KIGALI, Rwanda — Benki ya NMB imeingia katika ushirikiano na kampuni ya teknolojia ya afya, Dawa Mkononi, unaolenga kuwezesha Mpango wa Ufadhili wa Mitaji kwa maduka ya dawa na viwanda vya dawa.
Mpango huo utasaidia wasambazaji na wafanyabiashara wa bidhaa za dawa wanaokidhi vigezo kupata mitaji ya kuendesha na kukuza biashara zao.
Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosainiwa jijini Kigali, Rwanda, itawezesha NMB kutoa mikopo kupitia jukwaa la kidijitali la Dawa Mkononi, hatua inayolenga kupunguza changamoto za ukwasi zinazoathiri ununuzi, upatikanaji na usambazaji wa dawa katika mnyororo wa huduma za afya.
Mkurugenzi wa Mikakati na Ukuaji wa NMB, Francis Mittah, alisema ushirikiano huo unaonesha fursa iliyopo kwa benki na kampuni za teknolojia kushirikiana kubuni mifumo ya kifedha inayokidhi mahitaji ya biashara kupitia teknolojia za kidijitali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Dawa Mkononi, Joseph Paul, alisema upatikanaji wa mitaji ni sehemu muhimu katika kujenga mnyororo imara na wenye ufanisi wa usambazaji wa dawa, hususan kwa biashara zinazohitaji ukwasi wa kutosha ili kuhakikisha dawa zinapatikana wakati wote.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha zaidi mahusiano kati ya taasisi hizo mbili katika kuendeleza suluhisho za kifedha zinazoongozwa na teknolojia kwa biashara zinazofanya kazi katika mnyororo wa thamani wa sekta ya afya.
No comments:
Post a Comment