Dar es Salaam, Januari 20, 2025: Benki ya CRDB imeendelea kung’ara kimataifa baada ya kutunukiwa tuzo 2 za Mwajiri Bora (Top Employer) na taasisi ya kimataifa ya Top Employers Institute. Ushindi huu unaiweka Benki ya CRDB katika nafasi ya kipekee kama moja ya waajiri bora barani Afrika, ikitambua jitihada zake za kujenga mazingira bora ya kazi yanayochochea ubunifu, ustawi wa wafanyakazi, na maendeleo ya kitaaluma.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Godfrey Rutasingwa, alisema tuzo hizo zinadhihirisha juhudi za dhati za kuboresha maisha ya wafanyakazi wake ndani na nje ya kazi.
Tuzo ya Top Employer inatolewa baada ya tathmini ya kina ya viwango vya usimamizi wa rasilimali watu, ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika maendeleo ya kitaaluma, usawa wa kijinsia, programu za afya na ustawi wa wafanyakazi, na utamaduni wa uwazi na mshikamano. Katika maeneo haya, Benki ya CRDB imeonyesha ubora wa kipekee, ikiwasaidia wafanyakazi wake kufanikisha ndoto zao za kitaaluma huku wakichangia ukuaji wa Benki hiyo kwa kasi.
Rutasingwa alibainisha kuwa Benki ya CRDB inajipanga kuimarisha nafasi yake kama kinara wa usimamizi wa vipaji barani Afrika. “Tunajivunia kuwa sehemu ya mabadiliko yanayoangazia wafanyakazi kama rasilimali muhimu. Maendeleo endelevu ya benki yetu hayawezekani bila jitihada za kila mfanyakazi,” aliongeza.
Kupitia tuzo hizo za Top Employer, Rutasingwa amewahakikishia wadau, wateja, na washirika wa Benki hiyo kuwa itaendelea kuwekeza katika ubora wa wafanyakazi wake, lakini pia katika huduma na bidhaa ili kukuza ustawi wa watu wake na jamii kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment