Foreign Exchange Rates

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

Wednesday, 5 February 2025

UNDP, VODACOM NA COSTECH KUADHIMISHA WIKI YA UBUNIFU NA MKUTANO WA FUTURE READY SUMMIT

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Phillip Besiimire (kushoto), Mkurugenzi wa Kituo cha Uendelezaji na Uhawilishaji wa Teknolojia, Dkt. Athman Mgumia (kati) akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH na Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania Shigeki Komatsubara wakiwa pamoja wakati wa kutangaza ushirikiano wao ili kuandaa Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz2025) na Future Ready Summit 2025 yanayolenga kuangazia bunifu na maandalizi ya maisha katika wakati ujao, hafla hii imefanyika mnamo tarehe 5 Februari 2025 jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam | Februari 5, 2025 - Kwa lengo la kuimarisha ubunifu na kuendesha mabadiliko ya kidijitali, Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania kupitia programu yake ya FUNGUO, Vodacom Tanzania, na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) wametangaza ushirikiano wa pamoja wa kuandaa Wiki ya Ubunifu Tanzania 2025 (IWTz2025). Tukio hili kubwa, litakalojumuisha Mkutano wa Future Ready wa Vodacom, litafanyika kuanzia tarehe 12 hadi 16 Mei 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, pamoja na shughuli zitakazofanyika katika maeneo mbalimbali nchini.


Mada ya mwaka huu, “Ubunifu kwa Maendeleo Jumuishi na Yenye Ustahimilivu”, ikilenga kuonyesha dhamira ya pamoja ya kujenga jamii endelevu, jumuishi na ya kisasa katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana kwenye zama hizi za kidijitali na kuchochea ukuaji wa kibiashara kupitia tafiti na ubunifu.


Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Phillip Besiimire, alisisitiza kuwa, “Ushirikiano huu unaleta mabadiliko katika sekta ya ubunifu nchini Tanzania, kwa kuunganisha wabunifu na wajasiriamali wa kimataifa kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Kwa kuleta mitazamo na taaluma za kimataifa kwenye mijadala hii, tunalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mabadiliko ya kidijitali, sambamba na kuanzisha mifumo ya ikolojia ya ubunifu inayoongozwa na vijana. Jitihada za Vodacom za kutumia teknolojia kwa lengo la kuboresha maisha ndio zinazounda msingi wa ushirikiano huu unaoendeshwa na maono yanayofanana ya kuwawezesha watanzania kuendelea kupitia Uchumi wa kidijitali ulioendelevu na jumuishi.”

Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom aliongeza kuwa, mkutano wa Vodacom wa Future Ready Summit (FRS2025) ni tukio linaloweka msingi wa maadhimisho hayo pamoja na kuibeba kauli mbiu ya “Kubadilisha hatma ya miji: Usasa, Uendelevu na Jumuishi”, ambayo inadokeza umuhimu wa kuibadili miji ya Tanzania kwa ajili ya kutatua changamoto zinazotokana ukuaji wa kasi, mabadiliko ya tabia nchi na mabadiliko ya teknolojia.

Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara, amesisitiza dhamira ya UNDP ya kujenga mfumo wa ubunifu ulio jumuishi na wenye ustahimilivu. “Tunatambua kuwa ubunifu ni nyenzo muhimu katika kushughulikia changamoto za maendeleo endelevu na kuunda fursa shirikishi. Kupitia ushirikiano huu, tunalenga kuwainua Watanzania, hasa vijana na wanawake, kuwa chachu ya mabadiliko chanya. Wiki ya Ubunifu Tanzania 2025 (IWTz2025) itaonyesha ari ya ubunifu Tanzania kwenye jukwaa la kimataifa, kuvutia uhamasishaji na ushirikiano kupitia na mifumo iliyofanikiwa duniani.”

Ajenda ya maadhimisho hayo itahusisha hotuba, mijadala mtambuka, warsha na maonyesho, huku lengo likiwa ni:
  • Mustakabali wa miji mahiri, endelevu na jumuishi
  • Uwezeshaji wa vijana kwenye zama za kidijitali
  • Uboreshaji wa tafiti na ubunifu kwa ajili ya biashara
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo na Uhamisho wa Teknolojia kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Athumani Ngumia alisema kuwa mchango muhimu wa ushirikiano huo ni kukuza ubunifu.

