dhamira yake ya kuunganisha huduma za kibenki na uzoefu wa kipekee kwa wadau wa michezo.

Kabla ya mchezo huo, benki hiyo iliwawezesha baadhi ya wateja wake kusafiri kwa msafara maalumu kuelekea Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ambako walishuhudia pambano hilo kutoka jukwaa la VIP na kufurahia dabi hiyo katika mazingira ya kipekee.

Mkurugenzi wa Wateja Wadogo wa NBC, Elibariki Masuke, aliongoza shughuli hizo na kumkabidhi Elie Mpanzu tuzo ya mchezaji bora wa mechi. Tukio hilo lilishuhudiwa na mashabiki waliokuwa uwanjani pamoja na watazamaji waliofuatilia matangazo ya moja kwa moja kupitia televisheni.

Sambamba na shughuli za uwanjani, maofisa wa NBC walitoa huduma mbalimbali za kibenki kwa mashabiki na wadau waliohudhuria mchezo huo, zikiwemo huduma za kufungua akaunti na ushauri wa kifedha. Hatua hiyo iliipa benki fursa ya kuwasogezea wateja huduma zake, huku ikiendeleza ushiriki wake katika kukuza soka nchini.

Akizungumzia ushiriki wa NBC katika dabi hiyo, Masuke alisema benki hiyo inaendelea kutumia michezo mikubwa kuimarisha uhusiano na wateja wake pamoja na wadau wengine wa soka.

“Udhamini wetu hauishii tu katika kuboresha ligi tunazodhamini, bali pia katika kuhakikisha kuwa wadau wetu, wakiwemo wafanyakazi, viongozi na wateja, wanakuwa sehemu ya moja kwa moja ya mchezo huu. Tunataka soka liwe uzoefu wa kipekee, si tukio la dakika 90 pekee,” alisema Masuke.

Aliongeza kuwa NBC inaendelea kubuni mikakati ya kuboresha Ligi Kuu ya NBC kwa lengo la kukuza vipaji, kuongeza ushindani, kuchochea ajira kupitia michezo na kuimarisha hamasa ya soka nchini.

Katika misimu ya hivi karibuni, NBC imeendelea kuunga mkono maendeleo ya soka kupitia udhamini wa ligi na shughuli mbalimbali zinazolenga kuimarisha ushindani na ustawi wa mchezo huo. Miongoni mwa maeneo ya ushiriki wake ni kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha, zikiwemo bima ya afya na mikopo ya usafiri kwa timu, pamoja na kusaidia hafla za utoaji wa vikombe na tuzo.

Kupitia udhamini huo, NBC inaendelea kuunganisha michezo, huduma za kifedha na ushirikiano na wateja, huku ikiimarisha nafasi yake kama mdau wa maendeleo ya soka na michezo nchini Tanzania.


Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari na taarifa za hivi karibuni kuhusu sekta ya benki, biashara, fedha na maendeleo ya michezo nchini Tanzania.

Tufuatilie kwenye mitandao ya kijamii:




No comments:

Post a Comment