Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Wednesday, 23 March 2022

KILOMBERO YAWAHAKIKISHIA WANANCHI UPATIKANAJI WA SUKARI KATIKA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI

Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni ya Sukari ya Kilombero, Fimbo Butallah akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja Mauzo, Harshid Chavda na kushoto ni Meneja Usambazaji, Johannes Rugalema.

"Tunawasihi wafanyabiashara kote nchini kutopandisha bei ya sukari katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kuepuka taharuki inayoweza kujitokeza"

23 Machi 2022: Dar es Salaam — Kampuni ya Sukari ya Kilombero na kusambaza sukari chini ya chapa ya “Bwana Sukari” inapenda kuwatoa hofu wananchi, hususani wapenzi na watumiaji wa sukari ya Kilombero “Bwana Sukari” kuhusu upungufu wa sukari katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Aprili.

Hayo yamesemwa na Fimbo Butallah, Mkuu wa Idara ya Biashara siku ya Jumatano, 23 Machi, 2022 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam.

Tamko hilo limekuja kutokana na historia ya kupanda kwa bei za bidhaa nyingi za vyakula kila uanzapo mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kusababisha adha kubwa kwa wananchi, hususan waumini wanaofunga katika mwezi huo. Kutokana na hilo, kampuni ya Sukari ya Kilombero imewasihi wafanyabiashara wote, wa jumla na rejareja wanaouza bidhaa za “Bwana Sukari” kutopandisha bei, jambo ambalo limekuwa likiwakandamiza watumiaji wa sukari ambapo matumizi yake huongezeka zaidi katika mfungo wa Ramadhani.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Fimbo alisema, “Tunafahamu kuwa katika uchumi wa soko huria, sisi kama wazalishaji haturuhusiwi kuwapangia wafanyabiashara bei ya kuuza bidhaa. Hata hivyo tunao wajibu mkubwa wa kuwashauri kuhusu upandishaji holela wa bei, haswa pale ambapo sisi kama wazalishaji wa sukari hatujapandisha bei ya bidhaa hiyo. Tunawasihi wafanyabiashara kote nchini kutopandisha bei za sukari katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kuepuka taharuki inayoweza kujitokeza.”

Akizungumzia suala la uhaba wa sukari ambao mara nyingi hujitokeza katika mfungo wa Ramadhani, Fimbo alisema kuwa Kampuni ya Sukari ya Kilombero inayo akiba ya kutosha kulivusha taifa katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuongezea kuwa tayari kampuni imepata kibali cha kuagiza sukari kutoka nje ya nchi ili kuziba pengo la uzalishaji.

“Tumekwishaanza taratibu za uagizaji wa sukari ambayo inatarajiwa kuanza kuingia nchini muda wowote kuanzia hivi sasa. Tunapenda kuwatoa hofu wananchi kuhusu upandaji holela wa bei ya sukari, hususan chapa ya “Bwana Sukari” kwani kampuni imeandaa mikakati thabiti kukabiliana na tatizo hilo katika msimu huu”, alisema Fimbo.

Kampuni ya Sukari ya Kilombero, ambayo inamilikiwa na Kampuni ya Illovo Sugar Africa kwa Asilimia 75 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 25 ipo katika maandalizi ya mradi wake wa upanuzi ambao utakuza uwezo wa kampuni hiyo wa kutengeneza sukari na kupunguza uhaba wa sukari nchini kupitia chapa yake ya “Bwana Sukari”.

Mawasiliano:

Fimbo Butallah, Mkuu wa Idara ya Biashara
Namba ya Simu: +255 687 610 662
Barua pepe: fbutallah@illovo.co.za

No comments:

Post a Comment