Mwenyekiti Mtendaji wa kundi la makampuni ya MultiChoice, Imtiaz Patel. |
Kampeni hiyo imezinduliwa kwa kuzingatia ukweli kuwa kumekuwa na taarifa zisizo sahihi na ambazo hazitoki katika vyanzo na mamlaka husika na mara nyingi taarifa hizo huleta taharuki, woga na hofu kwa umma na hivyo kuathiri jitihada za kupambana na janga a COVID-19 kote duniani.
Tangu kulipuka kwa ugonjwa huo, MultiChoice imekuwa mstari wa mbele katika kupambana nao ambapo ilianza kutumia vyombo vyake kutoa matangazo ya tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona pamoja na kutoa misaada mbalimbali ya vifaa muhimu vya kukabiliana na ugonjwa huo.
Katika muendelezo huo, sasa MultiChoice imeungana na umoja wa mataifa kwenye kampeni mahsusi ijulikanayo kama ‘Pause’ ambayo inawaasa watu kuacha kutunga au kusambaza habari zisizothibitiswa na mamlaka stahiki kuhusu COVID-19 kwakuwa habari hizo zinaleta madhara kwa umma.
Mwenyekiti Mtendaji wa kundi la makampuni ya MultiChoice Imtiaz Patel, amesema, “Tuko katika wakati mgumu ambapo tunashuhudia madhara mbalimbali ya kiuchumi na kijamii yanayosababishwa na mlipuka wa COVID-19. Katika kipindi hiki, habari zisizo sahihi, zenye kupotosha na za uvumi zimekuwa kikwazo kikubwa katika kupambana na janga hili hivyo tumeona tuungane na Umoja wa Mataifa katika kampeni hii mahsusi ya kushawishi watu kuacha kusambaza, kubuni na kuzusha taarifa zozote zile zisizothibitishwa kuhusu maradhi haya”
Imtiaz ameongeza kuwa “Utoaji na usambazaji wa habari sahihi kutoka kwenye vyanzo sahihi na mamlaka husika ni muhumu sana katika kupambana na ugonjwa huu na ndiyo sababu MultiChoice imeamua kuungana na Umoja wa Mataifa ili kuruhusu vyombo vyake vya habari kushiriki katika kampeni hii muhimu”
Kuifuatilia kampeni hii tembelea #TakeCareBeforeYouShare
No comments:
Post a Comment