Foreign Exchange Rates

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

CRDB Bank Advert_070325

Wednesday, 8 July 2026

NMB YAWAWEZESHA WAKULIMA KUMILIKI MATREKTA KWA MALIPO YA AWAMU, YAONGEZA UFADHILI WA KILIMO

Meneja Mahusiano Kitengo cha Kilimo kutoka Makao Makuu ya Benki ya NMB, Elias Leasa (kushoto), akikabidhi funguo za trekta kwa Dustan Alan Bembati, mnufaika wa mpango wa ufadhili wa vifaa vya kilimo wa NMB, wakati wa makabidhiano yaliyofanyika katika Maonesho ya SabaSaba jijini Dar es Salaam.

SULUHISHO ZA KIFEDHA ZALENGA KUIMARISHA MNYORORO WA THAMANI WA KILIMO

Benki ya NMB imeendelea kuimarisha mchango wake katika kukuza sekta ya kilimo nchini Tanzania kwa kutoa suluhisho mbalimbali za kifedha zinazowawezesha wakulima, wafanyabiashara wa mazao na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa kilimo kupata mitaji kwa ajili ya uzalishaji, ununuzi wa mazao, uchakataji na upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika Banda la NMB wakati wa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SabaSaba), Mkuu wa Idara ya Kilimo kwa Wateja Wakubwa wa Benki ya NMB, Christopher Mwalugenge, alisema benki hiyo inaendelea kubuni huduma zinazokidhi mahitaji ya wadau wa kilimo katika hatua mbalimbali za uzalishaji.

Alisema huduma hizo zimejikita zaidi katika kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara wa mazao kupata fedha kwa wakati, hususan katika msimu wa mavuno ya mazao muhimu kama kahawa, tumbaku, ufuta na pamba.

Tunataka kuhakikisha wadau wa kilimo wanapata fedha na huduma zinazowawezesha kuongeza uzalishaji, kuboresha biashara zao na kufikia masoko yenye tija,” alisema Mwalugenge.

WAKULIMA WAWEZESHWA KUMILIKI MATREKTA NA MASHINE ZA KILIMO

Katika hatua nyingine, NMB imeendelea kuwezesha wakulima kumiliki zana za kisasa za kilimo, ikiwemo matrekta na mashine nyingine muhimu, kupitia utaratibu wa malipo ya awamu unaozingatia uwezo wa mkulima na msimu wa mavuno.

Meneja Mahusiano wa Kitengo cha Kilimo kutoka Makao Makuu ya NMB, Elias Leasa, alisema mpango huo unamwezesha mkulima kuanza kwa kulipa sehemu ndogo ya gharama ya kifaa na kuendelea kukamilisha malipo kwa awamu.

Alisema mkulima anaweza kuanza kwa kulipa asilimia 10 ya thamani ya trekta au mashine husika, kisha kuendelea na malipo kulingana na mzunguko wa mavuno ya mazao yake.

Mpango huo unalenga kupunguza changamoto ya utegemezi wa huduma za kukodisha matrekta, kuongeza matumizi ya teknolojia katika kilimo na kuwawezesha wakulima kuongeza tija katika uzalishaji.

WAKULIMA WAONA MANUFAA YA TEKNOLOJIA YA KILIMO

Mmoja wa wanufaika wa mpango huo, Dustan Alan Bembati, alisema upatikanaji wa trekta binafsi utasaidia kupunguza changamoto ya kuchelewa kwa shughuli za kilimo kutokana na uhaba wa matrekta ya kukodi.

Alisema kumiliki trekta kutamwezesha mkulima kupanga shughuli zake kwa wakati, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza uwezo wa kulima maeneo makubwa zaidi.

Kupata trekta kutatusaidia kutatua changamoto ya kusubiri huduma za kukodi, kuongeza ufanisi na kuboresha uzalishaji wetu,” alisema Bembati.

NMB YAENDELEA KUUNGA MKONO KILIMO CHA KISASA

Kupitia huduma zake za ufadhili wa kilimo, NMB inaendelea kushirikiana na wakulima na wadau mbalimbali katika kujenga sekta ya kilimo yenye tija, ushindani na inayotumia teknolojia za kisasa.

Jitihada hizo zinaendana na azma ya kuimarisha upatikanaji wa mitaji kwa sekta ya kilimo na kuwawezesha wakulima kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa Tanzania kupitia uzalishaji wa mazao yenye thamani katika masoko ya ndani na kimataifa.




No comments:

Post a Comment