Dar es Salaam – Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imezindua rasmi kampeni kabambe ya msimu wa sikukuu yenye lengo la kuwazawadia wateja wake kwa kutoa rejesho la asilimia 10 kwa miamala yote inayofanyika kupitia kadi ya Popote Visa, kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa na benki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Bw. Alex Dwashi, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa Umma wa TCB, amesema kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa benki wa kuimarisha ujumuishi wa kifedha na kuhamasisha matumizi ya malipo ya kidijitali, hasa katika kipindi cha sikukuu ambapo matumizi ya fedha huongezeka kwa kasi.
“Kupitia kampeni hii, TCB inaendelea kuwa karibu na wateja wake kwa kuwapatia suluhisho la malipo lililo salama, rahisi na lenye manufaa zaidi, sambamba na kuunga mkono ajenda ya taifa ya kupunguza matumizi ya fedha taslimu,” alisema Dwashi.
Kwa upande wake, Jesse Jackson, Afisa Mkuu wa Huduma za Kidijitali na Kibunifu wa TCB, amesema rejesho la asilimia 10 kwa watumiaji wa Popote Visa linalenga kuhimiza matumizi ya mifumo ya malipo yasiyotegemea fedha taslimu, ambayo ni salama na yenye ufanisi mkubwa zaidi.
Aliongeza kuwa benki inaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kuboresha huduma zake, kuongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma za kifedha, na kuwapa wateja uzoefu bora zaidi wa kidijitali.
Naye Lilian Mtali, Mkurugenzi wa Biashara za Wateja Wadogo na wa Kati wa TCB, ameeleza kuwa kampeni hiyo inatarajiwa kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja pamoja na kuchochea maboresho ya kimkakati ndani ya benki, huku ikiendeleza ajenda ya kidijitali na ubunifu katika sekta ya fedha nchini.
Kampeni hii itaendelea katika kipindi chote cha msimu wa sikukuu, ambapo TCB imewahimiza wateja wake kuhuisha na kutumia kadi zao za Popote Visa ili kunufaika na ofa hiyo. Benki imesisitiza kuwa kadi ya Popote Visa inakubalika duniani kote na hutoa taarifa za miamala papo hapo, jambo linaloifanya kuwa njia salama, rahisi na ya kisasa ya kufanya malipo ndani na nje ya nchi.
Kwa kampeni hii, TCB inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuleta ubunifu, urahisi na thamani zaidi kwa wateja wake katika kila hatua ya matumizi ya huduma za kifedha.
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
No comments:
Post a Comment