Dar es Salaam; November 5, 2026 - Benki ya NMB imepata mkopo wa dola za Marekani milioni 30 kutoka Benki ya Maendeleo ya China (China Development Bank – CDB), kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa biashara ndogo na za kati nchini Tanzania, hatua inayolenga kuchochea uwekezaji, kupanua shughuli za biashara na kuongeza fursa za ajira.
Makubaliano ya mkopo huo yametiwa saini katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Benki ya NMB jijini Dar es Salaam, yakilenga kuongeza uwezo wa benki hiyo kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wanaohitaji mitaji ya kuendeleza shughuli zao, wakiwemo wanaojihusisha na biashara kati ya Tanzania na China.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, amesema upatikanaji wa mitaji ya kutosha bado ni changamoto kwa wajasiriamali wengi, licha ya mchango mkubwa wa biashara ndogo na za kati katika uchumi wa taifa.
“Biashara ndogo zina mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania, lakini upatikanaji wa mitaji ya kutosha bado ni changamoto kwa wajasiriamali wengi. Mkopo huu wa dola milioni 30 utaongeza uwezo wetu wa kukidhi mahitaji yao ya fedha, kusaidia upanuzi wa biashara na kurahisisha shughuli za kibiashara,” amesema Zaipuna.
Amesema ushirikiano huo pia utaimarisha uhusiano wa NMB na taasisi za kifedha nchini China, huku ukiongeza fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania wanaoagiza na kuuza bidhaa katika soko la China.
Kwa mujibu wa Zaipuna, NMB tayari inatoa huduma za malipo kwa kutumia sarafu ya China (RMB), akaunti za biashara kwa sarafu hiyo pamoja na ufadhili wa biashara za kimataifa kupitia ushirikiano wake na mfumo wa malipo wa Cross-border Interbank Payment System (CIPS).
Ameongeza kuwa benki hiyo pia inawaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wazalishaji pamoja na wasambazaji wa bidhaa nchini China kupitia ziara za maonesho ya biashara ya Canton Fair, hatua inayosaidia kupanua masoko na kujenga mahusiano mapya ya kibiashara.
NMB YAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA KWA BIASHARA
Makubaliano hayo yanafikiwa wakati NMB ikiwa imetambuliwa na jarida la kimataifa la Global Finance kuwa Benki Bora kwa Biashara Ndogo na za Kati nchini Tanzania kwa mwaka 2026.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha uhusiano wa kifedha kati ya Tanzania na China na kuongeza uwezo wa sekta binafsi kupata mitaji kwa ajili ya uwekezaji na uzalishaji, sambamba na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
No comments:
Post a Comment