Dar es Salaam - Septemba 27, 2026: KASI kubwa ya mabadiliko ya teknolojia inaendelea kuongeza chachu katika sekta mbalimbali za uzalishaji na biashara, huku kampuni zikijikita zaidi katika ubunifu, kuboresha huduma kwa wateja na kudumisha ubora wa bidhaa ili kuendelea kuwa na ushindani katika soko.
Wadau mbalimbali wanasema kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia, hususan akili mnemba (AI), kunachochea uzalishaji wa bidhaa zinazotoa suluhisho na kukidhi matarajio yanayobadilika ya watumiaji.
Wanasema hali hiyo inafanya umuhimu wa kampuni kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia kuwa mkubwa zaidi ili kuendelea kuwa na nafasi katika soko.
Mkurugenzi wa Masoko wa MeTL Group, Fatema Dewji, alisema biashara zitakazoshindwa kuendana na maendeleo ya teknolojia zinaweza kuachwa nyuma, kutokana na ubunifu kuendelea kuwa na nafasi muhimu katika uuzaji, usambazaji na uundaji wa bidhaa.
“Wakati maendeleo na mabadiliko ya teknolojia yakiendelea kushika kasi, matumizi yake yanazidi kuchochewa hususan katika maeneo ya uzalishaji. Endapo kuna biashara ambazo haziko tayari kukabiliana na mabadiliko haya, zitaachwa mbali sana,” alisema Fatema.
Alikuwa akizungumza katika hafla ya ushirikiano kati ya MeTL Group na Haier Tanzania iliyofanyika mwishoni mwa wiki.
Ushirikiano huo unakuja wakati ushindani katika soko la vifaa vya matumizi ya nyumbani ukizidi kutegemea uwezo wa kampuni kuunganisha ubunifu wa kiteknolojia na ubora wa bidhaa ili kukidhi mahitaji ya watumiaji.
Akizungumzia mitazamo kuhusu matumizi ya akili mnemba (AI), Fatema alisema licha ya baadhi ya watu kuitazama teknolojia hiyo kama tishio kwa ajira, ubunifu na mawazo ya binadamu vitaendelea kuwa muhimu hata wakati biashara zikiendelea kuongeza matumizi ya teknolojia mpya.
“Teknolojia hii haiwezi kuchukua nafasi ya mawazo au watu wenye ubunifu na fikra,” alisema, akiongeza kuwa teknolojia hiyo inaweza badala yake kuwasaidia wafanyakazi, wakiwemo wanaohusika katika shughuli za uzalishaji.
Kwa upande wake, Meneja wa Haier Tanzania, Liu Chi, alisema soko la vifaa vya matumizi ya nyumbani nchini linaendelea kubadilika, huku watumiaji wengi sasa wakizingatia zaidi ubora wa bidhaa.
Alisema hali hiyo inaweka wajibu kwa kampuni kuhakikisha zinazalisha bidhaa zenye tija, ubora na uwezo wa kukidhi mahitaji yanayobadilika ya walaji.
Mabadiliko hayo yanaendelea kuonyesha umuhimu wa teknolojia na ubunifu katika kuongeza ushindani wa biashara, huku kampuni zikihitajika kuwekeza katika teknolojia, watu na bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko.
Fuata Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari na taarifa zaidi kuhusu biashara, benki, fedha, teknolojia na maendeleo ya sekta mbalimbali.
LinkedIn | Facebook | Instagram | X (Twitter)
.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)
No comments:
Post a Comment