Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_170926_270926

Absa Banner_170926_270926

Stanbic Bank Banner_070826

Stanbic Bank Banner_070826

Monday, 28 September 2026

VODACOM TANZANIA YAUNGANA NA VIONGOZI WA SEKTA YA BIASHARA KATIKA CEO GOLF TOURNAMENT 2026

Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando (kulia), akikabidhi zawadi kwa mshindi wa jumla kwa upande wa wanaume, Thomas Mwangi (kushoto), katika mashindano ya CEO Golf Tournament 2026, yaliyofanyika Septemba 26, 2026, katika viwanja vya Sea Cliff Golf Course, Zanzibar.

Mashindano hayo yaliwakutanisha viongozi wa biashara, Maafisa Watendaji Wakuu (CEOs), wanadiplomasia na wadau mbalimbali kutoka Tanzania na mataifa mengine ya Afrika, huku Vodacom Tanzania Plc ikiwa mdhamini mkuu wa tukio hilo lililolenga kuimarisha mahusiano, kujenga mitandao ya kibiashara na kukuza ushirikiano miongoni mwa viongozi wa sekta mbalimbali.

Zanzibar; Septemba 27, 2026 - Vodacom Tanzania Plc imeendelea kutumia mchezo wa golf kama jukwaa la kuunganisha viongozi wa biashara, makampuni, watoa maamuzi na wadau wa sekta mbalimbali kupitia ushiriki na udhamini wake katika CEO Golf Tournament 2026, iliyofanyika Septemba 26 katika Sea Cliff Golf Course, Zanzibar.

Mashindano hayo yaliwakutanisha viongozi wa makampuni, Maafisa Watendaji Wakuu (CEOs), wanadiplomasia na wachezaji wa golf kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali ya Afrika, yakiwemo Kenya, Uganda, Zambia, Malawi, Afrika Kusini na Nigeria.

Mkuu wa Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Business wa Vodacom Tanzania Plc, Joseph Sayi (kushoto), akikabidhiwa zawadi na Afisa Masoko wa kampuni hiyo, Chelsea Njau, baada ya kuibuka mshindi wa pili katika Mashindano ya CEO Golf Tournament 2026.

Zaidi ya wachezaji 80 kutoka mataifa hayo walishiriki mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Vodacom Tanzania Plc.

Wachezaji kutoka Kenya, Thomas Mwangi na Caroline Muigai, walitwaa ubingwa wa jumla kwa wanaume na wanawake mtawalia katika mashindano hayo yaliyochezwa kwa mfumo wa Stableford kwenye mashimo 18.

Mwangi alitwaa ubingwa wa jumla kwa wanaume baada ya kukusanya pointi 40, huku Muigai akiibuka kinara kwa wanawake kwa pointi 41.

Katika Division A, Patrick O’Rourke alitwaa nafasi ya kwanza, huku Ernest Sengeu akimaliza wa pili kwa pointi 31.

Thagaran Govender alishinda Division B kwa pointi 39, akifuatiwa na Gregory Eayrs aliyepata pointi 38.

Katika Division C, Abbas Simkoko alitwaa ushindi kwa pointi 40, akifuatiwa na Joseph Sayi aliyepata pointi 37.

Kwa upande wa wanawake, Salome Gakere alishinda kwa pointi 36, huku Vicky Elias akimaliza nafasi ya pili kwa pointi 35 baada ya kuibuka na matokeo sawa na Maryanne Mugo na kuamua kwa mfumo wa countback.

Ushiriki wa Vodacom Tanzania katika mashindano hayo umeenda zaidi ya mchezo wa golf na kuwa sehemu ya namna kampuni inavyotumia majukwaa ya michezo kujenga na kuimarisha mahusiano na jumuiya ya biashara, huku ikiunganisha teknolojia na huduma za kidijitali katika mahusiano hayo kwa lengo la kuchochea ukuaji wa biashara.

Akizungumza wakati wa mashindano hayo, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, alisema kampuni hiyo inajivunia kuunga mkono mashindano yanayounganisha michezo na jamii ya wafanyabiashara.

“Tunafurahi kudhamini na kushiriki mashindano ya CEO Golf Tournament kwa sababu gofu si mchezo pekee, bali ni jukwaa linalowakutanisha watu, mawazo na fursa,” alisema Kamando.

Alisema mashindano hayo yanatoa mazingira rafiki kwa viongozi wa biashara kutoka sekta mbalimbali kukutana na kujenga mahusiano ya kikazi.

Kamando pia alihusisha mashindano hayo na juhudi za kukuza utalii visiwani Zanzibar, akisema matukio ya kimataifa ya michezo yanaweza kuitangaza Zanzibar kwa wageni ambao wanaweza kurejea kwa ajili ya utalii au shughuli za kibiashara.

“Tunajivunia kushiriki katika kuitangaza Zanzibar kama kituo cha biashara, utalii na michezo. Matukio kama haya yanaongeza thamani si kwa washiriki pekee, bali pia kwa uchumi kwa ujumla,” alisema.

Kwa Vodacom Tanzania, ushiriki katika majukwaa kama CEO Golf Tournament unaipa kampuni nafasi ya kukutana na viongozi wanaofanya maamuzi katika sekta ya biashara, kusikiliza mahitaji yao na kuendeleza mazungumzo kuhusu namna teknolojia inavyoweza kusaidia biashara kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Ushiriki huo pia unaendelea kuwa sehemu ya juhudi za Vodacom Tanzania kujenga mahusiano na viongozi wa makampuni na wadau mbalimbali, kubadilishana mawazo na kuendeleza fursa za ushirikiano katika dunia ya biashara inayozidi kuunganishwa na teknolojia.


Fuata Kitomari Banking & Finance Blog

Kwa habari zaidi kuhusu biashara, benki, fedha, teknolojia na maendeleo ya sekta mbalimbali, endelea kutembelea na kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog.

LinkedIn: https://www.linkedin.com/feed/
Facebook: https://www.facebook.com
Instagram: https://www.instagram.com
X (Twitter): https://x.com/home

Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, akishiriki katika CEO Golf Tournament 2026, iliyofanyika Septemba 26 katika Sea Cliff Golf Course, Zanzibar.
Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Business, Joseph Sayi (kulia), akimkabidhi zawadi mshindi wa pili wa Division A, Ernest Sengeu (kushoto), katika CEO Golf Tournament 2026, Zanzibar.
Mkuu wa Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Business, Joseph Sayi, akishiriki katika CEO Golf Tournament 2026, Zanzibar—jukwaa lililowakutanisha viongozi wa biashara na wadau mbalimbali kutoka Tanzania na Afrika.
Wafanyakazi wa Vodacom Tanzania Plc wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuibuka washindi katika Mashindano ya CEO Golf Tournament 2026, yaliyofanyika Septemba 26, 2026, katika viwanja vya Sea Cliff Golf Course, Zanzibar.

No comments:

Post a Comment