Arusha - Septemba 22, 2026: Benki ya NMB kwa kushirikiana na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imewakutanisha vijana 20 wenye ujuzi katika sayansi ya data, akili mnemba (AI) na sayansi ya kompyuta, kwa ajili ya kubuni suluhisho za kiteknolojia zinazolenga kusaidia wakulima kupata huduma za kifedha na kuongeza tija katika kilimo.
Mpango huo unafanyika kupitia AgriFin Hackathon 2026, inayofanyika kuanzia Septemba 21 hadi 25, 2026 katika Kituo cha ICT cha NM-AIST jijini Arusha.
Hackathon hiyo inalenga kuwapa vijana wabunifu nafasi ya kutumia maarifa na ujuzi wao kutatua changamoto halisi zinazokabili sekta ya kilimo, hususan katika upatikanaji wa huduma za kifedha na matumizi ya teknolojia katika kuongeza uzalishaji.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu kutoka Makao Makuu ya NMB, Joanitha Rwegasira Mrengo, alisema ushirikiano huo unawezesha kuunganisha maarifa yanayopatikana darasani na ubunifu wa suluhisho ambazo zinaweza kutumika moja kwa moja katika kusaidia wakulima.
Alisema vijana hao wanapata fursa ya kutumia ujuzi wao katika teknolojia za kisasa huku wakilenga kutengeneza mifumo inayoweza kujibu mahitaji halisi ya sekta ya kilimo.
Kwa upande wake, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa NM-AIST anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ubunifu, Prof. Mwemezi Rwiza, alisema washiriki wa AgriFin Hackathon watapata mafunzo na ushauri kutoka kwa wataalamu katika maeneo mbalimbali, yakiwemo akili mnemba, usalama wa mtandao na biashara ya kilimo.
Aidha, wataalamu kutoka NMB watashiriki katika mchakato wa kutathmini na kuendeleza mifumo na suluhisho zitakazobuniwa na washiriki.
Ushirikiano huo unaweka pamoja utaalamu wa taasisi ya elimu na utafiti pamoja na uzoefu wa taasisi ya kifedha, kwa lengo la kuchochea ubunifu unaoweza kusaidia kutatua changamoto za kifedha na uzalishaji katika sekta ya kilimo.
AgriFin Hackathon 2026 inatarajiwa kufungwa Septemba 25, 2026, ambapo washiriki watawasilisha suluhisho zao mbele ya majaji kwa ajili ya tathmini na washindi kutangazwa.
Baadhi ya washindi wanatarajiwa kupata fursa za kuendeleza ubunifu wao nje ya Tanzania, ikiwemo Korea Kusini, hatua inayolenga kuwapa vijana nafasi ya kuendeleza teknolojia zao katika mazingira mapana zaidi ya ubunifu na biashara.
Mpango huo unaonyesha namna ushirikiano kati ya sekta ya fedha, taasisi za elimu na vijana wenye ujuzi wa teknolojia unavyoweza kusaidia kutengeneza suluhisho zinazolenga kuongeza matumizi ya teknolojia na upatikanaji wa huduma za kifedha katika sekta ya kilimo.
Fuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari na taarifa zaidi kuhusu benki, fedha, biashara, teknolojia na maendeleo ya sekta mbalimbali nchini Tanzania.
Mitandao yetu ya kijamii:
LinkedIn | Facebook | Instagram | X (Twitter)


.jpeg)
.jpeg)




No comments:
Post a Comment