Dar es Salaam; Julai 31, 2026 - Benki ya Exim Tanzania imezindua rasmi ushirikiano wake wa mwaka 2026 na Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (Young Scientists Tanzania – YST), ikiadhimisha miaka sita ya ushirikiano unaolenga kuwawezesha vijana wabunifu kupitia sayansi, teknolojia, utafiti na ubunifu.
Uzinduzi huo uliofanyika katika Makao Makuu ya Benki ya Exim Tanzania (Exim Tower) jijini Dar es Salaam unathibitisha dhamira ya pande hizo mbili ya kuendelea kuandaa kizazi kijacho cha watafiti, wavumbuzi na watatuzi wa changamoto za kijamii kupitia elimu na teknolojia.
Ushirikiano huo, ulioanza mwaka 2021, unaendelea kuonesha dhamira ya Exim Bank ya kuwekeza katika maendeleo ya vijana kama sehemu ya mchango wake kwa maendeleo ya muda mrefu ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D'Souza, alisema benki hiyo inaamini kuwa uwekezaji kwa vijana ni msingi wa kujenga taifa lenye ushindani, ubunifu na maendeleo endelevu.
"Exim Bank Tanzania tunaamini kuwa ubunifu huanza kwa kuwawezesha vijana. Ushirikiano wetu na Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania unaonesha dhamira yetu ya kuwaunga mkono wanafunzi wenye udadisi, ubunifu na ari ya kutafuta suluhisho zinazoweza kubadilisha jamii na kuchangia maendeleo ya taifa,"alisema D'Souza.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka sita iliyopita, YST imeendelea kuwa mshirika muhimu wa Benki hiyo katika kuibua vipaji vya vijana wanaotumia sayansi, utafiti na ubunifu kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
"Kwa kuwekeza katika elimu, ubunifu na maendeleo ya vipaji vya vijana leo, tunajenga msingi imara wa maendeleo endelevu ya Tanzania," alisisitiza.
Rekodi Mpya ya Ushiriki wa Wanafunzi
Programu ya YST 2026 imeweka rekodi mpya kwa kupokea miradi 1,330 kutoka shule 287 za sekondari zilizopo katika mikoa yote ya Tanzania.
Baada ya mchakato wa tathmini na ulezi wa kitaalamu uliofanywa na washauri wa YST, jumla ya miradi 162 imechaguliwa kuingia hatua inayofuata, huku miradi 45 bora ikitarajiwa kushiriki Maonesho ya Kitaifa ya Sayansi na Teknolojia yatakayofanyika Septemba 17, 2026 katika Ukumbi wa Maktaba Mpya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
YST Yaipongeza Exim Bank kwa Ushirikiano wa Kipekee
Kwa upande wake, Mwanzilishi Mwenza wa Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania, Dkt. Gozbert Kamugisha, aliishukuru Benki ya Exim Tanzania kwa kuendelea kuwa mshirika wa karibu katika kuwawezesha vijana wenye vipaji vya ubunifu.
Alisema ushirikiano wa mwaka huu umeenda mbali zaidi ya udhamini wa kifedha, ambapo wataalamu wa Benki ya Exim walishiriki moja kwa moja katika utekelezaji wa programu kwa kutembelea shule mbalimbali, kukutana na walimu na wanafunzi pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu tafiti na ubunifu.
"Kilichoifanya programu ya mwaka huu kuwa ya kipekee ni kwamba Benki ya Exim Tanzania haijajikita tu katika kutoa udhamini wa kifedha, bali pia imekuwa sehemu ya utekelezaji wa programu kupitia wataalamu wake waliotoa mwongozo kwa wanafunzi na walimu," alisema Dkt. Kamugisha.
Changamoto Bado Zipo
Hata hivyo, Dkt. Kamugisha alieleza kuwa YST bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha unaopunguza uwezo wa kuwafikia vijana wote wenye vipaji pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika maendeleo ya vijana wabunifu.
Alisisitiza kuwa mataifa yaliyofanikiwa kiuchumi yamewekeza kwa kiwango kikubwa katika sayansi, teknolojia na ubunifu, na kwamba Tanzania inapaswa kuendelea kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi na wadau wengine katika kuwawezesha vijana.
Ubunifu Kama Nguzo ya Maendeleo
Kwa zaidi ya miaka 16, Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania imeendelea kuwajengea uwezo wanafunzi wa shule za sekondari kupitia mafunzo ya utafiti wa kisayansi na ubunifu, ikiwawezesha kutambua changamoto zinazowazunguka na kubuni suluhisho zinazotekelezeka na zinazoendana na mazingira ya Tanzania.
Kupitia falsafa yake ya "Ubunifu ni Maisha," Exim Bank Tanzania inaendelea kuwekeza katika mipango inayokuza vipaji vya vijana katika maeneo mbalimbali ikiwemo Akili Unde (Artificial Intelligence), kilimo na mifugo, afya, uhifadhi wa mazingira, usalama wa chakula, mawasiliano pamoja na ubunifu wa kijamii.
Kadri maandalizi ya Maonesho ya Kitaifa ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 2026 yanavyoendelea, ushirikiano kati ya Exim Bank Tanzania na YST unatarajiwa kuendelea kuwa chachu ya kuwaibua wabunifu watakaotoa suluhisho za changamoto mbalimbali na kuchangia kujenga Tanzania yenye uchumi wa maarifa, ubunifu na maendeleo endelevu.
Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari za biashara, benki, uchumi, uwekezaji na maendeleo ya sekta ya fedha nchini Tanzania na duniani.
No comments:
Post a Comment