Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Monday, 6 January 2025

DKT. KIKWETE AKOSHWA NA USHIRIKI WA WADAU BINAFSI KWENYE MIRADI YA MAENDELEO, AIPONGEZA BENKI YA NBC

Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete (wa tatu kulia) akikabidhi tuzo maalum kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw. Theobald Sabi (wa pili kulia) ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa benki hiyo katika kufanikisha ujenzi Kituo cha Afya cha Kizimkazi kilichopo Wilaya ya Kusini, Unguja wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa kituo hicho iliyofanyika mwishoni mwa wiki Zanzibar. Wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Afya Zanzibar Bw. Nassor Ahmed Mazrui (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo (kulia).
Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete (kushoto) pamoja na viongozi wengine waandamizi wa chama na serikali visiwani Zanzibar wakisikiliza taarifa fupi kuhusu Kituo kipya cha Afya cha Kizimkazi kilichopo Wilaya ya Kusini, Unguja kutoka kwa Mwenyekiti wa taasisi ya Samia Foundation ambae pia ndio Mhandisi wa mradi huo, Mhandisi Fatma Kara (alieshika fimbo) wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa kituo hicho iliyofanyika mwishoni mwa wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw. Theobald Sabi (wa pili kulia). Benki ya NBC ni mmoja wa wadau muhimu kwenye ujenzi wa kituo hicho kilichojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Samia Foundation.
Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete (wa tatu kushoto) pamoja na viongozi wengine waandamizi wa chama na serikali visiwani Zanzibar wakisikiliza maelezo kuhusu vifaa tiba mbalimbali vilivyopo kwenye Kituo kipya cha Afya cha Kizimkazi kilichopo Wilaya ya Kusini, Unguja kutoka kwa mmoja wa wataalam wa afya kituoni hapo (alieshika mic) wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa kituo hicho iliyofanyika mwishoni mwa wiki.
Ushirikiano na ubia baina ya serikali na wadau mbalimbali ikiwemo taasisi binafsi ni njia rahisi zaidi katika kuchochea kasi ya maendeleo kwa faida ya wananchi. Ushirikiano wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Taasisi ya Samia Foundation, Taasisi ya Ahmed Al Falas Foundation na Benki ya NBC hadi kufanikisha mradi huu ni muendelezo wa mifano mizuri ya kuigwa…hongereni sana,’’ - Dkt. Kikwete.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw. Theobald Sabi (pichani) alisema ushiriki wa benki hiyo kwenye mradi huo ni muendelezo wa jitihada zake kupitia sera yake ya Uwajibikaji kwa Jamii (Citizenship), ambapo benki hiyo imeendelea kutenga sehemu ya faida yake kila mwaka ili kusaidia kutatua changamoto mbalimbali katika sekta za afya, elimu, mazingira, elimu ya fedha, na ajira.
Wananchi wakifuatilia uzinduzi huo.

Zanzibar: Januari 4, 2024 -
 Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete amepongeza ushirikiano baina ya wadau binafsi na serikali katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile inayohusiana na afya, akibainisha kuwa hatua hiyo ni chachu muhimu zaidi katika kuchochea kasi ya maendeleo nchini.

Dkt. Kikwete alitoa pongezi hizo mwisho wa wiki wakati akizindua rasmi Kituo cha Afya cha kisasa cha Kizimkazi kilichopo Wilaya ya Kusini, Unguja, Zanzibar kilichojengwa kwa ushirikiano baina ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wadau mbalimbali hususani Taasisi ya Samia Foundation, Taasisi ya Ahmed Al Falas Foundation na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

Hafla fupi ya uzinduzi wa kituo hicho chenye thamani ya sh bil 4.4 ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya afya visiwani Zanzibar akiwemo Waziri wa Afya Zanzibar Bw Nassor Ahmed Mazrui, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt Mngereza Mzee Miraji na viongozi mbalimbali waandamizi wa chama na serikali.

Zaidi, walikuwepo viongozi na maofisa wa taasisi hizo wadau ambapo taasisi ya Samia Foundation iliongozwa na Mwenyekiti wa taasisi hiyo ambae pia ndio Mhandisi wa mradi huo, Mhandisi Fatma Kara, Muwakilishi wa Taasisi ya Ahmed Al Falas Foundation na maofisa wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw Theobald Sabi pamoja na wananchi.

