Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Stanbic Bank Banner_070826

Stanbic Bank Banner_070826

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

Tuesday, 8 September 2026

VODACOM DIGITAL ACCELERATOR NA BRIDGE FOR BILLIONS WAINGIA UBIA KUIMARISHA MFUMO WA UJASIRIAMALI TANZANIA

Mkurugenzi wa Programu za Afrika wa Bridge for Billions, Liliosa Mbirimi (kulia), akizungumza wakati wa kutangazwa kwa ushirikiano wa miaka mitatu kati ya Vodacom Digital Accelerator (VDA) na Bridge for Billions, unaolenga kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini kwa kuwafikia zaidi ya wajasiriamali na wabunifu 1,000 na kusaidia biashara zaidi ya 40 kukua na kupanuka.

Ushirikiano huo ulitangazwa wakati wa Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz) 2026, Septemba 3, 2026, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando.
Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, akizungumza wakati wa kutangazwa kwa ushirikiano mpya wa miaka mitatu kati ya Vodacom Digital Accelerator (VDA) na Bridge for Billions, unaolenga kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini na kuwawezesha wajasiriamali na wabunifu kukua.

Ushirikiano huo ulitangazwa wakati wa Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz) 2026, Septemba 3, 2026, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Programu za Afrika wa Bridge for Billions, Liliosa Mbirimi.

Dar es Salaam, Septemba 4, 2026: Vodacom Tanzania Plc imeingia katika ubia wa miaka mitatu na Bridge for Billions, mtandao wa kimataifa wa ujasiriamali, kwa lengo la kupanua wigo na kuongeza matokeo ya mpango wa Vodacom Digital Accelerator (VDA) nchini Tanzania.

Kupitia ubia huo, taasisi hizo mbili zinalenga kujenga uwezo wa taasisi zinazosaidia wajasiriamali (Entrepreneurship Support Organizations – ESOs) kote nchini, hatua inayotarajiwa kuwawezesha kuwafikia zaidi ya wajasiriamali 1,000 na kusaidia biashara zaidi ya 40 kukua na kupanuka katika kipindi cha miaka mitatu.

KUWEKEZA KATIKA MFUMO WA UJASIRIAMALI

Ushirikiano huo unaashiria hatua mpya katika utekelezaji wa Vodacom Digital Accelerator, ambapo pamoja na kuendelea kusaidia biashara changa moja kwa moja, mpango huo sasa utawekeza pia katika kuimarisha taasisi na vituo vinavyowasaidia wajasiriamali.

Taasisi zitakazonufaika zitajumuisha vituo vya kulea na kukuza biashara changa, vituo vya ujasiriamali, vyuo vikuu pamoja na mashirika ya maendeleo ya biashara yanayowasaidia waanzilishi wa biashara.

Kwa mujibu wa mpango huo, uwekezaji huu unalenga kujenga mfumo imara wa ujasiriamali ambao utaendelea kutoa msaada kwa wajasiriamali hata baada ya kumalizika kwa programu maalumu ya kundi fulani la washiriki.

BRIDGE FOR BILLIONS KUTOA UTAALAMU

Kupitia makubaliano hayo, Bridge for Billions italeta nchini utaalamu wake katika programu za kulea na kukuza biashara changa (incubation), teknolojia za kidijitali na ujenzi wa uwezo wa taasisi zinazosaidia wajasiriamali.

Taasisi zitakazochaguliwa zitapatiwa mafunzo maalumu, zitawezeshwa kutumia zana na mifumo ya Bridge for Billions, pamoja na kupata msaada katika kubuni na kuendesha programu zao za ujasiriamali.

Aidha, taasisi hizo zitaunganishwa na mtandao wa kimataifa wa washauri na taasisi zinazosaidia wajasiriamali. Hii itawapa fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga mahusiano na taasisi nyingine kutoka sehemu mbalimbali duniani.

WAFANYABIASHARA KUNUFAIKA NA MSAADA WA KINA

Wajasiriamali watakaopatikana kupitia taasisi hizo watapitia mchakato maalumu wa kulea na kukuza biashara zao, huku biashara zitakazoonesha uwezo mkubwa wa kukua zikiendelea katika hatua ya acceleration.

Katika hatua hiyo, biashara zitapatiwa msaada wa kina zaidi katika kukuza shughuli zao, kuimarisha mifumo ya biashara na kujiandaa kwa fursa za uwekezaji.

Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa wajasiriamali hawapati tu mafunzo ya muda mfupi, bali wanapata mazingira yanayowawezesha kujenga biashara endelevu na zenye uwezo wa kupanuka.

VODACOM DIGITAL ACCELERATOR YAENDELEA KUJENGA BIASHARA

Tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2019, Vodacom Digital Accelerator imekuwa ikiunga mkono biashara changa na zinazokua zinazotumia teknolojia kutengeneza bidhaa na huduma zenye uwezo wa kukua katika sekta mbalimbali.

Sekta zilizofaidika na programu hiyo ni pamoja na afya, kilimo, elimu na huduma za kifedha, miongoni mwa nyingine.

Kupitia awamu zake mbalimbali, VDA imewapatia wajasiriamali mafunzo, ushauri wa kitaalamu, teknolojia, fursa za kuunganishwa na wawekezaji pamoja na fursa za kufikia mitandao na washirika wa Vodacom.

Ubia huu wa miaka mitatu unaendeleza safari ya VDA kutoka kwenye programu zinazotekelezwa kwa awamu moja baada ya nyingine hadi kwenye uwekezaji wa muda mrefu katika kuimarisha mfumo mzima wa ujasiriamali nchini Tanzania.

KUNDI LA KWANZA KUTANGAZWA OKTOBA 2026

Kundi la kwanza la taasisi zitakazoshiriki katika mpango huu linatarajiwa kutangazwa Oktoba 2026, huku maombi kwa wajasiriamali yakitarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa Septemba 2026.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza fursa kwa wajasiriamali kupata maarifa, mitandao, teknolojia na msaada unaohitajika ili kuanzisha, kuendeleza na kupanua biashara zao.

KUHUSU VODACOM DIGITAL ACCELERATOR

Vodacom Digital Accelerator (VDA) ilianzishwa mwaka 2019 na Vodacom Tanzania Plc kwa lengo la kusaidia biashara changa na zinazokua zinazotengeneza bidhaa na huduma zenye uwezo wa kukua na kufikia masoko mapana.

Kupitia awamu zake mbalimbali, VDA imewapatia wajasiriamali mafunzo, ushauri wa kitaalamu, teknolojia, fursa za kuunganishwa na wawekezaji pamoja na kufikia mitandao na washirika wa Vodacom.

KUHUSU BRIDGE FOR BILLIONS

Bridge for Billions ni mtandao wa kimataifa wa ujasiriamali unaoshirikiana na taasisi za umma na sekta binafsi kubuni na kuendesha programu za kulea na kukuza biashara changa zinazowafikia wajasiriamali kutoka katika mazingira mbalimbali.

Katika kipindi cha takribani muongo mmoja, Bridge for Billions imeendesha karibu programu 400 za ujasiriamali, kusaidia karibu wajasiriamali 7,000 kukamilisha programu za kulea na kukuza biashara, na kujenga jumuiya ya zaidi ya washauri wa kujitolea 5,000 katika zaidi ya nchi 150.

Bridge for Billions pia hushirikiana na taasisi zinazosaidia wajasiriamali ili kuimarisha uwezo wao wa kubuni, kuendesha na kupima matokeo ya programu za ujasiriamali.

Kwa maelezo zaidi kuhusu Bridge for Billions: www.bridgeforbillions.org

No comments:

Post a Comment