Dodoma. Benki ya NMB imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuunga mkono maendeleo ya sekta ya kilimo nchini baada ya kukabidhi hundi ya udhamini kwa Wizara ya Kilimo kwa ajili ya Maonesho ya Nanenane 2026.
Makabidhiano hayo yaliyofanyika jana jioni jijini Dodoma yamefikisha jumla ya mchango wa NMB katika maonesho hayo kufikia Shilingi milioni 572 ndani ya kipindi cha miaka minane mfululizo, yakidhihirisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya benki hiyo na Serikali katika kukuza kilimo, mifugo na uvuvi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango, alisema Maonesho ya Nanenane ni jukwaa muhimu linalowawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kupata maarifa mapya, teknolojia za kisasa pamoja na huduma za kifedha zinazochochea ongezeko la uzalishaji na kufungua fursa mpya za biashara.
Alibainisha kuwa kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo, NMB itaendelea kuwafikia wadau wa sekta ya kilimo kwa suluhisho mbalimbali za kifedha zinazolenga kuongeza tija na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, aliipongeza Benki ya NMB kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika maendeleo ya sekta ya kilimo. Alisema mchango wa benki hiyo umeendelea kuwafikisha wakulima karibu zaidi na huduma za kifedha na kuhimiza NMB kuendeleza ushirikiano huo ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi kupitia elimu ya kifedha, matumizi ya teknolojia na bidhaa zinazokidhi mahitaji ya sekta hiyo.
Ushiriki wa NMB katika Maonesho ya Nanenane unaakisi mkakati wa benki wa kuendelea kusaidia maendeleo ya sekta za uzalishaji, hususan kilimo, ambacho kinaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.
Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari za uhakika, uchambuzi na taarifa za kina kuhusu sekta ya benki, fedha, biashara na uchumi nchini Tanzania.

.jpeg)

No comments:
Post a Comment