Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_211026

Stanbic Bank Banner_201026

Friday, 23 October 2026

NMB NA CMC WAZINDUA KAMPENI YA MATREKTA KWA WAKULIMA WA KOROSHO MTWARA, RC MSENGI AITAKA NMB KUTOA ELIMU

Mtwara - Oktoba 23, 2026: Benki ya NMB kwa kushirikiana na CMC Agri Limited imezindua kampeni ya Korosho Yangu, Benki Yangu mkoani Mtwara, inayolenga kuhamasisha wakulima wa korosho kuongeza amana benki huku wakipata fursa ya kushinda matrekta, pikipiki na zawadi za fedha katika msimu wa korosho wa 2026/2027.

Kupitia kampeni hiyo, vyama vikuu vitano vya ushirika vitashindania matrekta, vyama vya msingi vya ushirika vya wakulima (AMCOS) vitashindania pikipiki, huku wakulima mmoja mmoja wakipata fursa ya kujishindia zawadi za fedha kwa kuongeza amana zao benki, kwa kuzingatia masharti ya kampeni.

Akizindua kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, amesema matrekta yatakayopatikana kupitia kampeni hiyo yanaweza kusaidia kupunguza changamoto za usafirishaji wa pembejeo za kilimo na korosho, hususan katika maeneo yenye miundombinu duni.

RC Msengi ameitaka NMB kutoa elimu ya kutosha kwa wakulima kuhusu masharti ya kampeni hiyo na upatikanaji wa mikopo ili kuwawezesha kuelewa fursa zinazopatikana na kuzitumia ipasavyo.

Aidha, ameshauri benki hiyo kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wakulima kupata mikopo itakayowawezesha kulipia bima ya afya kabla ya msimu wa mavuno, hatua inayoweza kuwasaidia kukabiliana na gharama za huduma za afya.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa NMB, Nsolo Mlozi, amesema matrekta yatakayoshindaniwa kupitia kampeni hiyo yatasaidia kurahisisha shughuli mbalimbali za kilimo, ikiwemo usafirishaji wa korosho, unyunyiziaji wa dawa na maandalizi ya mashamba.

Ameeleza kuwa washindi watapatikana kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, vikiwemo kiwango cha amana, miamala inayofanyika kupitia benki hiyo na masharti mengine ya kampeni.

Naye Meneja wa CMC Agri Limited Tanzania, Stuart Leishman, amesema matumizi ya zana za kisasa za kilimo ni muhimu katika kuongeza tija, kurahisisha shughuli za mashambani na kuboresha uzalishaji wa wakulima.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU, Alhaji Azam Mfaume, amesema kampeni hiyo itachochea ushindani miongoni mwa vyama vya ushirika katika kuongeza amana benki na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za kilimo kwa wakulima.

Kampeni ya Korosho Yangu, Benki Yangu ni sehemu ya juhudi za kuunganisha huduma za kifedha na mahitaji ya sekta ya kilimo, huku ikilenga kuwahamasisha wakulima kutumia huduma za benki katika kusimamia mapato yao na kuimarisha shughuli zao za uzalishaji.

Kwa taarifa zaidi kuhusu huduma na fursa za kifedha, endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog.


Fuatilia Kitomari Banking & Finance Blog







No comments:

Post a Comment