Dodoma; Agosti 2, 2026 - Mabanda ya Benki ya NMB yanaendelea kuwa miongoni mwa vivutio vikuu katika Maonesho ya Nane Nane 2026 yanayoendelea katika kanda mbalimbali nchini, huku mawaziri, viongozi wa Serikali na maelfu ya wananchi wakiyatembelea kujionea suluhisho za kifedha zinazowezesha maendeleo ya sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na biashara.
Ushiriki huo unaonyesha nafasi ya NMB kama mshirika mkuu wa MAENDELEO ya uchumi wa Tanzania kupitia utoaji wa huduma za kifedha zinazolenga kuongeza uzalishaji, kuimarisha biashara na kuboresha maisha ya wananchi.
Katika Kanda ya Kati jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, walitembelea banda la NMB na kupata fursa ya kujionea huduma mbalimbali za kifedha ambazo benki hiyo imeandaa mahsusi kwa ajili ya wakulima, wafugaji, wavuvi na wafanyabiashara.
Katika Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Morogoro, Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, alitembelea banda la NMB ambapo alipokea maelezo kutoka kwa Meneja Mahusiano wa Benki ya NMB Kanda ya Kati kutoka Idara ya Kilimo na Biashara, Miastela Magoma, kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali za kifedha zinazochochea maendeleo ya sekta ya kilimo na biashara.
Nayo katika Kanda ya Ziwa, mkoani Mwanza, Meneja Mahusiano wa Biashara kwa Serikali wa Benki ya NMB, Humphrey Kaaya, aliendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa za mikopo ya matrekta pamoja na suluhisho za kifedha zinazowezesha ununuzi wa zana za kisasa za kilimo, hatua inayolenga kuongeza tija na kuharakisha matumizi ya teknolojia katika uzalishaji wa kilimo.
Mbali na viongozi wa Serikali, mabanda ya NMB yameendelea kuvutia maelfu ya wananchi wanaotembelea maonesho hayo kila siku, wakipata elimu ya kifedha pamoja na taarifa kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali zinazowawezesha kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Kama mdhamini wa Maonesho ya Nane Nane 2026, NMB inaendelea kudhihirisha dhamira yake ya kusogeza huduma za kifedha karibu na wananchi kwa kutoa suluhisho bunifu vinavyowasaidia wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali kuongeza tija, kuboresha kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kwa kushiriki kikamilifu katika maonesho hayo, benki hiyo inaendelea kuimarisha nafasi yake kama mshirika wa maendeleo anayechochea ujumuishi wa kifedha na ukuaji wa sekta ya kilimo, ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.
Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari za uhakika kuhusu sekta za benki, fedha, biashara na uchumi nchini Tanzania na duniani.




No comments:
Post a Comment