Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_170926_270926

Absa Banner_170926_270926

Stanbic Bank Banner_070826

Stanbic Bank Banner_070826

Thursday, 8 October 2026

KOMBE LA EPL KUTUA TANZANIA, GUINNESS KUWAPA MASHABIKI FURSA YA KULISHUHUDIA DAR ES SALAAM

Dar es Salaam - Oktoba 8, 2026: Mashabiki wa Ligi Kuu ya England nchini Tanzania wanajiandaa kushuhudia tukio la kipekee baada ya Kombe la Ligi hiyo kutua rasmi nchini kwa mara ya kwanza kupitia Guinness, Mdhamini Mkuu wa Bia wa Ligi Kuu ya England.

Kombe hilo litawasili nchini Ijumaa, Oktoba 9, 2026, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) majira ya saa tatu asubuhi, kabla ya kuzungushwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ili kuwapa mashabiki fursa ya kuliona kwa karibu.

Kwa mashabiki wa EPL ambao wamezoea kuliona Kombe hilo likikabidhiwa baada ya msimu kumalizika kupitia televisheni, safari hii watapata nafasi ya kuliona moja kwa moja katika jiji lao.

Baada ya kuzunguka katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Kombe hilo litahamia The Super Dome, Masaki, ambako kutakuwa na hafla maalum itakayowapa wageni na mashabiki fursa ya kuliona kwa karibu zaidi na kupiga picha nalo.

Guinness Kuleta Uzoefu wa EPL Karibu na Mashabiki

Akizungumzia ujio wa Kombe hilo, Mkurugenzi wa Ubunifu na Masoko wa Serengeti Breweries Limited (SBL), Henry Esiaba, alisema Guinness inaleta uzoefu wa EPL karibu zaidi na mashabiki wa soka nchini.

“Mashabiki wa Tanzania wana mapenzi makubwa na Ligi Kuu ya England na kila wiki wanafuatilia mechi, wanajadili timu zao na kusherehekea pamoja. Safari hii tunataka kuwapa nafasi ya kuona Kombe lenyewe kwa karibu na kuwa sehemu ya tukio hili. Ni fursa kwa mashabiki kupata uzoefu tofauti na ule wanaoupata wanapotazama mechi kwenye televisheni,” alisema Esiaba.

 

Burudani ya soka itaendelea Jumamosi, Oktoba 10, ambapo mashabiki watakutana katika Uwanja wa KMC, Mwenge, kwa Guinness Matchday.

Katika tukio hilo, mashabiki watapata fursa ya kushuhudia kwa pamoja mechi za Ligi Kuu ya England kupitia skrini kubwa, ikiwemo mchezo wa Arsenal dhidi ya Leeds pamoja na Manchester United dhidi ya Tottenham Hotspur.

EPL na Dabi ya Kariakoo

Lakini kwa kuwa soka Tanzania lina ladha yake, siku hiyo mashabiki pia watapata nafasi ya kushuhudia Dabi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga mubashara kupitia skrini kubwa zitakazowekwa katika eneo la tukio.

Hii itakuwa fursa kwa mashabiki wa soka kukutana sehemu moja, kufuatilia mechi za Ligi Kuu ya England na wakati huohuo kushuhudia moja ya mechi zinazovuta hisia kubwa zaidi katika soka la Tanzania.

Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kampuni wa SBL, Juanita Mramba, alisema ujio wa Kombe hilo unalenga kuwaleta pamoja mashabiki na wadau wa soka kupitia uzoefu unaounganisha soka la kimataifa na shauku ya mashabiki wa Tanzania.

“Soka linawajumuisha watu wengi na Tanzania ni moja ya nchi ambazo mashabiki wake wanaishi kwa karibu sana na mchezo huu. Kupitia ujio wa Kombe la EPL, tunataka mashabiki wapate nafasi ya kuliona kwa macho yao, kupiga picha nalo na kushiriki katika matukio yatakayowakutanisha pamoja. Hii ni nafasi ya kusherehekea soka na mashabiki ambao wamekuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa mchezo huu,” alisema Juanita.

 

Fursa ya Kupiga Picha na Kombe

Mbali na kutazama mechi, mashabiki watakaohudhuria Guinness Matchday watapata pia fursa ya kupiga picha na Kombe la Ligi Kuu ya England, huku wakifurahia burudani na mazingira ya pamoja ya kusherehekea soka.

Ujio wa Kombe hilo Tanzania unaifanya Dar es Salaam kuwa sehemu ya ziara maalum ya Kombe la Ligi Kuu ya England katika Afrika Mashariki, huku Guinness ikiendelea kutumia nafasi yake kama Mdhamini Mkuu wa Bia wa Ligi hiyo kuwaleta mashabiki karibu na mchezo wanaoupenda.

Kwa siku mbili, Oktoba 9 na 10, macho ya mashabiki wa soka yataelekezwa Dar es Salaam, kuanzia ujio wa Kombe hilo JNIA, safari yake katika maeneo mbalimbali ya jiji, hafla ya The Super Dome, Masaki, hadi Guinness Matchday katika Uwanja wa KMC, Mwenge.

Kwa mashabiki wa EPL na soka kwa ujumla, hii ni nafasi ya kipekee ya kuliona Kombe la Ligi Kuu ya England kwa karibu na kusherehekea soka pamoja na mashabiki wengine.


Kitomari Banking & Finance Blog

Follow Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari zaidi za biashara, benki, fedha, kampuni na matukio ya kiuchumi.

LinkedIn | Facebook | Instagram | X (Twitter)

No comments:

Post a Comment