COSTECH imejidhatiti kuwaunganisha wadau kwa lengo la kuchochea utafiti, teknolojia na ubunifu ambao unaendana na vipaumbele vya nchi katika maendeleo na maono ya mwaka 2050. Maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu kwa mwaka 2025 ni jukwaa pekee kwa ajili ya sekta binafsi na umma kupeleleza na kutekeleza masuluhisho kwa ajili ya ukuaji endelevu.


Wiki ya ubunifu 2025 (IWTZ2025) na mkutano wa Future Ready Summit (FRS2025) inatarajia kuwaleta pamoja washiriki, wazungumzaji na wabunifu kutoka Tanzania, Afrika na sehemu mbalimbali duniani na kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana maarifa, kuendeleza ushirikiano wenye tija na kuhamasisha mawazo yenye kuleta mabadiliko.

Washiriki wa matukio haya wanahamasishwa kutekeleza shughuli mbalimbali sambamba na matukio hayo muhimu kwa lengo la kuhakikisha watu wengi zaidi nchini wanaweza kunufaika na mikutano hiyo itakayo kuwa inafanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.

Kuhusu programu ya FUNGUO

Programu ya FUNGUO umejitolea kuendeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) nchini Tanzania kwa kutumia mbinu shirikishi inayolenga kusaidia maendeleo ya biashara bunifu na zinazozingatia athari chanya kwa jamii, hususan kwa kuimarisha mazingira ya ubunifu kwa wajasiriamali na biashara ndogo na za kati (MSMEs). FUNGUO inatambua kuwa kusaidia na kukuza biashara hizi siyo tu kutachangia kuongeza ajira, hususan kwa wanawake na vijana, bali pia kutaboresha kipato, kuboresha hali ya maisha, na kuchochea maendeleo jumuishi na endelevu.

Mpango huu unafadhiliwa kwa pamoja na Umoja wa Ulaya (kupitia Mpango wa BEGIN), Serikali ya Uingereza (kupitia Mpango wa Ushirikiano wa Teknolojia na Ubunifu barani Afrika - ATIP), na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). FUNGUO unatekelezwa na UNDP Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF). Ushirikiano huu wa wadau mbalimbali unahakikisha ufanisi na athari chanya katika mazingira ya ubunifu nchini Tanzania. Kwa kushirikiana kwa karibu na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) pamoja na taasisi nyingine za serikali, FUNGUO inalenga kuchangia maendeleo endelevu nchini kwa kuweka mazingira wezeshi kwa biashara bunifu na MSMEs.

​​Kuhusu Vodacom Tanzania


Vodacom Tanzania PLC ni mtoa huduma wa mawasiliano anaeongoza nchini Tanzania, ikiwa na mtandao wa data wa kasi zaidi. Tunahudumia zaidi ya wateja milioni 26.3. Vodacom Tanzania na kampuni zake tanzu ni sehemu ya Vodacom Group yenye usajili nchini Afrika Kusini, ambayo nayo inamilikiwa na Vodacom Group Plc yenye makao makuu Uingereza. Vodacom Tanzania imesajiliwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) chini ya namba ya usajili ISIN: TZ1886102715 na jina la hisa: VODA.

Kwa maelezo zaidi, tafadhali tembelea tovuti yetu: www.vodacom.co.tz

Kuhusu COSTECH

Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) ilianzishwa kupitia Sheria ya Bunge Na. 7 ya mwaka 1986, ikichukua nafasi ya Baraza la Utafiti wa Kisayansi la Tanzania (UTAFITI). COSTECH ni shirika la umma linalohusika na kuratibu na kukuza shughuli za utafiti na maendeleo ya teknolojia nchini. Pia, inatoa ushauri kwa serikali kuhusu masuala yote yanayohusiana na sayansi, teknolojia, na ubunifu (STI) kwa lengo la kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.

COSTECH inafanya kazi chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Tume hii ina jukumu la kuandaa na kusimamia utekelezaji wa sera za sayansi na teknolojia, kuratibu tafiti mbalimbali, na kuhakikisha teknolojia za kisasa,zinazotengenezwa nchini au kuagizwa kutoka nje zinatumika ipasavyo. Pia, COSTECH inakusanya na kusambaza taarifa muhimu kuhusu sayansi na ubunifu, inahamasisha jamii ili kufanya mada hizi kufikika zaidi, na inashirikiana na mashirika ya kimataifa ili kuimarisha maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia nchini. Zaidi ya hayo, inahakikisha upatikanaji wa fedha za kusaidia miradi ya utafiti na ubunifu, na kutoa ushauri kwa serikali kuhusu masuala ya sayansi na teknolojia.

No comments:

Post a Comment