Benki ya NMB inaupa uwezeshaji na ushirikishaji wazawa kipaumbele katika kuchangia kwake utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo humu nchini, hasa ile endelevu ya kimkakati iliyoanzishwa na Serikali.
Sera hii ya benki hiyo ambayo pia inatumika kwenye kufadhili uwekezaji, ni mpango wake wa makusudi kusaidia uendelezaji na ushiriki wa Watanzania na biashara zao katika ujenzi wa taifa na maendeleo yake kwa ujumla.
Hiyo ni kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Huduma za Kifedha kwa Biashara za Kimataifa wa Benki hiyo - Bi. Linda Teggisa, aliyetoa ufafanuzi huo baada ya kuupokea ujumbe wa Mabalozi nane walioambatana na uongozi wa Chemba ya Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) walipotembelea banda la Benki ya NMB kwenye Maonyesho ya Saba Saba ambayo yanafungwa rasmi leo.
Bi. Linda aliufahamisha ugeni huo kwamba, pamoja na kuwahudumia wageni wanapokuja Tanzania kuwekeza na kushiriki katika miradi mbalimbali, maendeleo ya wazawa yanapewa kipaumbele kikubwa na benki yao. Alisema swala la kuwawezesha Watanzania ili washiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na mikubwa ni la msingi sana kwa Benki ya hoyo inayojivunia kuwa na rasilimali zenye thamani ya takribani shilingi trioni 6.5 pamoja na amana zipatazo shilingi trioni 4.7.
“Kwa ufupi sisi kama Benki kubwa nchini tunatoa huduma za kifedha ambazo zinahusisha sekta mbalimbali na miradi nyeti kama sekta ya kilimo, uchukuzi, nishati, maendeleo ya miundombinu pamoja na zile za afya na elimu. Lakini pia mfano mzuri wa uwezeshaji wa wazawa ni ule wa wakandarasi wa humu nchini.” Alisema Linda.
Mtaalamu huyo wa NMB aliwaambia mabalozi hao kutoka Misri, Pakistani, Kenya, Uganda, Falme za Nchi za Kiarabu na Sweden ambazo ni moingoni mwa nchi ambazo kampuni zao zinashiriki katika kutekeleza miradi ya kimkakati kuwa, Benki yao ina jukumu la kuwahudumia wenyeji lakini pia kuhakikisha kuwa wafanyabiashara na wawekezaji wa nje nao wananufaika na huduma zao bora za rejareja na zile za wateja wakubwa.
Bi. Teggisa alilifafanua hilo kwa kueleza jinsi Benki ya NMB inavyoshiriki katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwa kumsaidia mkandarasi mkuu wa mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki ambayo balozi wake hapa nchini alikuwa kwenye msafara wa TCCIA uliotembelea banda la benki hiyo.
Uwekezaji huu mkubwa wa kipekee kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania na uwezeshaji wa kuigwa, ndiyo uliyoifanya TCCIA na ujumbe wake wa mabalozi nane kati ya kumi iliyokuwa imewaalika kutembelea Saba Saba ya mwaka huu kufika katika banda la Benki ya NMB.
Rais wa chemba ya TCCIA, Bw. Paul Koyi, aliishukuru Benki ya NMB kwa kuyapa kipaumbele maslahi ya Watanzania na kuongoza kuchangia maendeleo ya nchi.
No comments:
Post a Comment