KIZIMKAZI, ZANZIBAR: Serikali imesema itaendelea kushirikiana na Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) katika kujenga sekta ya fedha yenye nguvu, ubunifu na jumuishi, kwa lengo la kukuza uchumi wa Taifa na kuongeza fursa za kifedha kwa Watanzania.
Akizungumza katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na TBA huko Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, kwa ajili ya kuadhimisha miaka 30 ya Umoja huo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali inajivunia mchango mkubwa wa sekta ya kibenki katika kustawisha sekta ya fedha nchini.
Amesema katika kipindi cha miaka 30, sekta ya kibenki imepiga hatua kubwa za kimaendeleo na kuwa nguzo muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kwa mujibu wa Mhe. Hemed, Tanzania imepitia mageuzi makubwa katika sekta ya kibenki, ambapo huduma za kifedha zimeondokana na utegemezi mkubwa wa matawi na huduma za ana kwa ana na kuelekea kwenye mifumo ya kidijitali inayounganisha benki, simu za mkononi na mifumo mbalimbali ya malipo.
Amesema mabadiliko hayo yamerahisisha upatikanaji wa huduma za fedha na kuwawezesha mamilioni ya Watanzania kupata huduma za kifedha, mitaji ya biashara, fursa za uwekezaji na kuweka akiba.
“Hatua hiyo imechangia kuleta matokeo chanya, ambapo mamilioni ya Watanzania wameweza kupata huduma za kifedha, mitaji ya biashara, fursa za kuwekeza na kuweka akiba, pamoja na kuchochea uundaji wa ajira na shughuli za uzalishaji, hivyo kuchangia katika kustawisha uchumi wetu,” alisisitiza.
TBA YAWEKA RASILIMALI KWENYE SHUGHULI ZA UZALISHAJI
Awali, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Rahma Mahfoudh, amesema TBA, kupitia mabenki wanachama, imekuwa na mchango mkubwa katika kuelekeza rasilimali fedha kwenye shughuli mbalimbali za uzalishaji na maendeleo ya Taifa.
Ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na biashara, kilimo, viwanda, makazi, miundombinu na miradi ya kimkakati ya Taifa.
Amesema mchango huo unazidi kuimarisha sekta ya fedha, ambayo ni mhimili muhimu katika kuchochea uwekezaji, uzalishaji na ukuaji wa uchumi, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
RASILIMALI ZA BENKI ZAFIKIA SH. TRILIONI 84.6
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania, Bw. Theobald Sabi, amesema sekta ya benki imeendelea kukua kwa kasi, huku jumla ya rasilimali za sekta hiyo zikifikia takribani Sh. trilioni 79.4 hadi mwisho wa mwaka 2025.
Amesema kiwango hicho kiliongezeka hadi takribani Sh. trilioni 84.6 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026.
Katika kipindi hicho, amesema mikopo kwa sekta binafsi iliendelea kukua kwa takribani asilimia 23, hali inayoonesha kuendelea kuimarika kwa nafasi ya sekta ya benki katika kusaidia shughuli za biashara, uwekezaji na uzalishaji nchini.
TBA YAADHIMISHA MIAKA 30
Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) ulianzishwa mwaka 1995, wakati Tanzania ikitekeleza mageuzi makubwa katika sekta ya fedha yaliyolenga kuongeza ushindani, kuhamasisha uwekezaji binafsi, kukuza ubunifu na kuimarisha usimamizi wa sekta ya fedha.
Miaka 30 baadaye, TBA imeendelea kuwa jukwaa muhimu la ushirikiano kati ya mabenki na wadau mbalimbali katika kukuza na kuimarisha sekta ya fedha nchini.
Maadhimisho hayo yanaangazia safari ya mageuzi ya sekta ya kibenki Tanzania na mchango wake katika kuongeza ujumuishi wa kifedha, uwekezaji, biashara na ukuaji wa uchumi.
Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari, uchambuzi na taarifa muhimu kuhusu sekta ya benki, fedha, biashara na uchumi Tanzania.


.jpeg)
.jpeg)




.jpeg)
.jpeg)

No comments:
Post a Comment