Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_301026_111126

Stanbic Bank Banner_201026

Thursday, 12 November 2026

AIRTEL YATEMBELEA TUME YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI, YAIMARISHA USALAMA WA TAARIFA ZA WATEJA

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia (kulia), akimkaribisha kwa salamu Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Bw. Charles Kamoto, wakati wa ziara yake katika ofisi za Tume jijini Dodoma.

Dodoma, Novemba 10, 2026 – Kampuni ya Airtel Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi wa taarifa binafsi za wateja ili kuhakikisha usalama wa huduma zake za kidijitali na kuendelea kutoa huduma bora.

Dhamira hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, wakati wa ziara maalum ya heshima katika ofisi za Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), ambapo alikutana na Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Dkt. Emmanuel Lameck Mkilia, pamoja na viongozi wengine.

Katika ziara hiyo, Kamoto aliishukuru Tume kwa mwongozo na ushirikiano inaoutoa kwa Airtel katika kuhakikisha kampuni inazingatia matakwa ya mfumo wa ulinzi wa taarifa binafsi. Alieleza kuwa mafunzo na miongozo iliyotolewa kwa wafanyakazi wa Airtel imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uelewa kuhusu namna sahihi ya kuchakata, kuhifadhi na kushughulikia taarifa za wateja.

Alisisitiza kuwa ulinzi wa taarifa binafsi haupaswi kuonekana kama suala la kutimiza matakwa ya kisheria pekee, bali ni sehemu muhimu ya uendeshaji wa biashara na kujenga uhusiano wa kudumu na wateja.

“Kwa Airtel Tanzania, kulinda taarifa binafsi si wajibu wa kutimiza matakwa ya kisheria pekee, bali ni jukumu la msingi na sehemu muhimu ya namna tunavyoendesha biashara yetu. Kulinda taarifa za wateja ni muhimu katika kujenga na kudumisha imani pamoja na mahusiano ya muda mrefu,” alisema Kamoto.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo inaendelea kuwekeza katika mafunzo na programu za uhamasishaji kwa wafanyakazi wake, sambamba na kuweka sera na mifumo ya ndani inayolenga kuhakikisha kuwa masuala ya ulinzi wa taarifa binafsi yanazingatiwa katika shughuli zote za kila siku.

Kwa mujibu wa Kamoto, hatua hizo zina umuhimu zaidi wakati Airtel ikiendelea kupanua huduma zake za kidijitali na mipango ya ujumuishaji wa huduma za kifedha, ambayo inahitaji mifumo imara ya kuhakikisha taarifa za wateja zinatunzwa na kushughulikiwa kwa usalama.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Lameck Mkilia, aliipongeza Airtel Tanzania kwa kutembelea ofisi za Tume na kutambua umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za udhibiti na sekta binafsi.

Alisisitiza umuhimu wa kampuni na taasisi mbalimbali kuelewa dhamira ya Tume, hususan katika kuhakikisha zinaweka mifumo imara ya kulinda na kuhifadhi taarifa binafsi za wateja wao.

“Naipongeza Airtel Tanzania kwa utayari wake wa kushirikiana na Tume katika kuunga mkono utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kuendeleza safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali na kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wananufaika na fursa za kidijitali,” alisema Dkt. Mkilia.

Airtel Tanzania imesisitiza kuwa itaendelea kuthamini na kuimarisha ushirikiano wake na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi katika kukuza usimamizi na utunzaji sahihi wa taarifa binafsi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga mazingira salama na yenye kuaminika kwa matumizi ya huduma za kidijitali nchini.

No comments:

Post a Comment