Dkt. Mpango aliyasema hayo wakati akizindua rasmi Matawi ya Benki ya NMB Chanika na Kinyerezi jijini Dar es Salaam. Alieleza kuwa uzinduzi wa matawi hayo utaongeza mchango wa NMB katika maendeleo ya taifa kwa kulipa kodi, kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, na kusaidia usalama wa miamala kama malipo ya bili za maji, umeme, ada za shule, na mauzo ya bidhaa.
Aidha, Makamu wa Rais alitoa wito kwa NMB kuendelea kuchangia kwenye maendeleo ya kijamii hususan katika sekta za afya na elimu. Alisema kuwa uwajibikaji kwa jamii ndio msingi wa kudumu wa mahusiano bora kati ya benki na wananchi.
“Kupitia kuongeza idadi ya mawakala wenu, mtakuwa mnasaidia kuzalisha ajira kwa vijana ambao ni wadau muhimu wa huduma hizi. Ninaipongeza NMB kwa juhudi hizi na nawasihi msiishie hapa, bali muendelee kuwekeza zaidi katika elimu ya fedha kwa wananchi, hasa wale wa vijijini,” alisema Dkt. Mpango.
Makamu wa Rais alisisitiza umuhimu wa kubuni mikakati bora ya kuongeza uelewa wa masuala ya fedha miongoni mwa wananchi. Aliitaka NMB kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania na Umoja wa Mabenki kubuni programu za kuongeza elimu ya kifedha, huku akitoa rai ya kupunguza gharama za huduma za kidijitali ili ziweze kufikiwa na watu wengi zaidi.
Aliongeza kuwa Sekta ya Benki na Fedha imeendelea kukua na kuonesha mafanikio makubwa, ambapo mchango wake kwenye ukuaji wa Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 2.3 mwaka 2019 hadi asilimia 8.6 mwaka 2023. Dkt. Mpango alihimiza NMB kujizatiti kwa mikakati madhubuti ya kuhimili mitikisiko ya kiuchumi, magonjwa, na changamoto nyingine za kimataifa.