WANANCHI, VIKUNDI VYA KIJAMII WETE, PEMBA VYAPIGWA MSASA NMB KIJIJI DAY
Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Pemba, imewataka Wananchi na Vikundi vya Kijamii na Ushirika Wilaya ya Wete, kuitumia vema Elimu ya Fedha na Huduma Jumuishi za Kibenki zikiwemo za bima na mikopo nafuu zilizotolewa kupitia Tamasha la NMB Kijiji Day lililofanyika Kijiji cha Gando, wiki chache baada ya kufungua tawi jipya la NMB Wete.
Wito huo, umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bi. Salama Mbarouk Khatib, wakati akifungua NMB Kijiji Day – Jukwaa linaloendeshwa na benki hiyo, likilenga kufikisha Elimu na Huduma Jumuishi za Kifedha kwa Watanzania walioko pembezoni, hasa wanaoishi katika maeneo yasiyofikiwa na huduma hizo muhimu.
NMB ilifungua tawi jipya la benki hiyo mjini Wete mwezi uliopita, kabla ya wikiendi iliyopita kufanya NMB Kijiji Day – jukwaa lililokuwaweka pamoja wananchi na wanachama wa vikundi mbalimbali vya kijamii kutoka Vijiji vya Gando na Junguni, ambao wanatajwa kuongoza kwa mitazamo hasi ya kuficha fedha ndani.
Mada mbalimbali zilitolewa katika semina iliyohusisha Vikundi vya Kijamii zaidi ya 10 vyenye wanachama zaidi ya 200 katika vijiji vya Gando na Junguni, iliyoendeshwa na Meneja Mahusiano na Amana wa NMB, Bi. Monica Job, Meneja Mauzo wa NMB Kanda ya Zanzibar, Muhsin Nahoda Mohamed, pamoja na Meneja Biashara wa NMB Kanda ya Zanzibar, Naima Said Shaame.
Akizungumza na wananchi wakati wa ufunguzi wa NMB Kijiji Day, Bi. Salama, wananchi na vikundi vya kijamii vya vijiji hivyo na mkoa mzima wa Kaskazini Pemba vinapaswa kuchangamkia fursa zitokanazo na tamasha hilo, pamoja na tawi jipya la NMB Wete, kwa kufungua akaunti, kuhifadhi pesa zao na kunufaika na huduma za bima, mikopo nafuu na nyinginezo.
Mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Wete, Abdallah Rashid Ali, Bi. Salama alibainisha kwamba, Wananchi na Vikundi vya Kijamii vilivyopo Gando vina rekodi nzuri ya mapato ya fedha, lakini fedha zao zinawekwa majumbani, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wake, hivyo watumie elimu waliyopewa kwenye semina ya programu hiyo kubadilika.
“Hivi karibuni NMB ilifungua tawi Wete, ili kufikisha Huduma Jumuishi za Fedha, hii ni fursa ya wanachi kuitumia kuhakikisha mnafungua akaunti, hasa za Watoto, Chipukizi na Mwanachuo kwa ustawi wa maendeleo yao kielimu. Kwa Wananchi na Vikundi vya Kijamii, fedha haiwekwi ndani, kwani ukiweka ndani utaitumia tu hata kwa matumizi yasiyo ya lazima.
“Kwa hiyo wale ambao wana tabia za kufukia fedha, wale wanaoweka fedfha zao mikekani, wale wanaoziweka fedha mchagoni, niwasisitize kwamba NMB inayafanya haya ili kuwawezesha kukua kiuchumi, kwa hiyo kafungueni akaunti NMB, wekeni pesa zenu ili sio tu mjiwekee pesa mahali salama, bali pia mnufaike na mikopo, bima na fursa mbalimbali.
Kwa upande wake, Meneja wa NMB Kanda ya Zanzibar, Bi. Naima Said Shaame, aliwapongeza wakaazi wa Gando na Junguni kwa kuwa na vikundi vingi vya kijamii vinavyojumuisha wanawake, wanaume na vijana na kwamba NMB Kijiji Day ilikuwa hapo kutoa elimu na kuhakikisha kila mshiriki ananufaika na fursa na huduma zao.
“Tuko hapa kuhakikisha elimu na fursa tulizonazo mnazijua, zinawafikia na mnazitumia ipasavyo. Ujanja ni kuwa na kipato na sio lazima kiwe kikubwa, kwani hata walio na kipato kikubwa wameanzia huku chini,” alisema Bi. Naima, huku akifafanua kwamba akiba sio kiasi cha pesa kinachobaki baada ya matumizi, bali ni tumizi la kwanza la bajeti ya mtu yeyote.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Wete, Abdallah Rashid Ali, aliishukuru na kuipongeza NMB kwa utayari wao katika kuwafikia na kuwafikishia Huduma Jumuishi za Kifedha, na kwamba ufunguzi wa tawi la NMB Wete ni uthbitisho wa hilo na kuwataka wananchi kulitumia tawi hilo kukua kiuchumi wa mtu mmoja mmoja, vikundi na wilaya yao kwa ujumla.
“Niwashukuru pia wakazi wa Gando na Junguni kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki NMB Kijiji Day, wito wetu kama Serikali kwenu ni kuhakikisha mnatumia vema fursa zitokanazo na ujio wa benki hii wilayani mwetu,” alisema DC huyo huku akisema anaamini elimu watakayopata washiriki itabadili mwelekeo wao katika masuala ya fedha.
Akizungumza baada ya semina hiyo, Mwenyekiti wa Kikundi cha Ushirika cha Tuwe Sote cha Kijiji cha Gando, Seif Kassim Hamad, alisema kikundi chake kinachojihusisha na ukulima wa Mwani, ni wanufaika wakubwa sio tu wa elimu ya fedha na Huduma Jumuishi za Kibenki waliyopewa katika NMB Kijiji Day, bali mikopo nafuu ya kilimo ya benki hiyo tangu awali.
Kwa upande wake, Bi. Riziki Salum Khaalfan, Mkazi wa Gando Chaoni na Mwanachama wa Kikundi cha Nyota Njema, aliishukuru NMB kwa semina hiyo, lakini akaenda mbali kwa kuitaka kuhakikisha inasaidia ongezeko la thamani ya bei ya zao la Mwani na kuwafungulia fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.
Naye Warda Juma Kassim wa Kikundi cha Tuwezeshane cha Gando Sokoni, kinachojihusisha na ushonaji na kudarizi nguo, alisema changamoto kubwa inayokwaza ustawi wa vikundi na wanachama wengi ni ukosefu wa mitaji na elimu ya kile wanachokifanya, sambamba na ufinyu wa masoko ya uhakika ya bidhaa wanazozalisha, eneo ambalo anaiomba NMB kuwasaidia.
Tamasha hilo lilitanguliwa na Bonanza la Michezo mbalimbali ikiwemo mbio za magunia, kufukuza kuku, rede, bao, kuvuta kamba na kisha bonanza kufungwa kwa mchezo wa soka kati ya Gando United FC na Junguni United FC, ambazo ziliumana vikali kwenye Uwanja wa Mkwambe na Gando United kushinda kwa penalti 7-6 za Junguni United.
No comments:
Post a Comment