Akizindua huduma hizo, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuonyesha njia katika huduma zake kwa kutambua kwamba wapo baadhi ya wateja ambao hushindwa kupata huduma kutokana na imani zao za kidini.
Kwa upande wake, Kamshna wa Bima na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware amesema ubunifu unaotatua changamoto zinazowakwamisha Watanzania kutumia huduma za bima unahitajika ili kuikuza sekta hiyo na kuwawezesha wananchi wengi kuwa na uhakika wa mipango na miradi wanayoitekeleza.
Mwaka 2021 Benki ya CRDB ilianzisha kitengo maalum cha huduma zinazofuata misingi ya Shariah yaani CRDB Al Barakah Banking hali iliyoifanya kuwa benki ya kwanza nchini kufikisha huduma zinazozingatia shariah nchi nzima. Katika kipindi hicho chote mpaka sasa, CRDB Al Barakah inao wateja zaidi ya 135,000 na kufanya uwezeshaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 125, sehemu kubwa ikielekezwa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.
“Katika mwendelezo wa kuboresha huduma zetu, Benki ya CRDB kwa kushirikiana na wenzetu, Zanzibar Insurance Corporation (ZIC) Takaful, leo tunazindua huduma za bima zinazofuata misingi ya shariah maarufu kama Takaful. Hii inapelekea kwa mara nyingine CRDB kuwa Benki ya kwanza nchini kuleta huduma hizi kwa wateja wake nchi nzima,” amesema Raballa.
“Kupitia ushirikiano huu tunakwenda kutoa huduma za bima za jumla (general insurance) ikiwamo bima za magari, bima ya nyumba, moto, biashara, bima ya usafirishaji, na bima ya mitambo. Nichukue fursa hii kuwakaribisha Watanzania wote kuchangamkia fursa hii ya bima inayofuata misingi ya shariah (Takaful) inayoenda kutolewa rasmi kupitia Benki yetu pendwa ya CRDB. Takaful ni kwa ajili ya mtu yoyoye anayetamani kupata bima inayofuata misingi ya Shariah na inapatikana katika matawi yetu yote yaliyosambaa nchi nzima,” amesema Raballa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa ZIC Takaful, Said Abdallah Basleym amesema ni furaha kwao kushirikiana na Benki ya CRDB, taasisi kubwa nchini kusambaza huduma za Takaful kwa Watanzania.
“Mshikamano huu naamini utasaidia kuzifikisha kwa wananchi wengi zaidi huduma za Takaful. Tutaendelea kushirikiana na wadau wengine wenye nia ya dhati ya kueneza huduma hizi kwa manufaa ya kila Mtanzania. Bima ndio namna pekee ya kulinda mali, biashara au afya ya mtu hivyo kila mmoja wetu anastahili kuwa nayo bila kikwazo cha aina yoyote,” amesema Basleym.
“Mshikamano huu naamini utasaidia kuzifikisha kwa wananchi wengi zaidi huduma za Takaful. Tutaendelea kushirikiana na wadau wengine wenye nia ya dhati ya kueneza huduma hizi kwa manufaa ya kila Mtanzania. Bima ndio namna pekee ya kulinda mali, biashara au afya ya mtu hivyo kila mmoja wetu anastahili kuwa nayo bila kikwazo cha aina yoyote,” amesema Basleym.
No comments:
Post a Comment