Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika katika katika Kituo cha Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC) huku wengine wakifuatilia ajenda zilizojadiliwa kwa njia ya mtandao, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt Ally Laay amesema gawio lililopitishwa ni sawa na ongezeko la 25% likilinganishwa na gawio la Shilingi 36 kwa hisa lililolipwa mwaka jana hali inayodhihirisha kuendelea kuimarika kwa pato kwa hisa ambalo mwaka 2022 limefika TZS 134.5.
Vilevile, Dkt. Laay amesema kampuni tanzu ya Burundi nayo inazidi kuimarika hivyo kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye faida ya kampuni mama. Kwa mwaka 2022, amesema Benki ya CRDB Burundi imepata faida kubwa zaidi tangu lilipoanzishwa mwaka 2012. Kampuni hiyo tanzu ilipata faida ya Shilingi 23 bilioni mwaka 2022 ambayo ni sawa na ongezeko la 79.7% kutoka Shilingi 12.8 bilioni iliyopatikana mwaka 2021. Kwa faida hiyo, kampuni tanzu hiyo ilichangia 7.0% kwenye faida ya kampuni nzima.
Akizungumzia utendaji wa Benki, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema katika mwaka wa fedha 2022, waliendeleza juhudi za kukuza mapato na wakafanikiwa kwa kiasi kizuri kwani mapato ya uendeshaji yaliongezeka kwa 28% na kufika Shilingi 745.8 bilioni yakichangiwa na kuongezeka kwa mikopo iliyotolewa. Kwa mwaka 2022, uwiano wa mikopo chechefu ulishuka mpaka 2.8% hivyo kuwa ndani ya ukomo uliowekwa kikanuni wa kutozidi 5%.
“Juhudi zetu za kuimarisha huduma zetu zilituletea mafanikio hasa katika kubana matumizi kwani uwiano wa gharama na mapato uliimarika kutoka 66.7% mwaka 2018 mpaka 49.4% mwaka 2022,” amesema Nsekela.
Nsekela amesema ufanisi uliopatikana umewezesha kuwekeza zaidi kuimarisha huduma kwa kuwekeza kwenye majukwaa ya kidijitali ambayo yanasaidia kukidhi mahitaji ya wateja kwa kuwapa huduma wazitakazo mahali walipo na kuzitumia kwa namna waitakayo. “Leo hii zaidi ya 95% ya miamala yote ya benki inafanyika kidijiti hasa kupitia SimBanking, huduma za benki kwa intaneti, na kwa zaidi ya mawakala 28,000 wa Benki ya CRDB,” ameongeza.
Kuhusu mikakati ya baadae, Nsekela amesema Bodi ya Wakurugenzi imeidhinisha mpango mkakati wa miaka mitano kuanzia mwaka 2023 – 2027 unaosisitiza kujenga uchumi shirikishi, kuongeza thamani endelevu kwa wanahisa, na kuingia katika ubia wa kimkakati ili kuikuza Benki na kuongeza ushawishi wake sokoni.
Mpango mkakati huo, amesema umetanguliza mbele maslahi ya wateja jambo linalomaanisha Benki sasa inawekeza katika kuyatambua mahitaji ya wateja na kuyafanyia kazi ili kukidhi matarajio yao.
Nsekela amewashukuru wanahisa wa Benki hiyo kwa ushirikiano ambao wameendelea kuipatia menejimenti na wafanyakazi wa benki hiyo, na kuwawathibitishia kwamba Benki itaendelea kufanya vizuri ili kuwapa thamani ya uwekezaji walioufanya na wanaoendelea kuufanya.
Kutokana na kupandishwa cheo kwa Bwana Raballa, amesema Bodi iliamteua Bwana Bonaventure Paul kukaimu ukurugenzi wa wateja wadogo. Vilevile, Bwana Godfrey Rutasingwa aliyekuwa anakaimu ukurugenzi wa Rasilimali Watu, alithibitishwa katika nafasi hiyo.
Kwa upande mwingine, wanahisa walipitisha kampuni ya Ernst & Young kuwa mkaguzi wa nje wa hesabu za fedha kwa mwaka 2023. Vilevile, wanahisa hao waliwachagua kwa mara nyingine tena Profesa Neema Morina Miranda Naiman Mpogolo kuwa Wajumbe Huru wa Bodi ya Wakurugenzi.
No comments:
Post a Comment