Dar es Salaam. Benki ya Taifa ta Biashara (NBC) imeeleza azma yake ya kuhakikisha elimu bora inapatakana kwa wananchi wengi zaidi ili kuchochea ukuaji wa uchumi kwa maendeleo ya Taifa.
Benki hiyo imebuni bidhaa na huduma za kibenki ambazo zinatoa fursa kwa wazazi na walezi kuwapa watoto elimu bora ambayo ni msingi mkubwa wa maendeleo katika ngazi ya familia na kitaifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi akizungumza juzi wakati wa mahafali ya 11 ya Shule ya Sekondari ya Ghome, alisema benki hiyo imejikita katika kuendeleza sekta ya elimu kupitia huduma nafuu na za uhakika hasa katika kugharamikia masomo (ada).
Kupitia akaunti ya Chanua, wazazi wanaweza kuweka akiba kwaajili ya kugharamikia ada za kwa urahisi zaidi.Pia, huduma ya Bima ya elimu inampa mzazi uhakika hata pale anapopata matatizo ikiwamo kifo au ulemavu.
“Tumebuni huduma hizi ili kuwa na mpango wa kudumu pale ambapo yanatokea majanga kama vile kifo au ulemavu wa kudumu,kuhakikisha watoto wanaendelea kupata elimu stahiki,” alisema.
Aidha, benki hiyo ina mpango wa kuwaendeleza wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kuwapa udhamini (Scholarship) ambapo kwa mwaka 2019/2020 jumla ya wananfunzi 63 wamenufaika na mpango huo jambo linaloongeza fursa ya upatikanani wa elimu.
“Tunaitazama sekta ya elimu kama sekta muhimu sana kwa maendeleo ya nchi na vilevile kiuchumi, NBC tumewekeza jitihada katika kubuni bidhaa na huduma mbalimbali ambazo zitawawezesha wazazi na walezi kuwapa watoto wao elimu bora na ya uhakika,” alisema.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Ghome, Ivon Mbieli alisema moja ya maeneo ambayo taasisi hiyo imejikita ni kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora ili kuweza kuleta matokeo chanya kwenye jamiii na taifa kwa ujumla.
“Tuna imani kubwa wanafunzi hawa wataendelea na elimu za juu zaidi na baadaye waje kuwa wataalamu mbalimbali kwa manufaa ya taifa letu,” alisema mkuu huyo.
No comments:
Post a Comment