Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Friday 25 October 2024

MTANZANIA ACHAGULIWA KUWA MKURUGENZI MTENDAJI BENKI YA DUNIA

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (kulia), akimpongeza Dkt. Zarau Wendeline Kibwe, kwa kuchaguliwa na Benki ya Dunia kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki hiyo atakayesimamia Kanda Namba Moja ya Afrika, inayojumuisha nchi 22 ikiwemo Tanzania, nafasi ambayo Tanzania imewahi kuihudumu miaka 54 iliyopita kupitia kwa Mtanzania mwingine, Bw. Christopher Kahangi, kati ya mwaka 1968 – 1970. Tukio hilo limetangazwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Benki ya Dunia wa Kanda Namba Moja ya Afrika, uliofanyika wakati wa Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa - IMF na Benki ya Dunia inayofanyika Jijini Washington D.C, nchini Marekani.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (katikati), akiwa na Viongozi wengine, Waziri wa Fedha wa DRC- Congo, Mhe. Nicolas Kazadi (wa tatu kulia), Waziri wa Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum (wa tatu kushoto, Balozi wa Tanzania-Marekani, Mhe. Dkt. Elsie Kanza (kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha- Dkt. Natu El-maamry Mwamba (wa pili kulia), Mkurugenzi Mtendaji anayesimamia Kanda Namba Moja ya Afrika, aliyemaliza muda wake, Dkt. Floribert Ngaruko (kulia) akiwa katika picha na Mkurugenzi Mtendaji Mpya wa Kundi hilo la Kanda namba Moja ya Afrika ya Benki ya Dunia kutoka Tanzania, Dkt. Zarau Wendeline Kibwe (wa pili kushoto), baada ya kutangazwa rasmi katika Mkutano wa Mwaka wa Kanda hiyo kushika wadhifa huo, Jijini Washington D.C, nchini Marekani.

Mkurugenzi Mtendaji Mpya wa Kundi la Kanda Namba Moja ya Afrika ya Benki ya Dunia kutoka Tanzania, Dkt. Zarau Wendeline Kibwe (katikati) akiwa katika Mkutano wa Kanda Namba Moja ya Afrika, uliomuidhinisha kushika wadhifa huo mkubwa, uliofanyika makao Makuu ya Benki ya Dunia, Jijini washington D.C, nchini Marekani. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji anayesimamia Kanda Namba Moja ya Afrika, aliyemaliza muda wake, Dkt. Floribert Ngaruko na kushoto ni Waziri wa Fedha wa DRC-Congo, Mhe. Nicolas Kazadi.






Na Benny Mwaipaja, Washington D.C.

Benki ya Dunia, imemchagua Mtanzania, Dkt. Zarau Wendeline Kibwe, kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki hiyo atakayesimamia Kanda Namba Moja ya Afrika inayojumuisha nchi 22 ikiwemo Tanzania, nafasi ambayo Tanzania imewahi kuihudumu miaka 54 iliyopita.

Uamuzi wa Dkt. Kibwe kuikwaa nafasi hiyo nyeti katika Taasisi hiyo kubwa ya Fedha Duniani, umetangazwa katika Mkutano wa Mwaka wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Benki ya Dunia, uliofanyika Jijini Washington D.C, nchini Marekani ambapo Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha Duniani IMF na Benki ya Dunia inafanyika.

Kabla ya kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki hiyo atakayesimamia Kanda Namba Moja ya Afrika, Dkt. Kibwe alihudumu katika Ofisi hiyo ya Bodi kama Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Mshauri na Mshauri Mwandamizi kwa zaidi ya miaka saba, tangu mwaka 2017.

Akizungumza Jijini Washington D.C, baada ya kutangazwa kuchukua nafasi hiyo, Dkt. Zarau Wendeline Kibwe amesema kuwa ataitumia nafasi hiyo kusimamia uendeshaji wa Benki na Taasisi zake Pamoja na kutetea Maslahi ya nchi katika Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia pamoja na maslahi ya Kanda ya Afrika anayoisimamia ili kukuza maendeleo na uchumi wa nchi hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali katika Mkutano huo uliomtangaza Dk. Kibwe kuchukua nafasi hiyo, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anayeongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mikutano hiyo ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF na Benki ya Dunia, amesema kuwa hayo ni matokeo ya juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anavyoifungua nchi na kukuza Diplomasia ya Kimataifa.

Dkt. Nchemba amempongeza Dkt. Kibwe kwa kupata nafasi hiyo na kwamba kutokana na umahili wake katika masuala ya uchumi na fedha, pamoja na uzoefu wake wa muda mrefu katika Ofisi hiyo, anaamini kuwa maslahi ya nchi yataendelea kulindwa ipasavyo kwa manufaa ya watanzania.

Dkt. Zarau Wendeline Kibwe ni mchumi wa kitanzania ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia kwa Kanda Namba Moja ya Afrika inayojumuisha nchi za Botswana, Burundi, Eritrea, Eswatini, Ethiopia, Gambia, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Shelisheli, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Uganda, Zambia, na Zimbabwe.

Kabla ya kujiunga na Ofisi ya Bodi, Dkt Kibwe alihudumu kama Mchumi wa Benki ya Dunia kwa Tanzania ambapo katika kipindi cha miaka 15 ya kazi yake, Dkt. Kibwe amehudumu katika Serikali ya Jamhuri wa Muungano katika nafasi mbalimbali ikiwemo ya Mchambuzi Mwanadamizi wa Sera (Ofisi ya Rais – Tume ya Mipango), Mhadhiri Msaidizi (Chuo Kikuu Dodoma), Afisa Forodha Msaidizi (Mamlaka ya Mapato Tanzania), na Mhadhiri Msaidizi (Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere).

Dkt. Kibwe ana Shahada ya Uzamivu (Ph.D.) katika Uchumi wa Maendeleo, Shahada ya Uzamili (MA) katika Uchumi wa Maendeleo, na Shahada ya Umahiri katika Sera za Umma, zote kutoka Taasisi ya Taifa ya Mafunzo ya Sera (GRIPS) huko Tokyo, Japani.
Alipata Shahada yake ya Kwanza ya Sayansi katika Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe kilichopo Morogoro, Tanzania.

No comments:

Post a Comment