“Ushirikiano na ubia baina ya serikali na wadau mbalimbali ikiwemo taasisi binafsi ni njia rahisi zaidi katika kuchochea kasi ya maendeleo kwa faida ya wananchi. Ushirikiano wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Taasisi ya Samia Foundation, Taasisi ya Ahmed Al Falas Foundation na Benki ya NBC hadi kufanikisha mradi huu ni muendelezo wa mifano mizuri ya kuigwa…hongereni sana,’’ alipongeza Dkt Kikwete.

Zaidi Dkt Kikwete aliepata wasaa wa kutembelea na kukagua sehemu mbalimbali za kituo hicho alitoa wito kwa viongozi wa serikali na uongozi wa kituo hicho kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi sambamba na kutunza miundombinu mbalimbali ya kituo hicho ili kiendelee kutoa huduma bora inayosadifu dhamira ya kuanzishwa kwake.

“Kufuatia uzinduzi wa kituo hiki cha kisasa zaidi, matarajio ni kwamba wagonjwa wengi wa maeneo haya na jirani watapata huduma za afya huku pasipo kuwa na ulazima wa kwenda hospitali nyingine mbali kidogo na hapa. Hata hivyo ipo haja ya kuhakikisha wataalamu wote muhimu wanapatikana hapa ili kuakisi nia njema za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi,’’ alisisitiza Dkt Kikwete.

Awali wakizungumza kwenye hafla hiyo Waziri Mazrui na Katibu Mkuu Dkt Mngereza walisema uzinduzi huo ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwamba ujenzi wa kituo hicho utasaidia kuhudumia wananchi 13,000 kutoka maeneo ya Kizimkazi Mkunguni, Kibuteni, kizimkazi Dimbani na maeneo ya jirani ndio utatumika kama kiwango sahihi cha ubora kitakachotumika katika ujenzi wa vituo vingine vitakavyoendelea kujengwa visiwani Zanzibar.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Unguja na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation, Bi Wanu Hafidh Ameir alisema ujenzi wa kituo hicho cha afya kwa kiasi kikubwa utasaidia kusogeza huduma za afya kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo hususani wanawake ambao wengi wao walikuwa wanahofia kubeba ujauzito kutoka na huduma za afya kuwa mbali na makazi yao.

“Baada ya ujio wa kituo hiki naamini sasa wanawake wa eneo hili mtaongeza kasi ya kuzaa kwa kuwa idadi ya watoto waozaliwa eneo hili ipo chini sana ikilinganishwa na maeneo mengine,’’ alisema Bi Wanu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw Theobald Sabi alisema ushiriki wa benki hiyo kwenye mradi huo ni muendelezo wa jitihada zake kupitia sera yake ya Uwajibikaji kwa Jamii (Citizenship), ambapo benki hiyo imeeendelea kutenga sehemu ya faida yake kila mwaka ili kusaidia kutatua changamoto mbalimbali katika sekta za afya, elimu, mazingira, elimu ya fedha, na ajira.

“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Benki ya NBC imetoa zaidi ya shilingi bilioni 4 kwa jamii. Leo, tunapozindua Kituo hiki cha Afya cha Kizimkazi, tunajivunia kuwa miongoni mwa wadau wakubwa waliofanikisha ujenzi wa kituo hiki muhimu. Tumechangia kiasi cha shilingi milioni 400 katika ujenzi wa kituo hiki ambacho kitaleta ahueni kubwa katika upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wakazi wa Kizimkazi na maeneo jirani wakiwe wakina mama na watoto’’ alisema Sabi

Zaidi, Sabi alisema benki hiyo imejipanga kuweka mfumo maalum wa malipo ya kidijitali katika kituo hicho cha afya utakaojumuisha Mashine ya kutolea fedha (ATM) na Mashine za malipo kwa kadi (Point of Sale – POS) ili kuongeza ufanisi na urahisiwa malipo kwa wagonjwa na watendaji wa kituo hicho.

Kwa upande wake Mhandisi Kara, alisema nia ya Taasisi ya Samia Foundation ni kuhakikisha miradi kama hiyo inatekelezwa zaidi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

No comments:

Post a Comment