Benki Yatoa Dhamana za Zabuni Hadi Dola Milioni 11 kwa Wadau wa Madini
CHUNYA, MBEYA; Oktoba 26, 2026 — Benki ya NMB imetangaza fursa za kifedha kwa wadau wa sekta ya madini nchini kwa kutoa dhamana za zabuni (Bid Bonds) zisizohitaji dhamana ya mali zenye thamani ya hadi dola za Marekani milioni 11, pamoja na dhamana za malipo ya awali (Advance Payment Guarantees) na utekelezaji wa mikataba (Performance Guarantees) za hadi Shilingi bilioni 11.
Huduma hizo zinalenga kuwawezesha wachimbaji, wafanyabiashara na watoa huduma katika migodi kushiriki zabuni kubwa na kutekeleza mikataba ya biashara kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza katika hafla ya NMB Business Executive Network iliyowakutanisha wachimbaji wa dhahabu na wadau wa sekta ya madini kutoka Chunya mkoani Mbeya na Songwe, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, amesema huduma hizo zinalenga kupunguza vikwazo vya kifedha vinavyowakabili wafanyabiashara na watoa huduma migodini.
Mponzi amesema benki itaendelea pia kutoa elimu ya fedha ili kuwasaidia wateja kusimamia biashara zao kwa ufanisi, kuimarisha uwezo wao wa kifedha na kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini.
Kwa upande wake, Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Wogofya Mfalamagoha, amesema shughuli za uchimbaji madini zimefungua fursa mbalimbali za ajira na biashara, hali inayochochea benki kuimarisha ushirikiano wake na wadau wa sekta hiyo.
Naye mwakilishi wa Chama cha Watoa Huduma Migodini (TAMISA), Gilbo Thomas, amesisitiza umuhimu wa upatikanaji wa vifaa vya uchimbaji madini ili kuongeza tija na kuboresha shughuli za wachimbaji.
Wakati huo huo, mwakilishi wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mbeya (MBEREMA), Saddam Kyando, ameiomba NMB kuangalia uwezekano wa kutumia leseni za uchimbaji madini kama dhamana ya mikopo kwa wachimbaji wadogo, hatua inayoweza kuwasaidia kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao.
Kwa upande wao, wachimbaji Fredrick Meshack, Sophia Mwanauta, Mussa Wilfred na Simon Mbalawata wamepongeza mikutano ya NMB na wateja wake, wakisema inatoa nafasi muhimu ya kujadili changamoto zinazowakabili pamoja na fursa za kukuza biashara katika sekta ya madini.
Kupitia huduma zake za kifedha na majukwaa ya mazungumzo na wateja, NMB inaendelea kuimarisha uhusiano na wadau wa biashara kwa lengo la kuwawezesha kutumia fursa za kiuchumi na kuchangia ukuaji wa sekta ya madini nchini.
Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari, uchambuzi na taarifa za hivi karibuni kuhusu sekta ya benki, fedha, biashara na uchumi.
Tufuatilie kwenye mitandao ya kijamii:
- LinkedIn: https://www.linkedin.com/feed/
- Facebook: https://www.facebook.com
- Instagram: https://www.instagram.com
- X (Twitter): https://x.com/home

.jpeg)



.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
No comments:
Post a Comment